Napenda kuanza porojo zangu kwa kuweza wazi kuwa nina maslahi makubwa sana na jambo ambalo leo naenda kulipigia porojo.

Ndio nina maslahi maana mimi ni mkazi wa Bombambili Kivule jijini Dar es salaam na barabara ya Ukonga Mazizini - Moshi Bar – Kwa Mkolemba au Moshi Bar kwa Diwani – Bombambili ndizo barabara zangu nipitazo kila siku.

Tulilia wakazi wa Ukonga Mazizini kwa muda mrefu juu ya kusahaulika kwa barabara yetu na hatimaye Mungu alisikia kilio chetu tukapatiwa kalami kiduchu kuanzia Mombasa hadi Zahanati pale Transfoma.

Kilio kikabaki wa kipande kingine sasa kuanzia hapo Mazizini hadi Moshi bar – Kwa Mkolemba na Moshi Bar Bombambili kupitia kwa Diwani.

Barabara hii ilijaa mahandaki na si mashimo jambo ambalo lilisababisha watumiaji sisi wa barabara hiyo kutafuta njia za panya kupita katikakati ya makazi ya watu.

Mwaka huu baada ya kukatika kwa mvua ambazo ziliharibu vilivyo miundombinu ya barabara hizi nilizotaja hapa juu palianza kujengwa kwa kuchongwa na kisha baadhi ya maeneo kumwagwa kifusi.

Hilo lilitoa faraja sana kwa wakazi wa Ukonga na vitongoji vyake, mnamo mwezi Julai tarehe 22 kam sijakosea, Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, Jerry Silaa na viongozi mbali mbali akiwepo Diwani wa kata ya Ukonga, Elizabeth Mbano na Mhandisi wa Manispaa Bwana Muhinda Kassimu walitembelea barabara hiyo kuakagua ujenzi wake.

Picha zilipigwa wakati wa tukio hilo na Blog hii ilizichapisha maana hata ubovu wa awali ilichapicha sana picha za ubovu huo na mahandaki yaliyopo.

Meya Silaa ambaye ni mkazi na Diwani wa Gongo la Mboto eneo jirani na Ukonga alizungumza na wanchi wachache waliofika kumlaki.

Miongoni mwa vitu alivyo sema siku hiyo ni pamoja na gharama za ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 3 ambapo alisema itagarimu Milioni 90 na itajengwa kwa kiwangio cha Changarawe na pia fedha hizo ni za ndani ya Manispaa hakuna mkono wa wahisani.

Porojo zangu hii leo ni shaka niliyonayo juu ya ujenzi ule wa kiwango cha Changarawe! Na sijui ilikuwa ni kufukia tu maeneo korofi au kuchonga na kuweka kifusi kwa urefu huo wa kilometa 3?

Maana tunacho kiona watumiaji wa barabara ile ni vumbi tu na mashimo kurudi pale pale maana kiukweli hakuna kilicho fanyika na fedha zetu wananchi wa manispaa ya Ilala tunaweza kusema zimeliwa au tumepigwa vumbi la uso.

Meya Silaa nui ndugu yangu na jamaa yangu sana lakini nasema wazi kilichofanyika katika barabara hii ni aibu kwa uongozi wako makini na ni dhihaka kwa wakazi wa Ukonga na vitongoji vyake.

Barabara ya kwa Diwani ilikuwa sio mbaya awali kama ilivyo sasa lakini baada ya tinga tinga la mkandarasi Yule kupita liliharibu kabisa njia ile na mvua zikichanganyia ni kilio.

Milioni 90 kutumika kwa kuweka vifusi viwili vitatu bila kuweka hata makalavati mawili matatu katika maeneo ambayo yalikuwa na mkondo wa maji imeshindwa?

Lakini hebu Mhandisi wa Manispaa ona aibu na wewe, ulikuja kweli kukagua ujenzi ule au ndio kumwamini mkandarasi kupita kiasi.

Naamini bado ni mapema sana wahusika ambao mlikuja mazizini kukagua ujenzi ule mkandarasi alipoanza basi mfike na leo muangalie na mpite maeneo yote ya barabara mpate kujionea milioni 90 zilivyotumika.

Fedha hizo hata wangepewa wananchi wajitokeze na majembe na sepeto zao walahi isingejengwa kwa kiwago kile.

Huu ni utumiaji mbaya wa fedha za wananchi hivyo hauna budi kuangaliwa.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: