Rais Jakaya Kikwete  wa Tanzania (kulia) na Rais Pierre Nkurunzinza wa Burundi (kushoto) wakishikana mikono ikiwa ni ishara ya kudumisha umoja na mshikamano mara baada ya kuzindua  alama ya mpaka inayotenganisha nchi za Tanzania na Burundi.
---
Na Aron Msigwa – MAELEZO - Ngara, Kagera.

Marais wa Tanzania na Burundi wamewatoa hofu wakazi wa maeneo ya mpakani mwa Tanzania na Burundi kuwa zoezi Uimarishaji wa mpaka wa kimataifa kati ya nchi hizo linalofanywa na wataalam wa upimaji na ramani katika maeneo ya mipaka ya nchi hizo halilengi kuleta mgawanyiko miongoni mwao bali kuweka utaratibu mzuri wa utambuzi wa alama za mipaka ya kimataifa na kuwawezesha wananchi wa pande zote kuwa na uhakika wa uhalali wa maeneo wanayoishi.


Wakizungumza kwa nyakati tofauti na wananchi wa kijiji cha Mugikomero wilayani Ngara kwa upande wa Tanzania na Nteritare kwa upande wa Burundi wakati wa uzinduzi wa zoezi uimarishaji wa mpaka kati ya Tanzania na Burundi viongozi hao wamesema kuwa Serikali za nchi zote zimeamua kufanya zoezi hilo kufuatia mabadiliko mbalimbali yaliyojitokeza katika maeneo ya mipaka ikiwemo alama za kwanza zilizowekwa na wakoloni mwaka 1924 kuchakaa na nyingine kung’olewa na wananchi kutokana na sababu mbalimbali, ongezeko la watu, shughuli za kiuchumi na baadhi ya maeneo ya mito iliyokuwa ikitenganisha nchi hizo kukauka.

Rais wa Tanzania Mh. Dkt. Jakaya Kikwete akizungumza na wananchi wa vijiji hivyo amesema kuwa kufanyika kwa zoezi hilo kunatokana na agizo la Umoja wa Nchi za Afrika (AU) lilotolewa mwezi June 2007 katika kikao cha wakuu wa nchini za Afrika kilichofanyika Accra, Ghana ambacho kilizitaka nchi zote za Afrika kuhuisha upya mipaka ifikapo mwaka 2017 ili kuondoa migogoro ya mipaka inayojitokeza.

Amesema baadhi ya nchi za Afrika zimekuwa katika malumbano na machafuko ya mipaka kutokana na kutokuwa makini katika kuhakiki maeneo ya mipaka na kuongeza kuwa Serikali ya Tanzania itahakikisha kuwa zoezi hilo linaendeshwa kwa ufanisi mkubwa katika maeneo mengine yaliyobaki.

“ Sisi na Burundi ni ndugu wa damu tumechagua njia ya mazungumzo na kalamu, Marafiki huchora mipaka kwa mazungumzo na kalamu, maadui huchora mipaka kwa nguvu na kwa wino wa damu, mipaka ya kalamu hudumu na hustawisha jamii wakati ile ya damu huleta chuki, hujuma ,dhuluma na kisasi” Amesisitiza.

Amesema kuwa serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Burundi itahakikisha kuwa eneo lote la mpaka kati ya Tanzania na Burundi lenye urefu wa kilometa 450 katika mikoa ya Kagera na Kigoma linafikiwa licha ya kuwepo kwa changamoto mbalimbali na gharama kubwa za kufanikisha zoezi hilo.

“Maeneo mengi yako msituni, yako kwenye mabonde, mito na ni vigumu kuyafikia,tumeamua kuyagharamia na kufanya wenyewe kwa fedha zetu wenyewe kuonyesha dhamira na utashi wetu kulikamilisha zoezi hilo kabla ya muda uliowekwa ili kuondoa sintofahamu iliyokuwepo” Amesisitiza.

Amesema kuwa serikali itahakikisha kuwa inatenga fedha za kutosha kukamilisha zoezi la uwekaji wa alama za mipaka ili kuwezesha serikali za nchi mbili kuwa na mkataba mpya ambao utafuta mkataba uliowekwa na wakoloni.

Amewataka wakazi wa maeneo hayo kuwa walinzi wa alama za mipaka na kuepuka kuhujumu zoezi hilo, kulima katika maeneo ya hifadhi kutokana na umuhimu wa alama hizo kimataifa na kwa wakazi wa maeneo husika kwa kuwa zoezi hilo baada ya kukamilika litaondoa mashaka kuhusu uhalali wa maeneo wanayoyamiliki, huduma, shughuli za biashara na ujenzi wa makazi.

Kwa upande wake Rais wa Burundi Mh. Pierre Nakurunzinza ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuendelea kushirikiana na serikali ya Burundi katika kutekeleza majukumu na masuala mbalimbali yenye manufaa kwa wananchi.

Amesema ushirikiano katika zoezi hilo unaonyesha wazi kuwa Serikali za nchi zote mbili zinafanya kazi kwa ushirikiano mkubwa na kuongeza kuwa kuanza kwa zoezi hilo ni uthibitisho tosha kuwa waafrika wanaweza kufanya mambo yao wenyewe kwa ufanisi mkubwa.

Amefafanua kuwa Tanzania imefanya mambo mengi sana kwa serikali ya Burundi na hilo linathibitisha dhamira safi na ushirikiano mkubwa tokea wakati wa machafuko na vita iliyotokea nchini Burundi.

“Serikali ya Tanzania imekuwa bega kwa bega na serikali yetu ya burundi,Tanzania imefanya mambo mengi sana kwa wananchi wa Burundi, iliwahifadhi wananchi wa Burundi wakati wa machafuko,iliwalisha iliwatunza na kuwathamini na zoezi tunalolifanya sasa la kuhakiki mipaka ni dogo sana ikilinganishwa na undugu na umoja wetu” Amesisitiza.

Amewataka wakazi wa pande zote mbili kuhakikisha kuwa wanatoa ushirikiano kwa wataalamu wa upimaji na ramani wa nchi zote mbili na kuongeza kuwa wananchi wote watakaoathiriwa na zoezi hilo kutokana na kupoteza maeneo yao watalipwa fidia na kutafutiwa maeneo mengine.

Kwa upande wao mawaziri wa Ardhi,Nyumba na Makazi wa nchi hizo Prof. Anna Tibaijuka wa Tanzania na Jean Claude Nduwayo wa Burundi wameeleza kuwa zoezi la uhakiki wa mpaka wenye urefu wa kilometa 450 na alama 58 zilizoanzia Pwani ya Mashariki ya Ziwa Tanganyika hadi Kusini mashariki mwa mto Mwibu lina manufaa makubwa kwa wananchi wan chi zote mbili.

Wamesema Tanzania na Burundi zimefanya kazi kwa ushirikiano kupitia kamati ya Pamoja ya Ufundi ya Mipaka ya Kimataifa (JTC) amabayo ilitoa maamuzi muhimu ya ufanikishaji wa zoezi hilo ikiwemo uamuzi wa upana wa eneo la wazi la mpakani (buffer zone) kuwa mita 12.5 kila upande wa mpaka, Kuanza kwa kazi ya uimarishaji wa mpaka mwezi Machi mwaka huu pamoja na uratibu wa shughuli ya uzinduzi wa shughuli ya uimarishaji wa mipaka.

Wamefafanua kuwa uamuzi wa kuimarisha mpaka umetokana na kuwepo kwa ongezeko kubwa la shughuli za kiuchumi katika maeneo ya mpakani, hali ya mabonde na milima iliyopo ya mabonde na milima katika sehemu kubwa ya mipaka inayofanya utambuzi wa mpaka kuwa mgumu kwa wananchi wa kawaida.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: