Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete jana, Jumatatu, Novemba 10, 2014, alianza kuwasiliana na mamia kwa mamia ya wananchi mbali mbali nchini kujibu ujumbe mfupi wa maandishi (SMS) wa kumpa pole, kumtakia heri na nafuu ya haraka ambao amekuwa anatumiwa na wananchi tokea mwishoni mwa wiki.
Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akiwasiliana na baadhi ya wananchi waliokuwa wakimjulia hali kupitia simu yake ya mkononi kupitia ujumbe mfupi(sms) leo Jumatatu. Rais Kikwete anayepata matibabu katika hospitali ya Johns Hopkins jijini Baltimore Maryland nchini Marekani anaendelea vizuri na anafanya mazoezi mara kwa mara na afya yake inaendelea kuimarika (picha na Freddy Maro).
Tangu alipofanyiwa upasuaji wa tezi dume (prostrate) Jumamosi iliyopita kwenye Hospitali ya Johns Hopkins, Baltimore, Jimbo la Maryland, Marekani, Rais Kikwete amepokea mamia kwa mamia ya SMS zikimpa pole na kumtakia nafuu ya haraka.
Rais Kikwete bado anaendelea kujibu SMS hizo na wananchi ambao wamemtumia SMS Rais Kikwete waendelee kusubiri majibu ya Mhe. Rais kwa sababu anakusudia kujibu SMS zote ambazo ametumiwa.
Aidha, Rais Kikwete jana alizungumza kwa simu na uongozi wa juu wa Tanzania kwa mara ya kwanza tokea afanyiwe upasuaji. Rais alizungumza na Makamu wa Rais Mheshimiwa Dkt. Mohamed Gharib Bilal, Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein na Waziri Mkuu Mizengo Peter Pinda.
Wakati huo huo, madaktari wanaondelea kumtibu Rais Kikwete jana waliondoa bandeji kwenye sehemu ambako alifanyiwa upasuaji wakieleza kuwa hali yake inaendelea vizuri na anapata nafuu kwa kasi nzuri.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
11 Novemba, 2014
Toa Maoni Yako:
0 comments: