Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi amempongeza Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa zaidi ya shilingi Bilioni 2 kwa ajili ya kuwezesha usimikaji wa Mfumo wa uendeshaji na usimamizi wa mashauri kwa njia ya mtandao.
Mhe. Katambi ametoa pongezi hizo leo Agosti 27, 2024 Jijini Dar es salaam wakati wa kufungua mafunzo ya Mfumo huo kwa wadau wa kwa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA).
Aidha, Mhe. Katambi amesema Serikali inatambua dhamana ambayo CMA imepewa katika kuhakikisha inachochea amani, utulivu na haki katika maeneo ya kazi ili kukuza Uchumi na ustawi wa wafanyakazi na waajiri.
Vile Vile, amesema Mfumo huo utasaidia kuhudumia wananchi kwa muda mfupi sambamba na kuondoa urasimu katika utoaji huduma.
Katika hatua nyingine, Mhe. Katambi amesema Serikali itaendelea kuongeza kasi ya kutatua migogoro, kusogeza huduma karibu na wafanyakazi, waajiri kupitia Tume inayotembea na kuendeleza usimikaji wa mifumo ya kielektroniki ili kurahisisha usajili na utatuzi wa migogoro ya kazi.
Sambamba na hayo, amesema Serikali inaendelea kusimika mifumo ya kielektroniki ya usajili, utatuzi na usimamizi wa migogoro ya Kazi.
Awali akizungumza Mkurugenzi wa CMA Mhe. Usekelege Mpulla amesema Mifumo huo utawawezesha wafanyakazi na waajiri popote walipo kusajili migogoro ya kazi ikiwemo kutumia simu-janja pasipo kulazimika kufuata ofisi za CMA.
Toa Maoni Yako:
0 comments: