Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam. 

Mwanasheria Damas Ndumbaro ametoboa siri ya ugomvi wake na rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi kuwa ni basi la Taifa Stars na urais.

“Kuna mambo mengi yamejificha nyuma ya mgogoro huu, lakini nadhani chuki yangu na Malinzi imechangiwa na mambo kadhaa,” alisema Ndumbaro katika mazungumzo maalumu na gazeti hili.

“Sababu ya kwanza ni pale lilipokamatwa basi la TFF kwa deni ambalo nadhani linazidi Sh150 milioni. Malinzi alimpigia simu Silas Mwakibinga (aliyekuwa Mkurugenzi wa Bodi ya Ligi), akimwagiza kwamba bodi itoe pesa hizo kwa ajili ya kugomboa basi,” alisema Ndumbaro.

“Mimi niligoma kwa sababu ni mmoja kati ya watu waliokuwa wanatia saini katika utoaji wa fedha hizo. Fedha zilizokuwapo pale ni za Yanga. Unajua mpaka leo Yanga hawajafika kuchukua pesa zao ambazo zipo katika udhamini wa Azam TV na sisi bado tumewawekea.

Nikamuuliza Mwakibinga, hawa Yanga kuna mtu mmoja anaweka ngumu pale, lakini vipi kama akiondoka ghafla leo? Kesho asubuhi watakuja kuzichukua, tutazipata wapi? Nikagoma.

“Mwakibinga alimweleza Malinzi azungumze nami, lakini akagoma, akasema ‘mimi siwezi kuzungumza na Ndumbaro.’”

Ndumbaro aliongeza kuwa sababu ya pili ilikuwa ni pale alipokataa wakaguzi waliochaguliwa na Malinzi wasiikague Bodi wa Ligi.

“Nadhani wakati anaanza kututafuta sisi (Bodi ya Ligi) akiamini kuwa labda tuna fedha nyingi, akatuma wakaguzi wake waje kutukagua. Aliituma Kampuni ya Price Waterhouse Coopers. Wakaja jamaa fulani pale wawili ni Wahaya (kabila la Malinzi), nikajua madhumuni yao yalikuwa nini,” alisema Ndumbaro.

“Lakini, kwa mujibu wa katiba ya TFF, wakaguzi pekee wa TFF ndio wanaoruhusiwa kutukagua sisi, Bodi ya Ligi. Hapo Malinzi alikuwa anakaribia kuvunja katiba. Nikaona bora nimwokoe kwa kugomea wakaguzi wake.”

Baada ya sababu hizo mbili, Ndumbaro anaamini kuwa sababu ya tatu ambayo ni kubwa zaidi ambayo pia ni ya msingi ni jinsi ambavyo Malinzi amedanganywa na wapambe wake kuwa anautaka urais katika uchaguzi ujao.

“Wapambe wake (Malinzi) wamemdanganya kuwa Friend’s of Simba wanamwandaa Ndumbaro kuwa rais mpya wa TFF mara Malinzi atakapomaliza kipindi chake cha kwanza, kitu ambacho siyo kweli.

“Napenda nikutamkie, mimi sina ndoto hizo, sina mpango huo kabisa na Malinzi aelewe hivyo. Kifungo chake cha miaka saba kwangu kimelenga kuhakikisha kuwa anamaliza vipindi vyake vyote viwili kwa amani kabisa,” alisema Ndumbaro.”
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: