Siku ya leo nilikuwa na rafiki yangu Samson Wambura sehemu tukibadilishana mawazo huku tukipata kinywaji na nyama choma, Kamanda Wambura alitoa mfano ambao mpaka sasa bado unazunguka kwenye akili yangu. Wambura alisema kuna Bwana mmoja ambaye yeye alikuwa na ujuzi wa Uhunzi (mjenzi) nyumba nyingi na majengo mengi ya eneo hilo alikuwa ameyabuni yeye na kusimamia ujenzi wake. Siku moja aliamka asubuhi na kumweleza boss wake kuwa hatamani tena kuajiriwa na kufanya chini ya mtu. Boss wake akafikiria kwa muda kisha akamwambia nikuombe jambo moja tu, ninaomba unifanyie kazi ya mwisho ya mimi na wewe kisha baada ya hapo kila mtu atakuwa na maisha yake.
Yule Bwana Mjenzi kwa shingo upande akalalamika sana kuwa atafanya hiyo kazi kwa sababu tu ya kumuheshimu.Yule Boss akafurahi akampa kazi mjenzi kuanzia mchoro.Yule Bwana mjenzi kutokana na kuona kama ameonewa akabuni mchoro sio mzuri sana, akaanza ujenzi wa nyumba ambayo kimsingi hakuifanya katika ubora wake unaostahili alikuwa hatumii muda wake kusimamia ujenzi, alikuwa akipewa fedha kwa ajili ya kujenga nyumba hiyo anatumia kwa matumizi mengine hali hiyo iliendelea mpaka ujenzi wa nyumba ulipokamilika.
Siku aliyomaliza alimwita Boss wake akamweleza kuwa kazi imekamilika, Boss wake akamweleza baada ya siku tatu atakuwa akiikabidhi nyumba hiyo kwa mwenye nayo alimsisitiza sana mjenzi awepo siku ya makabidhiano ya nyumba hiyo yeye pamoja na familia yake. Mjenzi alifurahi kuwa amealikwa na hiyo ilikuwa kazi yake ya mwisho kuifanya.
Siku ya siku ikafika watu wakakusanyika ilipofika saa ya makabidhiano mbele ya wafanyakazi wake waliokuwa wamekusanyika na baadhi ya marafiki waliokuwepo, Boss alimuita Yule mjenzi na familia yake akaanza kumshukuru mjenzi kwa moyo wake tangu alipoanza kufanya nae kazi. Boss alimshukuru sana Mjenzi kutokana na michoro na ujenzi aliousimamia amemfanya Boss kuwa miongoni mwa mamilionea katika nchi. Mjenzi alikuwa akitabasamu saa zote.
Boss akaendelea akasema anamshukuru Mjenzi hata alipomuomba kusimamia ujenzi wa mwisho kabisa alikubali kufanya kazi hiyo. Boss akaeleza kwa kweli hakuwa na namna nyingine ya kumshukuru Mjenzi zaidi ya Kumkabidhi hiyo nyumba. Boss alisema alimwomba mjenzi ajenge pasipokujua kuwa hiyo ni nyumba yake ya baadae akamshukuru mjenzi kwa kazi hiyo na akamkabidhi funguo kwa ajili ya kuishi kwenye nyumba hiyo.
Moyo wa mjenzi uligubikwa na huzuni akakumbuka namna ambavyo alitafuta mchoro mbayambaya na kusimamia vibaya na kuiba fedha, kiukweli nyumba haikuwa na kiwango stahiki kwa sababu tu Mjenzi hakujua kuwa ile nyumba atakuja kuishi mwenyewe baadae kama angalijua angaliisimamia mwenyewe vizuri zaidi ya hapo.
Tafakari...
Tulipokuwa tunakwenda shule hatukujua kama Elimu ilikuwa kwa ajili ya manufaa yetu wenyewe, wengine tulicheza na Elimu, wengine hatukujua Michezo tuliyocheza wakati tunakua ingekuja kutugharimu maisha yetu ya sasa, tunatamani tungejenga tena maisha yetu kwa sasa lakini sisi wenyewe tuliweka matofali ya ujenzi wa maamuzi kwenye kila kona ya maisha yetu.
Kila aina ya maamuzi unayoyafanya tambua kuwa unajenga nyumba utakayokuja kuishi mwenyewe na familia yako, wewe na ndugu zako. Wewe unao uwezo wa kujenga nyumba unayotaka kuishi baadae ukiamua kuwa “tupatupa” jua unajenga jumba bovu la baadae kwenye Uzee wako.
Nini Unajenga kupitia maamuzi yako ya sasa ndio yanajenga hatma yako ya Kesho.
Wanachofanya wabunge au viongozi kupitisha miswada mibovu, kutunga sheria kandamizi na kutunga katiba mbovu ni sawa na akili ya mjenzi kwenye simulizi hii, ikumbukwe kwamba sheria hizi zitawaathiri watanzania wote wakiwemo wao wenyewe na familia, ndugu, jamaa na marafiki zao kwani haya madaraka waliyonayo hawatakuwa nayo katika maisha yao yote watakayoishi hapa duniani.
Toa Maoni Yako:
0 comments: