Bharti Airtel imetangaza leo kwamba michuano ya kimataifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ya Airtel Rising Stars itaanza kutimua vumbi katika jiji la Lagos nchini Nigeria kuanzia September 16 hadi 22 ambapo Tanzania itawakilishwa na timu za wasichana na wavulana.
Michuano hii inafanyika kwa mara ya pili mfululizo kwa lengo la kutoa fursa kwa vijana chipukizi kutoka sehemu mbali mbali barani Afrika kuonyesha vipaji vyao na kuchochea maendeleo ya mpira wa miguu.
Akizungumzia mashindano hayo Mkurugenzi Mtendani wa Airtel Tanzania Sunil Colaso amesema: “Michuano ya Afrika ya Airtel Rising Stars itasaidia kuinua kiwango cha soka barani Afrika na Airtel inafarijika kupata fursa hii ya kuendeleza vipaji vya wachezaji chipukizi”.
Huu ni mwaka wa tatu tangu kuanzishwa kwa programu hii ya Airtel Rising Stars barani Afrika ambapo maelfu ya vijana wamepata nafasi ya kushiriki katika nchi 16 kuanzia ngazi ya chini, mkoa hadi Taifa.
Wachezaji nyota kutoka katika kila nchi hizo sasa wanaelekea nchini Nigeria kuchuana kwa lengo kuonyesha vipaji vyao zaidi na kupata mshindi ambaye ndiye atakuwa kinara wa Airtel Rising Stars barani Afrika mwaka huu. Mshindi pia atajinyakulia kitita cha dola za Mimarekani 10,000 ambazo ni zaidi ya milioni kumi na sita za Tanzania. Fedha hizi zitatumika kuwaendeleza vijana hao kielimu.
Michuano hii ya Afrika mwaka jana ilifanyika jijini Nairobi ambapo timu ya wasichana kutoka Ghana ilinyakua taji huku timu ya wavulana kutoka Niger ikiukwaa ubingwa kwa upande wa wavulana.
Mchuano unatarajiwa kuwa mkali zaidi mwaka huu huku timu mwenyeji Nigeria ikiwa imejianda vilivyo kuhakikisha kwamba wanawapa raha mashabiki wao na hatimaye kutwaa ubingwa wa mashindano hayo. Timu nyingine zinazotarajiwa kutoa upinzani mkali na hata kuiadhili Nigeria nyumbani kwao ni Ghana na Zambia.
Kwa kuendesha mashindano haya ya vijana Airtel inaelekea kutimiza lengo lake ililojiwekea awali la kuwa mdhamini mkubwa wa mchezo wa soka kwa vijana barani Africa.
Wachezaji bora kutoka katika mashindano hayo ya Afrika watapata fursa ya kushiriki kliniki mbili zitakazofanyika chini ya usimamizi wa klabu maarufu duniani: Arsenal na Manchester United. Kliniki hizo zitafanyika Lagos (Nigeria) na Lubumbashi (Democratic Republic of Congo) mwezi Aprili 2014 na kusimamiwa na makocha wa Manchester United na Arsenal.
Akizungumzia umuhimu ya kliniki za Airtel Rising Stars Colaso amesema: “Zitasaidiwa kuwaendeleza vijana kisoka na kuwapa hamasa ya kutaka kuwa wachezaji wa kulipwa”. Kliniki hizo ndizo zitakazozindua rasmi mwaka wa nne mwezi Aprili 2014.
Toa Maoni Yako:
0 comments: