Askari wa FFU wakizunguka mitaa mbali mbali ya mji wa Iringa jana kama njia ya kulinda amani kwa wafanyabiashara ambao waliendelea kutoa huduma baada ya wenzao kuwa katika mgomo. |
MOja kati ya maduka mjini Iringa yakiendelea kutoa huduma mbali ya wafanyabiashara wengine kuwepo katika mgomo kushinikiza kuachiwa huru kwa mwenyekiti wa wafanyabiashara Taifa Bw Johnson Minja. |
Maduka mtaa wa uhindini mjini Iringa yakiwa yamefungwa jana kuunga mkono mgomo wa wafanyabiashara nchini. |
Wananchi mbalimbali wa mji wa Iringa wakiwa katika soko kuu la mjini Iringa kupata huduma zao wakati sehemu mbali mbali huduma zikiwa zimesitishwa kufuatia mgomo wa wafanyabiashara nchini. |
Na matukiodaimaBlog.
BAADHI ya wafanyabiashara mkoani Iringa jana wamegoma kuungana na
wafanyabiashara wenzao nchini kushiriki mgomo wa kushinikiza jeshi la polisi kumwachia huru mwenyekiti wao wa chama cha wafanyabiashara nchini Bw Johnson Minja anayedaiwa kushikiliwa na jeshi la polisi kwa mahojiano.
Wafanyabiashara hao waliosusia mgomo huo walifikia uamuzi huo kama hatua ya
kupinga uamuzi wa wenzao ambao walifunga maduka yao kwa siku nzima kuungana na wafanyabiashara wa mkoa wa Dar es Salaam ambao walifanya hivyo .
Uchunguzi uliofanywa na mtandao huu wa www.matukiodaima.co.tz katika mitaa mbali mbali ya mji wa Iringa na maeneo ya nje ya mji wa Iringa ulionyesha kuwa mgomo huo kukosa ushirikiano kutokana na baadhi ya maduka ya pembezoni mwa mji wa Iringa na yale ya vijijini na baadhi ya maduka ya katikati ya mji wa Iringa kuendelea na huduma kama kawaida huku wakiomba ulinzi kwa jeshi la polisi ili wao kuendelea kutoa huduma kama kawaida.
Huku cha kushangaza hata baadhi ya salun na bucha za nyama katika baadhi ya maeneo mjini hapa zilifungwa huku baadhi ya maduka yanazozunguka soko kuu la Iringa pia yakifungwa japo katika soko hilo umati mkubwa wa wananchi waliendelea kupata huduma kama kawaida .
Mmoja kati ya wafanyabiashara wa mji wa Iringa Bw JOhn sanga alisema kuwa ameshindwa kuungana na wafanyabiashara wa mji wa Iringa katika mgomo huo kutokana na shinikizo kubwa ambalo lilikuwa likionyeshwa na watu waliokuwa wakisambaza jumbe za mgomo huo juzi na jana kupitia kikundi cha watu kama 11 ambao wengi wao walikuwa wakitoa vitisho wakati wa kusambaza taarifa hizo.
"Kweli nimeshindwa kufunga duka langu leo kutokana na vitisho vya watu hao ambao wanatulazimisha kufunga kwa nguvu huku wakitambua kuwa si kila mfanyabiashara ni mwanachama wa chama chao hicho cha wafanyabiashara ....kutulazimisha kufunga biashara zetu ni kutunyanyasa sisi tusio wanachama na tambua kila mmoja ana maisha yake wao badala ya kukutana viongozi kwa ajili ya kulimaliza suala hilo wanataka wote tufunge maduka huu ni ushauri mbaya kuliko"
Hata hivyo alisema hajaweza kufunga na ataendelea kutoa huduma wakati wote wa mgomo wa wafanyabiashara hao kwani si lazima kila mfanyabiashara kuungana nao katika chama chao na kiongozi wao.
Huku mfanyabiashara Geofrey kalinga akieleza kusikitishwa na serikali kushindwa kuchukua hatua kali kwa kikundi hicho cha wafanyabiashara wachache ambao wanachochea mgomo huo na kuwakosesha wengine amani ya kufungua biashara zao na kuwa kuendelea kuchelewa kuchukua hatua ni kubariki migomo kama hiyo kuendelea.
Kwani alisema ni jambo la kushangaza kuona watu hao wachache wakitumia nguvu kuwazuia wengine kuungana nao katika mgomo huo huku wakitambua kuwa chama hicho ni chama cha hiari kujiunga ama kutojiunga hivyo walipaswa kushughulika na wanachama wao na sio wafanyabiashara wote.
"Haya ni mambo ya ajabu sana hivi inawezekana vipi hiki kikundi cha wachache kutulazimisha wafanyabiashara wote kujiunga na chama chao... sasa leo wanatutaka kufunga biashara kwa muda usiojulikana kesho watakuja na jambo jingine lakini swali la msingi hapa hicho chama chao kinatusaidia nini sisi ambao si wanachama tunapofungiwa biashara zetu ya mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) kwa kuchelewa kulipa kodi....ama wanatusaidia vipi na kodi kubwa ya mapango ya
vyumba vya biashara ambazo tumekuwa tukilipa .....kama jibu hakuna
basi watuache na wao waendelee na migomo yao"
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi wafanyabiashara waliofunga maduka yao walisema kuwa sababu ya kufunga maduka kwa muda usiofahamika ni kutoka jeshi la polisi kumwachia huru kiongozi wao kitaifa Bw Minja anayedaiwa kukamatwa toka juzi na jeshi la polisi na hajulikani alipo.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa mkoa wa Iringa Suzana Ndelwa alisema kuwa kufungwa kwa maduka katika mji wa Iringa kumewaathiri wananchi kiuchumi kutokana na baadhi yao kutoka nje ya mji wa Iringa kufuata huduma za jumla ila kufungwa kwa maduka hayo kumeyumbisha uchimi wao na wa Taifa kwa ujumla na kuwa ilipaswa kwa upande wa mkoa wa Iringa mkuu wa mkoa huo kuingilia kati suala hilo.
Mbali ya baadhi yao kutoma kufunga maduka yao bado ule usemi wa kufa kufaana ulionekana kutawala katika maeneo mengi ya mji wa Iringa kutokana na mgomo huo baada ya baadhi ya wafanyabiashara wadogo maarufu kama machinga kunufaika zaidi na mgomo huo kwa kupanga bidhaa zao nje ya maduka yanayofanya biashara kama zao na kupata wateja zaidi kupitia mgomo huo huku baadhi ya wafanyabiashara wakionekana kuuzia bidhaa zao stoo na wengine kufungua maduka yao nusu mlingoti na kuendelea kutoa huduma kama kawaida.
Wakati wafanyabiashara hao wakiwa katika mgomo huo mjini Iringa, Mafinga
na baadhi ya wachache wa Ilula bado jeshi la polisi lilionekana
kuweka ulinzi wa kutosha katika maeneo ya wafanyabiashara hao
huku askari wa kikosi cha kutuliza ghasia (FFU)) wakionekana
kuzunguka kila kona ya mji wa Iringa ili kuthibiti vurugu iwapo
zingejitokeza.
Jitihada za kumpata mkuu wa mkoa wa Iringa Bi Amina Masenza ama kamanda wa
polisi wa mkoa wa Iringa Ramadhan Mungi ili kuweza kuzungumzia
jinsi mkoa ulivyojipanga kumaliza tatizo hilo la mgomo ama jeshi la
polisi lilivyojipanga kuwalinda wafanyabiashara ambao waligoma
kuungana na wenzao katika mgomo huo hazikuzaa matunda baada ya simu
za viongozi hao wawili kuita bila kupokelewa .
Toa Maoni Yako:
0 comments: