Waziri wa Habari Utamaduni Utalii na Michezo Said Ali Mbarouk akitoa hotuba.
---
Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar.
WIZARA Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo imeeleza kuwa katika sekta ya habari mafanikio makubwa yamefikiwa katika utekelezaji wa malengo ya kila siku ambayo yamesaidia kukuza sekta hiyo hapa nchini.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Utaili na Michezo Mhe. Said Ali Mbarouk aliyasema hayo wakati akitoa taarifa ya Utekelezaji Mpango Kazi wa Wizara hiyo kwa kipindi cha Julai 2014 hadi Disemba 2014 katika Mkutano kati ya Wizara hiyo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, Ikulu mjini Zanzibar.
Waziri Mbarouk alisema kuwa taasisi zilizopo kwenye sekta ya habari zina majukumu mbali mbali ikiwa ni pamoja na kusimamia vyombo vya Habari vya Serikali na vya binafsi, kutoa vibali kwa waandishi wa habari, kutoa taarifa, mafunzo, ushauri na taaluma ya uandishi wa habari, kuelimisha pamoja na kuburudisha.
Aidha, alisema kuwa sekta hiyo imekuwa na jukumu la kukemea na kuhamasisha jamii juu ya masuala ya kiuchumi, kijamii, kisiasa pamoja na kushiriki katika utekelezaji wa mipango mbali mbali ya Serikali.
Alisema kuwa pamoja na mafanikio yaliopo pia, kuna changamoto zinazozikabili sekta hiyo ambazo zinahitaji kufanyiwa kazi ili malengo ya sekta hiyo yaweze kufikiwa katika utekelezaji wake.
Kwa upande wa sekta ya Utalii, Waziri Mbarouk alisema kuwa sekta hiyo imefanikiwa kwa kiasi kibwa katika kutekeleza maklengo yake ambayo yamepelekea kuongeza kwa idadi ya watalii wanaokuja kutembelea Zanzibar ambao hutoa ajira kwa wananchi pamoja na kuchangia kiasi kikybwa cha pato la nchi.
Akieleza juu ya sekta ya Utamaduni na Michezo, Waziri Mbarouk alisema kuwa taasisi zilizomo kwenye sekta hiyo zimepewa jukumu la kusimamia, kuratibu na kukuza shughuli za utamaduni na michezo, kuenzi, kuhifadhi na kuendeleza histroria ya Zanzibar pamoja na kushajiisha matumizi sahihi ya Kiswahili ndani na nje ya Zanzibar.
Nae Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein kwa upande wake alitoa pongezi kwa uongozi na watendaji wote pamoja na Wenyeviti wa Bodi mbali mbali zilizomo ndani ya Wizara hiyo kwa kazi nzuri waliyoifanya katika utekelezaji wa malengo yao ndani ya miezi sita iliyopita na kusisitiza kuongeza kasi zaidi katika utekelezaji wa malengo wanayojiwekea ili waweze kupata mafanikio zaidi.
Akiendelea kukutana na viongozi wa Mawizara ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk. Shein alifanya mkutano na uongozi wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais katika kuelezea juu ya Utekelezaji wa Mpango Kazi wa Ofisi hiyo kwa robo mbili kati ya Julai hadi Disemba kwa mwaka wa fedha 2014/2015, huko Ikulu mjini Zanzibar.
Akitoa taarifa ya Utekelezaji wa Mpango Kazi wa Ofisi hiyo kwa kipindi hicho, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mhe. Mohamed Aboud Mohamed alitoa shukurani kwa Dk. Shein kwa niaba ya uongozi na wafanyakazi wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais kwa kutumia hekima, busara na uadilifu katika kuwatumikia wananchi wa Zanzibar.
Waziri Aboud alisema kuwa mbali na hatua hizo Dk. Shein amekuwa akifanya juhudi za kuwaletea maendeleo ya kiuchumi, kisiasa na kijamii wananchi wa Zanzibar na kuyafanya maisha yao kuwa bora siku hadi siku.
Aidha, Waziri Aboud alisema kuwa Ofisi hiyo inaendelea kufarajika sana na uongozi wa Dk. Shein katika kusimamia na kuyatolea maamuzi mambo mbali mbali yanayohusu Zanzibar kwa maslahi ya wananchi.
Pamoja na hayo, Waziri huyo alisema kuwa uongozi wa Dk. Shein umekuwa ukiwasaidia sana wasimamizi wa shughuli za Serikali kwani utekelezaji katika Taasisi za Serikali unaonesha mabadiliko na kuelekea katika utendaji wenye ufanisi na kuongeza tija.
Akieleza Dira ya Ofisi hiyo, Waziri Aboud alisema kuwa ni kuwa na Serikali yenye kutoa huduma bora kwa jamii na yenye uhimili mzuri wa uchumi, umoja na maendeleo endelevu.
Aidha, alisema kuwa dhamira ya Ofisi hiyo ni kuratibu na kusimamia utekelezaji wa shughuli za Serikali katika sekta zote za SMZ na mambo ya Muungano kwa kufuata misingi ya katiba, sheria na taratibu, pamoja na kuhakikisha kufuata misingi ya haki za binaadamu na ushirikishwaji.
Kwa upande wake Dk. Shein alitoa pongezi kwa Ofisi hiyo kwa kufanya vizuri katika utekelezaji wa Mpangokazi wake kwa kipindi cha miezi sita pamoja na kufanya kazi vizuri kwa kumsaidia Makamu wa Pili wa Rais katika kufanya kazi.
Nae Makamu wa Pili wa Rais Mhe. Balozi Seif Ali Idd alitoa shukurani kwa viongozi na watendaji wote wa Ofisi hiyo kwa ushirikiano wanaompa katika kutekeleza majukumu ya kazi zake.
Toa Maoni Yako:
0 comments: