Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameongoza mamia ya waombolezaji kumsindikiza kwenye safari yake mwisho na kumzika Mama Tulakela Milia Samnyuha, mama mzazi wa Spika wa Bunge Mheshimiwa Anna Makinda.

Rais Kikwete akifuatana na Mama Salma Kikwete amewasili kwenye kijiji cha Yakobi wilayani Njombe, Mkoani Iringa, tayari kwa mazishi hayo kiasi cha saa sita mchana, akatia saini kitabu cha wageni na kutoa heshima zake za mwisho kwa marehemu aliyefariki alhamisi iliyopita akiwa na umri wa miaka 86.

Mara baada ya kumalizika kwa shughuli za kuaga, mwili wa Mama Samnyuha umepelekwa kwenye makaburi ya familia kwa ajili ya mazishi ambayo yalimalizika kiasi cha saa nane.

Miongoni mwa viongozi wengine ambao wamehudhuria mazishi hayo ni pamoja na Waziri Mkuu Mheshimiwa Mizengo Pinda, Katibu Mkuu wa CCM Mheshimiwa Wilson Mukama, wabunge wa chama tawala na vyama vyama vya upinzani akiwamo Kiongozi wa Upinzani Bungeni Mheshimiwa Freeman Mbowe.

Mama Tulakela Milia Samnyuha ambaye alizaliwa Mei 6, 1925, amefariki dunia siku moja tu kabla ya kufikisha umri wa miaka 86 kamili.

Mara baada ya mazishi hayo, Rais Kikwete ameondoka mkoani Iringa, baada ya ziara ya siku mbili mkoani humo, kwenda Dodoma ambako kesho anafungua Semina Elekezi kwa ajili ya viongozi waandamizi wa Serikali. Semina hiyo ya siku nne, inahudhuriwa na Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: