Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Halima Dendego akisisitiza juu ya utekelezaji wa Mpango wa Kujiandaa kukabili Maafa Mkoani Mtwara wakati wa uzinduzi wa mpango Mkoani Mtwara, kushoto kwake ni Mkurugenzi Idara ya Uratibu Shughuli za Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Brig.Jen Mbazi Msuya.
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Halima Dendego akikabidhi Mpango wa Kujiandaa kukabili Maafa Mkoani Mtwara kwa Mkuu wa Wilaya ya Masasi Mhe. Bernard Nduta wakati wa uzinduzi wa mpango huo, Mkoani Mtwara.
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Halima Dendego (waliokaa katikati) akiwa na wajumbe wa kamati za maafa za Halmashauri za Mtwara Mikindani mara baada ya kuzindua Mpango wa Kujiandaa kukabili Maafa Mkoani Mtwara Mkoani Mtwara, (wapili kulia waliokaa) ni Mkurugenzi Idara ya Uratibu Shughuli za Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Brig. Jen Mbazi Msuya.
---
Na Mwandishi Maalum.

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Halima Dendego amezitaka Halmashauri za mkoani humo kupunguza utegemezi wa rasilimali za kukabili maafa kutoka kwa wafadhili wa nje badala yake zitumie rasilimali zilizopo mkoani humo katika kujenga uwezo wa kukabili maafa kwa kulipa kipaumbele suala la Kupunguza Athari za Maafa katika mipango na programu za maendeleo.

Akiongea wakati wa uzinduzi wa Mpango wa Kujiandaa Kukabili Maafa Mkoani Mtwara ulioandaliwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya uratibu wa shughuli za maafa, tarehe 24 Aprili, 2015, mkoani Mtwara, Dendego alibainisha kuwa Halmashauri zinaweza kupunguza utegemezi wa rasilimali za kukabili maafa, kwa kuondokana na mtazamo wa kukabili maafa uliozoeleka ambao unatenganisha kwa kiasi kikubwa hatua za utoaji wa misaada ya kibinadamu, kurudisha hali na shuguli za kawaida za maendeleo.

“Majanga ya mafuriko, Ukame, na mlipuko wa kipindupindu yamekuwa yakizisumbua Halmashauri zetu mara kwa mara. Tunaweza kutumia rasilimali zetu kukabili majanga haya badala ya kutegemea wafadhili wa nje, kwa kutumia rasilimali zetu tunaweza kutoa elimu kuhusu athari za ujenzi na kuendesha shughuli za uchumi katika maeneo hatarishi, umuhimu wa usafi wa mazingira matumizi ya mbegu zinazostahimili ukame pamoja na kuzuia ujenzi katika maeneo hatarishi” alisema Dendego.

Aliongeza kuwa, Upunguza Utegemezi wa rasilimali za kukabili maafa unawezekana kwa kuwa na jamii yenye kuhimili maafa kwa Kuzuia, kupunguza athari na kujiandaa kama vipaumbele katika menejimenti ya maafa katika ngazi zote. Ili kuhakikisha kunakuwa na jamii hiyo, kila Halmashauri inapaswa kukaa na wadau wote katika halmashauri husika na kuainisha maeneo ya kushughulikia kwa haraka na kuwa na mgawanyo bayana wa majukumu.

“Juhudi za jamii ni nguzo muhimu katika kujiandaa kukabili maafa, juhudi hizo zinajumuisha kuainisha na kutekeleza hatua zinazoweza kuchukuliwa kujiandaa kukabiliana na maafa yanayoweza kutokea ghafla kama mafuriko na yale yanayochukua muda mrefu na wa kati kama ukame na janga la mabadiliko ya tabia nchi” alisema Dendego.

Awali akiongea katika uzinduzi huo Mkurugenzi Idara ya Uratibu Shughuli za Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Brig.Jen Mbazi Msuya alifafanua kuwa kuandaliwa kwa mpango huo ni jitihada zinazochukuliwa na serikali za kujenga uwezo katika ngazi za Halmashauri kukabiliana na maafa.

“kama inavyoeleweka nchi yetu imekuwa ikikumbwa na majanga yakiwemo ya asili na yanayosababishwa na vitendo vya binadamu. Katika kukabili maafa hayo yamekuwa yakijitokeza mapungufu ikiwemo kutokuwepo mipango madhubuti iliyoandaliwa ya kukabiliana na maafa mara yanapotokea” alisema Msuya.

Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Uratibu wa Shughuli za Maafa kupitia Ufadhili wa Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF), tayari imeshaandaa na kufanya uzinduzi wa Mipango hiyo katika mikoa mitano na kufanya zoezi la mezani la utekelezaji wa mipango hiyo kwa Halmashauri zake; Mikoa hiyo ni; Dodoma, Shinyanga, Simiyu, Kilimanjaro na Mtwara.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: