Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.
Jovago imetangaza leo kwamba imeingia katika ushirikiano na Tigo Tanzania, kampuni ya simu inayoongoza nchini. Katika ushirikiano huu, wateja wa Tigo Pesa sasa wataweza kulipia malazi yao kupitia akaunti zao za Tigo Pesa. Hii inakuja wakati muafaka ambapo muingiliano wa malipo ya pesa kupitia simu za mkononi katika tovuti za intanet umeonekana kama kiungo muhimu katika ukuaji wa sekta ya utalii katika mitandao.
Huu ni ushirikiano wa pili kwa utoaji huduma ya malipo ya mtandao wa simu katika sekta hii ya kufanya booking. Ushirikiano huu unaruhusu watumiaji uhakika na urahisi zaidi wa kupata malazi kwa njia ya mtandao.
Mtandao unaoongoza barani Afrika kwa kufanya booking za hoteli na malazi www.Jovago.com umetangaza ushirikiano na Tigo Pesa, moja ya huduma za kutuma na kupokea fedha zinazoongoza katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati. Ushirikiano huu unawapatia fursa nyingine wateja kupata huduma yenye ufanisi zaidi tofauti na ulipaji uliozoeleka wa kulipa kwa kadi na kulipa kwa fedha taslimu papo kwa papo.
“Hakika bara la Afrika sasa linaelekea katika ulimwengu wa kidijitali, ni kwa sababu hiyo tunataka kujumuisha mahitaji ya soko na mienendo yake, na hivyo kutengeneza mikakati yetu kutokana na mahitaji hayo,” alisema Mkurugenzi Mkuu, Estell Verdier.
Tigo Pesa ni huduma ya kwanza Afrika Mashariki iliyoanzisha App yake mahususi na iliyowezesha utumiaji na upokeaji wa fedha kutoka nchi moja na nyingine yenye uwezo wa kubadilisha ankara ya fedha moja kwa moja kwenye akaunti ya mteja na kuepusha haja ya kwenda kubadili fedha kwenye masoko ya ubadilishaji fedha. Ni dhahiri kwamba maendeleo mengi makubwa yanatokea katika teknolojia ya simu za mkononi.
Mkuu wa Idara ya kutuma na kupokea fedha kutoka Tigo, Ruan Swanepoel alisema, “Tunayo furaha kushirikiana na Jovago kuwapatia wateja wetu urahisi wa kulipia kwa usalama malazi yao ya hoteli kupitia simu zao za mkononi. Kulipia kwa Tigo Pesa ni namna rahisi ya kusafiri.
Verdier pia alisema kwamba ukiondoa urahisi watakaopata wateja kupitia njia hiyo ya malipo, Jovago kwa sasa pia wanatoa orodha kubwa zaidi ya hoteli barani Afrika ambapo mteja anaweza kuchagua na vilevile wanazungumza na hoteli hizo kwa niaba ya wateja kuhusu punguzo za bei, ili wateja waweze kupata sehemu ya malazi mazuri na kwa bei nzuri zaidi.
Ni muhimu pia kutambua kwamba katika robo ya mwisho ya mwaka wa 2014, ukuaji wa huduma za simu Tanzania umeongezeka kwa kiasi cha asilimia 2.8 kutoka asilimia 2.0 ya awali. Tanzania kwa sasa ina jumla ya watumiaji wa simu za mkononi milioni 28, ambayo ni takribani asilimia 63 ya watu wote.
Kutokana na ripoti ya World Tourism, Afrika Mashariki ni kanda yenye mafanikio na maarufu kwa matumizi ya malipo kwa njia ya simu za mkononi, Kenya ikiongoza kwa asilimia 80 katika kundi la watu wazima wanaofanya hiyo miamala.
Kwa kumalizia, Verdier pia alisema kwamba kwa sasa zaidi ya asilimia 30 ya wanaotembelea www.jovago.com wanatumia simu zao za mkononi. Katika muktadha huu malipo ya simu za mkononi ni kiungo muhimu sana katika ukuaji wa sekta hii.
Hii si mara ya kwanza kwa kampuni hizi mbili kushirikiana, Jovago.com na Tigo Pesa hapo awali wameshashirikiana katika mradi wa UNICEF Passport to Life yenye malengo ya kumpatia kila mtoto wa kiafrika cheti cha kuzaliwa. Wakati wa kufanya booking Jovago, wateja wanapewa nafasi ya kutoa mchango kwa mradi huu wa usajili wa uzazi (dola 5 kwa booking ambaye inaenda kwa UNICEF) bila malipo yoyote ya ziada.
Toa Maoni Yako:
0 comments: