Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Bivac Company Ltd Lishe yenye makao makuu yake Arusha, Beatrice Alban akionesha maharage Lishe yanayouzwa na kampuni hiyo.
Na Dotto Mwaibale, Singida
KAMPUNI ya Bivac Company Ltd Lishe yenye makao makuu yake Arusha imewaomba wakulima Mkoa wa Singida kuchangamkia fursa ya kuanzisha kilimo cha maharage lishe na kuwa itawasaidia kuwatafutia soko.
Ombi hilo limetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo , Beatrice Alban hivi karibuni mjini Singida wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kilimo cha maharage hayo ambayo ni muhimu kwa masuala ya lishe.
Alban alisema wamefika Mkoa wa Singida kupeleka fursa yenye faida zaidi ya tatu ya kwanza ikiwa inahusu masuala ya lishe ambayo imekuwa ni changamoto kubwa kuanzia ngazi ya familia hadi jamii ambapo Seikali imeiona na ya pili ni uchumi hasa kwa mkulima ambaye kila siku amekuwa hapigi hatua na badala yake amekuwa akirudi nyuma.
Mkurugenzi huyo alisema kuwa kwa kuiona changamoto hiyo kampuni hiyo inatamani kuona mkulima akipiga hatua kubwa katika masuala ya kilimo na sio kurudi nyuma.
Alban alizungumzia fursa nyingine kuwa ni ile inayohusu afya ya watoto ambayo inakwenda na usemi usemao ‘afya ya mtoto ni furaha ya mzazi’ kwani mtoto akiwa na afya bora mzazi atafanya kazi vizuri na kutunza kila kitu anachokipata na kujumuika na jamii katika shughuli mbalimbali.
Alisema katika nchi yetu kumekuwa na changamoto ya lishe hasa kwenye mikoa mingi hasa ile inayofanya vizuri kwenye masuala ya kilimo,
Alisema Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Siliani Arusha waligundua maharage yenye virutubisho vingi ambayo yanaweza kuufanya mwili kukua na kupokea matokeo kwa haraka na kuwa maharahe hayo yanaitwa maharage lishe.
Alisema maharage hayo ni ya kawaida na yanapikwa kama yanavyopikwa mengine lakini hayo yamerubishwa kwa kutumia teknolojia ya udongo na kuongezwa madini ya zinki na chuma ambayo ni muhimu na kuwa kama mwili wa binadamu utakosa madini hayo utakuwa ukinyemelewa na magonjwa mengi na mgonjwa akipelekwa hospitali kutokana na mwili wake kukosa madini hayo hata dawa atakayopewa haitaweza kufanya kazi.
“Mwili wetu unahitaji kuwa na madini ya zinki na chuma kwa wingi ili tuweze kuwa na afya bora,” alisema Alban.
Mkurugenzi huyo alitoa maelezo hayo ili kuonesha umuhimu wa maharage hayo ambapo alisema kampuni hiyo ipo tayari kutoa ushauri na maafisa ugani kwa ajili ya kilimo cha maharage hayo ikiwa ni pamoja na kuwatafutia soko.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Bivac Company Ltd Lishe yenye makao makuu yake Arusha, Beatrice Alban akionesha maharage Lishe yanayouzwa na kampuni hiyo.
Muonekano wa maharage lishe yakiwa sokoni
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Bivac Company Ltd Lishe yenye makao makuu yake Arusha, Beatrice Alban (kushoto) akiwa katika moja ya maonesho ya vyakula.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Bivac Company Ltd Lishe yenye makao makuu yake Arusha, Beatrice Alban akiwa Uwanja wa Ndege wa Songwe jijini Mbeya wakati wa safari za kuhamasisha kilimo cha maharage hayo.
Toa Maoni Yako:
0 comments: