Akizungumza wakati wa mkutano rasmi kati yake na mwenyeji wake, Mhe. Edgar Lungu, Rais wa Zambia, Rais Kikwete alisema kuwa umefika wakati sasa wa kuifufuA Reli ya TAZARA ambayo ni kiungo muhimu na alama kubwa ya ushirikiano kati ya Tanzania na Zambia.
Mhe. Rais Kikwete alifafanua kuwa umuhimu wa reli hiyo ni wa kihistoria ambao unahusisha nchi tatu za Tanzania, Zambia na Jamhuri ya Watu wa China ambao kwa kiasi kikubwa walichangia ujenzi wa reli hiyo.
Aidha, aliongeza kuwa Tanzania na Zambia zimekubaliana kuwekeza zaidi katika reli hiyo ikiwemo kuboresha uendeshaji na ukarabati ili kuirejesha katika hali yake ya awali na hatimaye kukuza biashara na uwekezaji.
Alifafanua kwamba hapo awali reli hiyo iliweza kusafirisha tani zaidi ya milioni 2 za bidhaa kwa mwaka wakati sasa reli hiyo inasafirisha tani laki 2 kwa safari inayotumia hadi siku 12 kutoka Dar es Salaam hadi New Kapiri Mposhi wakati malori yanatumia siku tano pekee.
“TAZARA inapita katika kipindi kigumu sasa, hivyo tumezungumza namna ya kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili ikiwemo uendeshaji na ukarabati ili irejee katika hali yake ya awali”, alisisitiza Rais Kikwete.
Katika hatua nyingine Mhe. Rais Kikwete alimpongeza Rais Lungu kwa kuchaguliwa hivi karibuni kuwa Rais wa Zambia na pia alitoa salamu za pole kwa Rais huyo na Wazambia wote kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Hayati Michael Satta.
Kwa upande wake, Rais Lungu alisema kuwa Tanzania na Zambia zinajivunia mafanikio ya ushirikiano yaliyopo baina ya nchi hizi mbili ambayo yamejikita katika sekta za Kilimo, Usafirishaji, Nishati na Mawasiliano.
Pia, alisema kwamba nchi yake ipo tayari kuimarisha ushirikiano wa kihistoria uliopo ambao unaanzia ngazi ya serikali, kanda, Bara na Kimataifa na kusisitiza umuhimu wa kuitumia Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) ambayo ilianzishwa rasmi mwaka 1992 kwa ajili ya kusimamia utekelezaji wa makubaliano mbalimbali yanayofikiwa na nchi hizi mbili. Aidha, alikubaliana na hoja ya kuifufua reli ya TAZARA kwa manufaa ya nchi hizi mbili.
Rais Kikwete ambaye alikuwa nchini humo kwa mwaliko wa Rais Lungu alifuatana na Mama Salma Kikwete, Mhe. Bernard Membe, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Saada Mkuya Salum, Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Charles Tizeba, Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Abbas Kandoro, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Grace Mujuma, Balozi wa Tanzania nchini Zambia na Viongozi Waandamizi kutoka Serikalini na Mamlaka mbalimbali.
Toa Maoni Yako:
0 comments: