Mmoja wa wazee wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tawi la Manguanjuki, Kata ya Mandewa mkoani Singida kwa niaba ya wenzake akiwasilisha malalamiko mbele ya Wajumbe wa Kamati ya Siasa ya chama hicho Kata ya Mandewa, (hawapo pichani) dhidi ya viongozi wao wa chama ambao pamoja na mambo mengine, wameshindwa kutekeleza majukumu yao ya uongozi kwa mujibu wa Katiba ya CCM, ikiwemo kushindwa kuitisha mikutano halali ya chama kwa mfululizo wa miaka minne tangu walipochaguliwa.
Wazee wakisikiliza kwa makini maamuzi ya chama baada ya kupokea malalamiko hayo.
Katibu wa CCM Kata ya Mandewa, Yusuph Makera Kijanga akizungumza na wazee hao kwenye mkutano huo.

Na Mwandishi Wetu Singida

WAZEE wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tawi la Manguanjuki Kata ya Mandewa Manispaa ya Singida wameiomba Kamati ya Siasa ya CCM ndani ya kata hiyo kuwaondoa mara moja viongozi wa chama hicho ndani ya tawi hilo-Mwenyekiti Abdalah Kitiku na Katibu wake Jasta Kiwigah ambao pamoja na mambo mengine, wameshindwa kutekeleza majukumu yao ya uongozi kwa mujibu wa Katiba ya CCM, ikiwemo kushindwa kuitisha mikutano halali ya chama kwa mfululizo wa miaka minne tangu walipochaguliwa.

Wakizungumza mbele ya wajumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM ya kata hiyo, wazee hao wameomba maamuzi ya haraka yachukuliwe ili kunusuru uhai wa chama kwenye maeneo hayo kutokana na viongozi hao kuonesha dhahiri ukiukwaji mkubwa wa kanuni na taratibu za chama, sanjari na kutokuwa na mahusiano mazuri baina yao na viongozi wa serikali ya kijiji na wananchi

Akizungumza baada ya kupokea malalamiko hayo, Mwenyekiti wa CCM Kata ya Mandewa Hamis Ireme kwa niaba ya kamati hiyo, alisema amepokea malalamiko ya wazee hao na kuahidi kuitisha mkutano wa wanachama ili kuangalia uwezekano wa kukaimisha nafasi hizo.

“Kamati ya siasa ya kata baada ya kupokea malalamiko ya wazee na kujiridhisha tumekubaliana kukutana na wanachama ili kujadiliana juu ya jambo hilo kwa kuangalia uwezekano wa kukaimisha nafasi za Mwenyekiti na Katibu, lengo ni kuleta ustawi na kuchagiza maslahi mapana ya chama na wanachama wetu ndani ya tawi la Manguanjuki,” alisema Ireme.

Kwa upande wake, Katibu wa CCM Kata ya Mandewa, Yusuph Makera Kijanga alisema kamati hiyo inatarajia kuitisha mkutano mkuu wa wanachama mapema mwezi Novemba mwaka huu, ambapo pamoja na mambo mengine, jambo hilo lililojitokeza litatolewa taarifa ili kupata baraka juu ya mabadiliko yoyote yanayoweza kufanyika.

Aidha, Kijanga aliwataka viongozi wengine wa matawi ndani ya kata hiyo kuwajali, kuwapenda, kuwasikiliza na kuwa karibu na wanachama na wananchi wote kwa kuonesha mshikamano ili kwa umoja na pamoja kuwezesha CCM kutekeleza Ilani yake kikamilifu.

“Hii Kata ya Mandewa ni kubwa sasa kama hatutashikamana pamoja tutachelewesha maendeleo. Na nisisitize hakuna aliye juu ya chama, yeyote mwenye dhamana ya chama ndani ya kata yetu atakayekwenda kinyume ajue ataharibikiwa yeye kabla hajakiharibu chama chetu,” alisema Kijanga.

Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: