Na Mohamnmed Mhina, Handeni
 
Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani mkoani Tanga limeanzisha utaratibu wa kutoa elimu kwa madereva wa pikipiki maarufu kama Bodaboda mkoani humo ili kuwajengea uwelewa juu ya matumizi salama ya barabara.

Kamanda wa Polisi mkoani Tanga ACP Coastantino Masawe, amesema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kutaka kupunguza ajali za barabarani nyingi kati ya hizo zikiwa zinasababishwa na waendesha pikipiki.

Amesema mafunzo hayo yanaendeshwa na wakufunzi kutoka Kikosi cha Usalama barabarani mkoani humo wakiongozwa na Mkuu wa Kikosi hicho mkoani Tanga SP Abdi Isango na tayari wameshatoa elimu hiyo kwa vijana wa wilaya za Kilindi na Korogwe.

Amesema kuwa Jeshi la Polisi kama chombo chenye wajibu na mamlaka ya kusimamia sheria za nchi, limeona ni muhimu kutoa elimu ya sheria na taratibu za usalama barabarani ili wananchi wazielewe na waweze kujikinga na ajali zinazoweza kuepukika.

Akiwa wilayani Handeni kwa lengo hilohilo, Mkuu wa Kikosi cha Usalama barabarani mkoani Tanga SP Abdi Isango, amewataka waendesha pikipiki kufahamu kuwa pamoja na wao kujua kuendesha vyombo hivyo, lakini ni makosa kwa mtu yeyote kuendesha chombo cha moto bila ya kuwa na leseni ya udereva.

Kamanda Isango amesema leseni ambazo zinakuwa na madaraja tofauti, ni kibali kinachotolewa na Serikali ili kumpa mtu dereva uwezo wa kisheria wa kuendesha chombo cha moto.

Amesema sheria imepiga marufuku kwa waendasha pikipiki kupakia abiria zaidi ya mmoja na kwamba wote watakaopanda pikipiki ni lazima kila mmoja awe amevaa kofia ngumu kichwani ili imkinge itokeapo ajali aidha ya kugongwa na chombo kingine ama kuanguka kwa bahati mbaya.

Hata hivyo, Mkuu huyo wa Kikosi cha Usalama Barabarani mkoani humo, ametoa wiki moja kuanzia jana kwa wamiliki na madereva wote wa pikipiki kwa kila mmoja awe amenunua kofia mbili kwa ajili ya dereva na abiria atakayempakia.

Na amepiga marufuku vijana wenye umri chini ya miaka 18 kuendesha chombo cha moto kwani ni makosa kisheria na akikamatwa na akifikishwa mahakamani na akipatikana na hatia anaweza kupata adhabu.

Kwa upande wao vijana walioshiriki kwenye mafunzo hayo, wameelezea ugumu wa upatikanaji wa leseni za udereva na kwamba kila anayetaka kupatiwa leseni ni lazima asafiri umbali mrefu kutoka wilaya moja hadi mjini Tanga jambo ambalo wamesema linawawia vigumu kwao kutokana na kipato chao.

Hata hivyo wamesema wamenufaiaka sana na elimu walioipata na kusema ingawa wanajua kuendesha pikipiki lakini kumbe kuna mambo mengi ambayo walikuwa hawayajui kwa undani.

Vijana hao John Mchezo(28), Martin Luca(28), Shabani Mlenge(20) na Dickson Chacha(30) ambao wote ni wakazi na waendeshaji wa pikipiki mjini Handeni wamesema miongoni mwa mambo waliojifunza ni pamoja na kujua kuwa kumbe ni kosa kisheria kumpakia kwenye pikipiki mtoto mwenye umri chini ya miaka 8 bila ya kuwa na mtu mzima wa kumhsikilia.

Naye kijana Jafari Kandoro(28) alisema kua wamebaini kuwa miongoni mwa watu waliokuwa wakiwakamata vijana wa bodaboda hawakuwa askari Polisi bali ni matapeli.

Alisema kweli huo umedhihirika mwezi uliopita ambapo yeye akiwa na pikipiki alikamatwa na mtu mmoja aliyevaa kiraia akijifanya kuwa ni askari Polisi na kumtaka ampe shilingi 10,000 la sivyo angempeleka Polisi kwa uendeshaji mbaya wa pikipiki.

Hata hivyo kijana huyo alimtilia mashaka mtu huyo na kupiga simu Polisi na ndipo alipotimuwa mbio baada ya kuwaona askari lakini hata hivyo alisema Polisi walimfukuza hadi wakamtia mbaroni kwa kosa la kujifanya Askari Polisi. 

Amesema Polisi pia walimkamata kijana mwingine aitwaye Athumani Salum(20) mkazi wa Kivesa mjini Handeni, baada ya kukutwa akiwasumbua waendesha pikipiki akijifanya kuwa ni askari Polisi wakati hakuwa askari.

Naye Mkuu wa Polisi wa wilaya ya Handeni SSP Seth Mwakajinga,  amewataka vijana hao kushirikiana na Polisi kwa kutoa taarifa za wahalifu mbalimbali ili wakamatwe na kuifanya wilaya ya Handeni kuwa salama zaidi.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: