Moja ya kanisa lililochomwa moto huko Visiwani Zanzibar kipindi cha mwishoni mwa mwaka 2012. (Picha na Maktaba).

Na Mohammed Mhina, wa Jeshi la Polisi

WAKATI Watanzania wakiendelea kutafakari tukio la kuuawa kwa kupigwa risasi kwa Padre Evaristus Mushi, wa Kanisa Katoriki Zanzibar, watu wasiojulikana wamelishambulia kwa mawe na baadaye kulichoma moto Kanisa la Walokole la Shaloom lililoko eneo la Kiyanga kwa Sheha mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Kusini Unguja Zanzibar, ACP Augostine Olomi, alisema jana kuwa tukio hilo limetokea majira ya saa 9.30 usiku.

Amesema moto huo ulizuka mara baada ya kikundi cha watu watatu kuonekana wakipita njia karibu na kanisa hilo na baada ya muda mlinzi wa kanisa hilo alisikia kanisa likishambuliwa kwa mawe juu ya makapaa.

Amesema baada ya mlinzi huyo kubaini kuwepo kwa hatari, alilazimika kukimbia kwenda kujificha lakini huku akiangalia kwa mbali kinachoendelea.

Kamanda Olomi amesema kuwa wakati mlinzi huyo akiwa amejibanza mafichoni huku akiangalia kinachotokea, mara aliona moto ukiwaka ndani ya kanisa na ndipo alipopiga simu kwa kiongozi wa kanisa hilo naye kuwajulisha Polisi.

Amesema Polisi walipofika hapo walisaidiana na wananchi kuuzima moto huo lakini wakati huo tayari ulishateketeza thamani za kanisa hilo na vitu vingine vilivyokuwa kanisani hapo.

Kamanda Olomi amesema moto huo ungeweza kusababisha athali kubwa kama usingedhibitiwa mapema.

Hata hivyo amesema uimara wa dali lililotengenezwa kwa Gibsam kumesaidia kuunusuru moto huo kuunguza mapaa na kuliteketeza kabisa kanisa hilo.

Amesema wakati uongozi wa kanisa hilo ukifanya tathimini ya harasa iliyopatikana kutokana na moto huo, Jeshi la Polisi limeanza kuwasaka washukiwa kwa kutafuta taarifa kwa raia wema na bado hakuna mtu ama watu waliokamatwa kuhusika na tukio hilo.

Hata hivyo Kamanda Olomi amesema Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vikundi vya Ulinzi Shirikishi na Polisi Jamii, wataanza utaratibu wa kuyalinda makanisa yote ili kuzuia matishio mengine kama hayo.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: