Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Utamaduni, Bibi. Lilly Beleko kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo akimkabidhi Mzee Muhidini Gurumo barua kama ishara ya Serikali kutambua mchango wake uliotukuka katika tasnia ya Muziki nchini pamoja na kumpongeza kwa kustaafu kazi kazi hiyo, hivi karibuni nyumbani kwake Makuburi, Jijini Dar es Salaam. Wanaoshuhudia nyuma ya Mkurugenzi ni Rais wa Shirikisho la Muziki Tanzania, Bw. Addo Mwasongwe na kulia pembeni ya Mzee Gurumo ni Mkewe, Bibi. Pili Said Kitwana.

Na Concilia Niyibitanga- WHVUM

Serikali kupitia Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo imempongeza Mzee Muhidini Gurumo kwa mchango wake uliotukuka katika tasnia ya Muziki nchini pamoja na kumpongeza kwa kustaafu kazi hiyo.

Akiwasilisha barua ya Serikali ya kutambua mchango wa nguli huyo juzi nyumbani kwake Makuburi Jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Utamaduni kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Bibi. Lilly Beleko alisema kuwa Serikali inatambua na kuthamini mchango wake katika muziki wa Dansi hapa nchini.

‘Serikali inathamini mchango wako katika Muziki hapa nchini na itaendelea kuzienzi kazi hizo na inakupongeza kwa kazi nzuri ulioifanya ya kuelimisha, kuhamasisha na kuburudisha jamii’. Amesema Bibi. Beleko.

Naye Rais wa Shirikisho la Muziki nchini, Bw. Addo Mwasongwe, alisema kuwa Shirikisho linampongeza kwa kazi zake nzuri na litaendelea kumtumia katika kazi za muziki ikiwa ni pamoja na kutoa ushauri katika tasnia hiyo.

Nguli huyo wa muziki wa dansi nchini katika enzi zake za uimbaji ametunga nyimbo za kuelimisha jamii kufanya kazi kwa bidii, kudumisha usawa, amani na kuwakumbusha wazazi kutimiza wajibu wao wa kuwalea watoto katika maadili mema.

Mzee Gurumo ambaye alianza kazi ya muziki mnamo miaka ya 1960 na kustaafu kazi hiyo mwaka huu amesema kuwa anaishukuru Serikali kwa kutambua kazi yake na amefarijika kwa kukabidhiwa barua ya kumtambua na kumpongeza kwa kustaafu kazi hiyo.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: