Makachero wa Jeshi la Polisi Zanzibar, wamegundua kuwepo kwa nyumba moja inayotumika kama ghala la kuhifadhia na kusambazia mihadarati kwenda kwa wafanyabiashara wadogo na wakubwa visiwani humo.

Afisa Uhusiano wa Jeshi la Polisi Zanzibar Inspekta Mohammed Mhina, amesema kuwa pamoja na kubainika kwa nyumba hiyo, Makachero hao pia wamewatia nguvuni watu wanne wakiwemo wawili wa familia moja kwa tuhuma za kuhusika na shehena ya mihadarati hiyo.

Akizungumzia tukio hilo, Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Zanzibar Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Muhudi Mshihiri, amesema kuwa nyumba hiyo iligundulika huko kwenye eneo la Kiembesamaki karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Zanzibar

Kamanda Mshihiri amesema kuwa, zaidi ya mafurushi 81 na kiroba cha mbegu za mihadarati vimekamtwa katika nyumba hiyo ambapo mafurushi sita kati ya hayo yalikamatwa kwa mmoja wa wamiliki wa ghala hilo Bakari Maganga Budole(33) wakati akienda kusambazia kwa wauzaji wadowadogo wa biashara hiyo.

Amewataja watuhumiwa wengine walikamatwa kuhusiana na mihadarati hiyo kuwa ni Hamisi Maganga Budole(35), Lusia Toufick Nassoro(28) na Shabani Ibrahim Mhegu(32) wote wakazi wa eneo la Kisimambaazi katika Shehia ya Kiembesamaki mjini Zanzibar.

Kamanda Mshihiri amesema kuwa bado Makachero wake wanaendelea na upelelezi ili kubaini wanakoipata mihadarati hiyo ili kuusambaratisha mtandao mzima.

Amesema kuwa baada ya Polisi wa Kikosi cha Wanamaji na Bandari Zanzibar kuwakamata watuhumiwa wa mihadarati mara kwa mara na kudhibiti uingiaji wake,  hivi sasa wafanyabiashara hao hutumia majahazi kwa kusafirishia na kushusha mizigo yao katika maeneo ya Bandari Bubu visiwani hapa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Polisi Kikosi cha Wanamaji na Bandari Zanzibar, SP Martin Lisu, amesema bado wanaendelea na utafiti ili kuzibaini bandari zote zisizo rasmi na kuweka mitego ili kuwanasa wale wote wanaojishughulisha na uingizaji wa mali za magendo ikiwemo mihadarati na madawa mengine ya kulevya kutoka viwandani.

Hivi karibuni Polisi wa Kikosi cha Wanamaji na Bandari Zanzibar, waliwakamata watu wawili kwa nyakati tofauti wakiingiza mihadarati visiwani humo kwa kutumia mito ya kulalia na huku mingine ikifungwa kama mahindi ya kuchoma na kuwekwa kwenye viroba.

Hata hivyo Jashi la Polisi limewaomba wananchi kuendelea kutoa taarifa katika vituo vya Polisi pale wanapobaini kuwepo na uhalifu wowote ukiwemo ujambazi wa kutumia silaha na madawa ya kulevya ili wahusika wakamatwe na kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma zao.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: