Mkurugenzi wa Kitengo cha Kuzuia Dawa za Kulevya, Kamishna Mwandamizi wa Polisi (SACP), Godfrey Nzowa.

Na Mwandishi Wetu, Gazeti la Mwananchi.

Magareza mbalimbali ya China, Hong Kong na Macau yamefurika Watanzania wanaojihusisha na dawa za kulevya.

Wanakuja kwa makundi. Wake kwa waume, vijana kwa wazee, wenye elimu na historia tofauti za kimaisha... lakini kilichowaleta China, Hong Kong na Macau ni kimoja tu; biashara ya dawa za kulevya.

Hawa ni zaidi ya Watanzania 130 ambao wamefungwa katika magereza mbalimbali kwenye nchi za China, Hong Kong na Macau.

Ingawa wanadai kupata mlo mzuri, mahali pazuri pa kulala na fursa kadhaa katika magereza, lakini bado wamekosa kitu kimoja muhimu duniani; uhuru.

Faraja wanayoitegemea ni ya Mchungaji John Wootherspoon, raia wa Australia anayeishi China ambaye amepata kibali cha kutembelea magereza mbalimbali.

Wafungwa wa Kitanzania wapo katika magereza mbalimbali kama Shek Pik, Stanley, Loo Woo na Macau.

Fursa ya kukutana na wafungwa ilikuwa ndicho chanzo cha Wootherspoon kuona kuwa kuna idadi kubwa ya Watanzania katika magereza kuliko hata idadi ya wazawa wenyewe.

“Kila mwezi Watanzania wanne hadi sita walikuwa wakiingia magerezani na wengine wengi wakiwa rumande kwa makosa mbalimbali,” anasema

Wootherspoon ana kazi moja kubwa katika magereza hayo, ambayo ni kuwafariji kwa neno la Mungu.

“Ninapata nafasi ya kukaa nao kila siku na ninapowasikiliza, nimegundua kuwa wanajuta na wametumiwa tu na watu wenye ufahamu na biashara hiyo,” anasema

Wootherspoon, ambaye yupo nchini kwa sasa, anasema kuwa anachotaka ni kuwakataza vijana wengine kwenda China kwa kusafirisha dawa za kulevya.

Ujumbe wa majonzi kwa ndugu za wafungwa

Baada ya kuona hali imekuwa mbaya, Wootherspoon aliamua kuja Tanzania ili angalau awasaidie wafungwa hao kuwasiliana na familia zao. Kitabu maalum kidogo kilitayarishwa kwa kila mfungwa kuandika ujumbe kwa baba, mama, dada, kaka mume au mke. Ilikuwa ni lazima kila mfungwa aweke namba ya simu ili ujumbe uwafikie walengwa kule waliko. Januari Mosi, 2015, mchungaji huyo anatua na ujumbe huo katika ardhi ya Tanzania.

Haikuwa kazi rahisi kwa ndugu na jamaa za wafungwa hao kupokea ujumbe huo katika hali ya kawaida.

Siku ya kwanza, familia ya mfungwa wa kike ambaye alijifungua mtoto wa kiume akiwa gerezani, anafikishiwa na ujumbe.

Akibubujikwa machozi mama wa mfungwa huyo anasema hajawahi kudhani kuwa binti yake anaweza kusafirisha dawa za kulevya.
“Aliniaga kuwa anasafiri kibiashara kwa sababu alikuwa na duka la viatu, lakini katu sikudhani anayafanya hayo,” anaeleza mama huyo. Mzazi huyo, ambaye haikuwa rahisi kumbembeleza, anasema kuwa binti yake mwenye umri wa miaka 30 tu alikuwa ndiyo nguzo ya familia.

Msichana huyo ambaye amehukumiwa kifungo cha miaka 14 kwenye gereza la Loo Woo, China, ameiacha familia yake ikigubikwa na umaskini wa hali ya juu.

“Ameniachia watoto wawili, sina kazi wala biashara, watoto wanahitaji kusoma,” anasema
Ujumbe mwingine mrefu kutoka kwa mfungwa mwingine Hong Kong ulimfikia mama yake ambaye sambamba na umaskini, anaishi na Virusi vya Ukimwi.

“Mama najua unaumwa na nimekuachia mtoto, nisamehe sana lakini uniombee. Nilifanya hivi ili tuondokane na umaskini,” anasema katika ujumbe wa binti huyo kwa mama yake.
Mama wa mfungwa anaposoma ujumbe huo naye anaangua kilio mithili ya msiba.

“Amefungwa miaka yote hiyo, acheni nilie unadhani hadi atakapoachiwa nitakuwa hai?” analia mama huyo.

Kila mfungwa ana hadithi yake ya kimaisha lakini ilibainika kuwa wengi wanafanya hivyo kwa sababu za umaskini.

Kwa mfano, mfungwa mmoja aliandika ujumbe kwa mama yake, lakini akimweleza kuwa hali yake ya kiafya si nzuri kwani anaumwa.

Wootherspoon anamweleza mama wa mfungwa huyo kuwa binti yake amelazwa kwa wiki tatu na hali yake si nzuri.

Wafungwa wengine ni wasomi

Ujumbe mwingine kutoka kwa mfungwa mwanaume ulitumwa kwa mke wake. Yeye, katika ujumbe huo, anatubu kwa mke wake kuwa amefanya kosa lililomgharimu uhuru wake na furaha ya kukaa na familia yake. Mke wa mfungwa huyo baada ya kusoma ujumbe huo anaeleza kuwa anashangazwa na uamuzi wa mume wake kufanya biashara hiyo wakati ni msomi mwenye shahada.

“Ameniachia watoto watatu, wote wanataka ada za shule, wanataka kula, kuvaa. Yaani ninaishi maisha magumu mno hadi nafanya vibarua,” anasema.

Ujumbe mwingine wa matumaini unatoka kwa kijana wa miaka 27 ambaye anakiri kuwa aliwahi kukanywa na wazazi asifanye hivyo lakini alikaidi kwa kuwa mara ya kwanza alipofanya hivyo nchini Italia, alifanikiwa.

“Baba ulinikataza, lakini niliona itakuwa kazi rahisi kama nilivyofanya mwanzo. Nakupenda sana na mniombee nitoke salama. Msiwe na wasiwasi mimi mzima wa afya,” ameandika mfungwa huyo katika ujumbe aliotuma kwa baba yake.

Waliobeba mimba kama mbinu ya kusafirisha ‘unga’

Katika ujumbe huu kutoka China, Hong Kong na Macau, ndipo ilipobainika kuwa baadhi ya wasichana walitumia mbinu ya kubeba ujauzito ili kusafirisha kirahisi dawa za kulevya.
Mbinu hiyo ilifanyika hivi...

Baada ya mimba kufikisha miezi minne au mitano, ndipo msichana humeza kete za dawa za kulevya.

Kwa kuwa kipimo cha kujua iwapo mtu amemeza kete za dawa za kulevya ni X Ray, na wajawazito hawapimwi kwa njia ya mionzi, wanawake hao hupita bila kukaguliwa.

Hata hivyo wafungwa hao hawakujua kuwa mbinu hiyo hujulikana katika nchi nyingine, hali iliyosababisha wakamatwe.

Mjamzito anaweza kumeza kete hadi 30 na baadaye huzitoa kwa njia ya haja kubwa.

Lakini akiwa njiani hatakiwi kula chochote ili kuepuka kuzitoa kete hizo kwa njia ya kinywa au haja kubwa.

Kamishna wa polisi wa Kitengo cha Dawa za Kulevya, SACP Godfrey Nzowa anasema hapa nchini wapo raia wa kigeni ambao walitumia njia hiyo, lakini walikamatwa .

Nzowa anasema wanawake hao baadhi wameshazaa watoto ingawa mmoja wa watoto waliozaliwa amepata mtindio wa ubongo.

Alibeba ‘unga’ ili apate fedha ya matibabu ya mtoto

Baadhi ya wafungwa imebainika kuwa hushawishika kubeba dawa za kulevya kutokana na hali mbaya ya kiuchumi waliyonayo.

Kwa mfano ujumbe wa mfungwa mwingine unaeleza kuwa, aliamua kukubaliana na magwiji wa kuuza dawa za kulevya ili tu apate fedha za matibabu ya moyo ya mtoto wake nchini India.

“...Mtu mmoja ambaye ni rafiki yangu wa karibu alisema anataka anisaidie kwa njia hiyo, kwa hiyo akanipeleka kwa (jina linahifadhiwa), na akaniambia nikiufikisha Hong Kong nitapata Sh 25milioni...nikajua nikifanya hivyo nitapata milioni 11 ninazotakiwa kulipa ili binti yangu aende Apollo,” unasema ujumbe huo.

Haikuwa rahisi kwa mke wa mfungwa huyu kusoma ujumbe mrefu kutoka kwa mume wake.

Kabla hata hajaelezwa kuhusu hali ya mume wake, alianza kulia na baada ya kuusoma anaangusha kilio zaidi.

Licha ya kujuta na kueleza hisia zao, wengi walionyesha kukumbuka mila na tamaduni zetu kama vile vyakula, muziki wa kizazi kipya na muziki wa dini.

Wanauza chakula gerezani kujipatia fedha

Baadhi ya wafungwa wa Tanzania katika magereza hizo wanasoma na wengine kuuza chakula ili kujipatia kipato.

Ili kujipatia fedha wameamua kuuza mlo wao wa mchana wanaogawiwa gerezani hapo kwa raia Hong Kong au China na wazungu.

Kwa kawaida katika magereza hayo, kuna milo mitatu, asubuhi, mchana na usiku hivyo wafungwa wa kike huuza mlo wa mchana kwa wafungwa wenzao ambao hawatosheki na sahani moja huuzwa kwa Dola 2 ya Hong Kong ambayo ni sawa na Sh 3,460.

“Hapa magereza tunakula mara tatu kwa siku, lakini ili kujipatia fedha tunawauzia chakula chetu mara nyingi cha mchana wafungwa wengine ambao wanaona chakula wanachopewa ni kidogo na hakiwatoshi,” alisema mfungwa mmoja kupitia barua aliyoituma.

Watanzania hao wanazitumia fedha hizo kununulia vitu vidogo vidogo kama sigara, mafuta ya kujipaka na baadhi wanazihifadhi na kuwatumia ndugu zao nchini.

Wootherspoon anasema wanaofanya biashara ya chakula gerezani wengi ni wafungwa wa kike na wakati wafungwa wanaume wao huuza chakula chao mara chache.

“Chakula chao mara nyingi ni wali na kipapatio cha kuku, au makaroni na kunde, lakini mara nyingi wafungwa hao huuza mlo wao wa mchana,” anasema Wootherspoon.

Wafungwa hao wanaeleza zaidi kuwa siku za sikukuu kama Christmass, wanapewa wali na mapaja ya kuku.

Wafungwa wanaonunua chakula hupata fedha zinazoingizwa kwenye akaunti ya magereza na ndugu zao.

Fedha inakuja kwa jina la mfungwa anayenunua chakula na baadaye mchakato hufanywa wa kuzihamisha kwenda kwenye akaunti ya mfungwa anayeuza.

Pamoja na kuuza chakula, wafungwa hao wengi wanasoma masomo mbalimbali ikiwemo, lugha za Kiingereza, Kichina, kutengeneza viatu, kushona, kutengeneza kompyuta na ufugaji.

Akizungumza kuhusu maisha ya wafungwa hao magerezani Mkuu wa Kitengo cha Habari cha Wizara ya Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa, Mkumbwa Ali, anasema uamuzi wao wa kusoma ni jambo jema hasa wakati wanapokuwa kwenye wakati mgumu kama walio nao.

“Kama wanasoma wanafanya jambo zuri badala ya kutoka gerezani wakiwa hawana chochote,” anasema
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: