Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Exim, Jaffari Matundu (kati) akizungumza na wanahabari (hawapo pichani) kutangaza ununuzi wa Benki ya Canara Tanzania ambayo rasmi inakuwa sehemu ya benki ya Exim Tanzania. Ununuzi huu ni wa tatu kufanywa na benki ya Exim ndani ya miaka sita iliyopita ikiwa sehemu ya juhudi zake katika kuboresha sekta ya kibenki ndani na nje ya Tanzania. Kushoto ni Afisa Mkuu wa Kitengo cha Fedha, Shani Kinswaga na Mkuu wa Idara ya Uwekezaji Kimkakati, Sumit Shekhar wakiwa katika tukio hilo lililofanyika Makao Makuu ya Exim Bank jijini Dar es Salaam mnamo tarehe 29 Januari 2025.
Na Mwandishi Wetu.
Dar es Salaam, Tanzania – Benki ya Exim Tanzania inayo furaha kutangaza kukamilika kwa ununuzi wa Canara Bank Tanzania Limited. Huu ni ununuzi wa benki ya tatu ambao umefanyika na Benki ya Exim ndani ya miaka sita iliyopita, ikizidi kuimarisha nafasi yake kama mdau muhimu katika sekta ya benki nchini Tanzania.
Ununuzi huu ulianza kwa kusainiwa kwa makubaliano mnamo mwaka 2024 na kufuatiwa na kibali kutoka Benki Kuu ya Tanzania, na sasa umekamilika rasmi. Hatua hii ni ishara ya dhamira ya Benki ya Exim ya kukua, kuleta ubunifu, na kuboresha huduma zinazolenga mahitaji ya wateja.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Exim, Jaffari Matundu alisema, “Tuna furaha kubwa kuwakaribisha wateja wa Canara Bank Tanzania kwenye familia ya Benki ya Exim. Ununuzi huu ni ushahidi wa dhamira yetu ya kutoa suluhisho za kifedha zenye ubunifu na huduma za kipekee, tukihakikisha mabadiliko chanya kwa wadau wetu.”
“Ununuzi huu ni hatua ya kimkakati katika safari yetu ya kuboresha sekta ya kibenki ndani na nje Tanzania. Pamoja, tutaendelea kubuni, kukua, na kutoa suluhisho zenye huduma zinazokidhi mahitaji ya wateja wetu yanayobadilika huku tukichangia maendeleo endelevu ya Uchumi,” aliongeza Matundu.
Tangu kuanzishwa kwake mwaka 1997, Exim Bank imekuwa moja ya benki tano kubwa zaidi nchini, ikiendeleza upanuzi wa ndani na nje ya Tanzania kupitia ununuzi wa kimkakati. Safari hii ilianza kwa ununuzi wa benki moja nchini Uganda mwaka 2016, ikafuatiwa na ununuzi wa UBL Bank Tanzania mwaka 2019, FNB Bank Tanzania mwaka 2022, na sasa Canara Bank Tanzania mwaka 2024. Benki hiyo pia ina ofisi ya uwakilishi nchini Ethiopia, ikithibitisha matarajio yake ya kikanda.
Kuungana na ununuzi wa benki ni muhimu katika kuongeza ufanisi na kuimarisha sekta ya benki. Ununuzi wa kimkakati wa Benki ya Exim umesaidia kupunguza benki ndogo zisizo na tija, kuzalisha benki kubwa zaidi zenye ushindani, na kuongeza uwezo wa fedha, kupanua masoko mapya, kuboresha mseto wa bidhaa, kuongeza uimara wa sekta dhidi ya misukosuko ya mitaji, na kupunguza gharama za usimamizi na teknolojia. Hatua hii inaendana na maono ya Benki ya Exim ya kuwa taasisi kubwa ya kifedha kikanda ikiwa pia ni sehemu ya kuunga mkono mpango wa Benki Kuu ya Tanzania wa kupunguza benki ndogo ndogo kwa lengo la ufanisi zaidi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Uwekezaji Kimkakati, Sumit Shekhar alisisitiza, “Tumedhamiria sio tu kuwa sehemu ya maendeleo lakini pia kuchangia kikamilifu katika juhudi hizi. Iwe kusaidia wafanyabiashara wadogo wadogo, ujumuishwaji kifedha, ama kusogeza teknolojia katika jamii, tupo kwa ajili ya kuleta mabadiliko Chanya.”
Kujumuishwa kwa wateja wa Canara Bank Tanzania katika mfumo wa Benki ya Exim kunaleta manufaa makubwa, ikiwemo upatikanaji wa teknolojia za kisasa za kibenki kama huduma za mtandaoni na suluhisho za malipo, bidhaa mbalimbali za kifedha kama kadi za mkopo, kadi za malipo, na kadi za kabla ya malipo, mtandao mpana wa ATM, pamoja na ongezeko la matawi nchi nzima. Uwezo mkubwa wa kifedha, ikiwemo ukomo wa mikopo ya juu kwa mteja, pia ni fursa zaidi kwa wateja.
Sekta ya benki ya Tanzania, licha ya kuwa na uchumi mdogo ukilinganisha na Afrika Kusini na Nigeria, ina idadi kubwa ya benki. Hali hii imehitaji muunganiko wa lazima ili kuhakikisha uimara, ushirikishwaji, na mtiririko endelevu wa mikopo. Benki ya Exim inasaidia juhudi za serikali katika kukuza mfumo wa kifedha ambao ni wa ufanisi na jumuishi unaochochea ukuaji wa uchumi.
Naye Afisa Mkuu wa Kitengo cha Fedha kutoka Exim Bank, Shani Kinswaga alimalizia, “Ununuzi wa benki ya Canara Tanzania umepanua benki yetu, ikiwa ni pamoja na ongezeko la soko, rasilimali za kifedha, na faida.”
Shani alimalizia, “Kufikia mwishoni mwaka jana (2024), takwimu zimeonesha benki yetu imeendelea kuimarika zaidi ukijumuisha mali za jumla za TZS trilioni 3.1, kiasi cha mikopo TZS trilioni 1.8, na kiasi kilichowekwa cha TZS trilioni 2.5.”
Toa Maoni Yako:
0 comments: