KUNDI la muziki wa kizazi kipya maarufu kama Bongo Fleva, Tip Top ‘Conection’ lenye maskani yake Manzese jijini Dar es Salaam, juzi walifanya kufuru ya aina yake katika Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma, katika tamasha la Fiesta 2011.

Kundi hilo linaloongozwa na Ahmad Ally ‘Madee’, lilikuwa miongoni mwa wasanii waliokuwapo katika ratiba ya wasanii waliotumbuiza kwenye tamasha hilo lililoratibiwa na Kampuni ya Clouds Media Group na ushirikiano na Prime Time Promotions huku mdhamini wake mkuu akiwa ni Kampuni ya Bia ya Serengeti.

Baada ya mshereheshaji B12, kutamka kuwa sasa ni zamu ya kundi la Tip Top Connection mashabiki walipagawa na kubwa zaidi mara wasanii hao walipopanda jukwaani walisababisha mkanyagano kwa mashabiki waliojitokeza kwa wingi katika tamasha hilo.

Mara baada ya zamu ya kundi hilo kufika, Madee ambaye ndio kiongozi wa kundi hilo, alipanda kwa bashasha kubwa na kuwafanya mashabiki washindwe kutulia sehemu moja na kuwapa kimuhemuhe kwa utamu wa nyimbo za kundi hilo, hasa ule wa ‘Bado Tunapanda’.

“Kila walipofika kwenye kiitikio Uwanja mzima zilisikika sauti za mashabiki wakiimba kwa pamoja na kundi hilo ‘Bado Tunapanda tunapanda milima najua tutafika tutafika mazima ” huku wote wakiwa wamenyoosha mikono yao juu.

Jukwaa lilioekana kama dogo vile, kwani msanii mwingine wa kundi hilo, Tunda Man na mwenzake Deso walikuwa wakilishambulia kupita kiasi, kitu kilichowafanya mashabiki wavunje uzio na kusogea mbele kabisa kwa wasanii hao huku kila mmoja akiwa na nia ya kuwapa mikono au kuruka kwa raha zao.

Kwa upande wa ulinzi nao ulikuwa makini kuhakikisha kwamba mashabiki hao hawavunji shughuli hiyo, hivyo kuufanya uwanja huo uwe kwenye joto na pilika pilika za wadau hao walionyesha shauku kubwa. Kama hiyo haitoshi kwa kiasi kikubwa, wasanii hao waliweza kufanya vitu adimu uwanjani hapo, huku wakiongozwa na Madee anayejiita Rais wa Manzese, miongoni mwa wasanii wakali katika muziki wa kizazi kipya. Wengine waliotoa burudani na kupagawisha ni pamoja na Godzilla, Joe Makini, Diamond na Barnaba.

Baada ya wasanii waliotoa burudani katika onyesho lililofana mkoani hapa ambao pia wamepata nafasi ya kuonyesha uwezo wao kwenye jukwaa la Serengeti Fiesta 2011 mkoani haapa ni wasanii wenyeji wa Mkoa wa Dodoma, Darasa, Country Boy, Stamina, Idd, Beka, Chriss wa Maria, Mika, Barnaba, Belle 9, Diamond, Godzilla, Nako2Nako na Joe Makini.

Aidha Belle 9 aliyepanda jukwaani na kuimba nyimbo zake tatu, huku ule wa Nilipe Nisepe ukipokelewa kwa shangwe kitu kilichowafanya mashabiki wagome kushuka jukwaani, wakishinikiza kijana huyo kurudia tena kuimba wimbo huo.

Kwa ujumla wasanii wote walitambua walichokuwa wakitakiwa kukifanya mbele ya mashabiki wao hivyo kila mmoja alijituma kadri alivyowezwa ili kuhakikisha jina lake linabaki katika vichwa vya mashabiki na wadau wa muziki kwa ujumla.

Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: