Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utawala Bora Mhe. George Mkuchika, (katikati) akiwa na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Prof. Mussa Juma Assad (kushoto) pamoja na wajumbe wengine wakiimba wimbo wa wafanyakazi wakati wa Mkutano wa Pili wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi uliofanyika jana katika Ukumbi wa Hoteli ya Naf Beach iliyoko mkoani Mtwara.

 Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali Prof. Mussa Juma Assad akisoma hotuba ya kumkaribisha mgeni rasmi wakati wa Mkutano wa Pili wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi uliofanyika jana katika Ukumbi wa Hoteli ya Naf Beach iliyoko mkoani Mtwara.
 Mgeni rasmi, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utawala Bora Mhe. George Mkuchika, akiwahutubia wajumbe wa Baraza la Pili la Wafanyakazi wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi muda mchache kabla ya kulifungua baraza hilo jana katika Ukumbi wa Hoteli ya Naf Beach iliyoko mkoani Mtwara.
Wajumbe wa Baraza la Pili la Wafanyakazi wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wakimsikiliza kwa makini Mgeni rasmi, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utawala Bora Mhe. George Mkuchika (hayupo pichani) wakati wa mkutano wa baraza hilo uliofanyika jana katika Ukumbi wa Hoteli ya Naf Beach iliyoko mkoani Mtwara. (PICHA ZOTE NA SARAH REUBEN - OFISI YA TAIFA YA UKAGUZI).

Na Evelyn Thomas - Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi, Mtwara.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utawala Bora Mhe. George Mkuchika (Mb) amefungua mkutano wa Baraza la Pili la Wafanyakazi wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi uliofanyika jana mkoani Mtwara.

Katika mkutano huo, Waziri Mkuchika ameipongeza ofisi hiyo kwa kufanya ukaguzi wenye viwango vya juu na hatimaye kupungua kwa hati chafu au zenye mashaka katika Serikali Kuu na Serikali za Mitaa.

"Mimi binafsi najivunia sana kutokana na jitihada na mafanikio ya kazi za Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi ambayo yameijengea heshima nchi yetu na ulimwengu kwa ujumla, licha ya kupungua kwa hati chafu, hivi sasa Nchi yetu, ikiwakilishwa na Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi, inakagua shughuli za Umoja wa Mataifa jambo ambalo ni la kujivunia sana", amesema Waziri Mkuchika.

Mkuchika ameongeza kuwa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi ni chombo nyeti sana, si hapa Tanzania tu bali katika nchi zote zinazozingatia demokrasia,uwajibikaji na uwazi, katika mapato na matumizi ya rasilimali za umma ili kuleta maendeleo ya watu wake.

Akizungumza wakati wa kumkaribisha mgeni rasmi, Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Prof. Mussa Juma Assad amesema mkutano huo una dhumuni la kutoa fursa kwa watumishi, kupitia wawakilishi wao, kujadiliana juu ya masuala mbalimbali ya msingi yanayohusu tija na ufanisi mahali pa kazi.

" Dhana ya kuwa na Mabaraza ya Wafanyakazi katika sehemu za kazi, hasa katika utumishi wa umma ina lengo la kutoa fursa kwa watumishi, kupitia wawakilishi wao, kujadiliana juu ya masuala mbalimbali ya msingi yanayohusu tija na ufanisi kwa upande mmoja na upande mwingine maslahi yao kama watumishi", amesema Prof. Assad.

Prof. Assad amefafanua kuwa mkutano huu wa Baraza la Wafanyakazi utatumika kujadili malengo na mipango ya Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi ikiwa ni pamoja na Maslahi ya Watumishi kwa ujumla.

Mkutano wa Baraza la Pili la Wafanyakazi wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi utamalizika leo jioni ambapo kaulimbiu ya mwaka huu ni “Weledi na nidhamu katika kutekeleza majukumu ya Utumishi wa Umma ni chachu ya kutoa huduma bora kwa wananchi.”
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: