Na Said Mwishehe, Globu ya jamii

MAISHA yangu ya uandishi wa habari kwa miaka 19 sasa, mimi Said Mwishehe hakuna siku hata moja nimewahi kuandika makala, maelezo, maoni au ushauri kuhusu Mtanzania ambaye anasumbuliwa na maradhi.

Nimekuwa na utamaduni wa kutoa pole au kushiriki kwenye maombi ya kuhakikisha mwenzetu anayeumwa, Mwenyezi Mungu ampe unafuu na apone haraka. Nimekuwa nikifanya hivyo kadiri ninapopata taarifa. Ila sijawaji kuandika maelezo mareeefu kumzungumzia mgonjwa!

Kwa mara ya kwanza leo naomba nivunje mwiko huo. Iwapo nitakuwa nakosea naomba nisamehewe. Nimeshindwa kuvumilia, nimeshindwa kukaa kimya. Nimeshindwa kuzungumza na moyo wangu na kisha kubaki nayo kichwani. Hapana nimeshindwa. Naomba ruhusa niandike kuhusu Ruge Mutahaba.

Ndio! Nataka kumzunguzia Ruge Mutahaba. Huyu huyu Bosi Ruge, ni huyu huyu Ruge ambaye wengi wamefanikiwa kupitia kwenye mikono yake. Ruge ambaye ukisikia atazungumza na Watanzania kupitia vyombo vya habari vya Clouds Media Group wote tunasubiri. Tunaka kufahamu anazungumza kuhusu nini. Ruge ambaye tunamuita Scofield wa Tanzania.

Mungu Muumba wa mbingu na ardhi, nipe ujasiri wa kuandika maelezo ambayo yatanyooka na kueleweka kwa haraka. Unapotaka kumzungumzia Ruge Mutahaba lazima kichwa kitulie, lazima uwe na hakika ya kile ambacho unataka kukisema.

Najua na Watanzania wanajua kwa sasa Bosi Ruge yupo kitandani. Ruge anaumwa. Pole kaka. Natoa pole kwako bosi Ruge. Nina hakika Mungu atakunyanyua na kusimama tena. Mungu atakuponya, Watanzania kila mmoja kwa imani yake wanakuombea Ruge upone haraka. Pole kaka, pole rafiki, pole swahiba wa Watanzania.

Taarifa za kuumwa kwako nimezipata kupitia taarifa mbalimbali ambazo zimekuwa zikitolewa kuhusu wewe. Sebastian Maganga alitoa taarifa rasmi kuhusu kuumwa kwako.

Na juzi hapa nimemsikia mdogo wako Mbaki Mutahaba, aliyetoa maelezo kuhusu hali yako. Nimemsikia akitoa taarifa ya gharama ya fedha ambayo inatumika kila siku kwa ajili ya matibababu yako.

Ruge narudia tena, sina shaka hata kidogo, afya yako itaimarika na kurejea kwenye majukumu yako ya kila siku. Nikiri sijawahi kukutana na wewe 'Live' tukazungumza au kujadili chochote. Huo ndio ukweli. Hata hivyo kukua kwa teknolojia ya habari na mawasiliano, nimekuwa nikikutana na wewe kupitia vyombo vya habari mbalimbali na hasa vile ambavyo unavisimamia vya Clouds Media Group.

Kaka kupitia wewe umenibadilisha kwenye mambo mengi. Umenifundisha maisha ni nini? Ili uishi unatakiwa kufanya nini? Unatakiwa kufanya mambo ya aina gani kufikia mafanikio. Ruge Mutahaba pole kaka. Katika maisha kuna watu ambao najua umekutana nao na kuzungumza nao.

Najua ni wengi lakini idadi yao haizidi wale ambao umewafikia kupitia vyombo vya habari. Sitaki kuzungumzia wasanii wa fani mbalimbali. Sisemi uliokutana nao kwenye jukwaa la fursa ambalo huambatana na tamasha la Fiesta.

Ruge wewe ni mwalimu wa kila kitu. Mwenyezi Mungu aliamua kuweka vitu ndani yako kwa ajili ya wengine. Leo unaumwa, mioyo yetu inaumizwa na kuumwa kwako. Pona kaka. Tunaumia kwa sababu kukosekana kwako katika kipindi hiki yapo baadhi ya mambo hayaendi sawa. Kuna kitu tunaona kinakosekana. Tunamuomba Mungu akupe afya njema na urejee nyumbani.Tunakuhitaji sana.

Amka Ruge wetu, amka Bosi Ruge, amka Scofield wa Tanzania. Najua umekaa kwa muda mrefu kitandani lakini huu ni wakati sahihi kwako kumka tena.Tunakusubiri kaka, tunakusubiri kaka mkubwa. Njoo tuendelee na maisha ya kuijenga Tanzania yetu.

Uwezo wako, maarifa yako, akili yako na ubunifu wako umechangia kwa kiasi kikubwa nchi yetu kupiga hatua kimaendeleo. Unaweza usione moja kwa moja lakini namna ambavyo umetengeneza fursa na Watanzania wakazitumia vema wengi wao wamebadilika. Wamepiga hatua kubwa za kimaendeleo.

Muangalie Nasibu Abdul a.k.a Diamond. Amepita kwenye mikono yako. Wapo wengi ambao wamenufaika kimaisha kupitia akili yako. Njoo kaka tunakusubiri nyumbani Tanzania. Kama binadamu najua huwezi kufanya kila kitu kikafurahisha watu wote lakini ukweli utabaki kuwa wengi wamenufaika kupitia wewe.

Naandika huku nikikumbuka ile kauli mbiu 'Tunakufungulia Dunia kuwa unachotoka'. Kaka Ruge binafsi nimekuwa ninachotaka. Nikwambie kaka Ruge kuumwa kwako, tunaumwa wengi. Huo ndio ukweli.

Mungu amekupa akili ya kujua ufanye nini na kwenye jambo gani. Umekuwa msaada mkubwa kwa Watanzania wengi. Hakuna kampeni ambayo ulianzisha ikakwama. Nimekumbuka wimbo wa Tuulinde na Amani ambao uliishirikisha wasanii mbalimbali.

Kaka Ruge tumekuzoea kukuona unaumiza kichwa kuhakikisha mambo yanakwenda. Rudi brother tuijenge nchi yetu. Sioni mahali ambapo Ruge ulitaka kufika ukakwama. Kila mahali ambako ulitamani kufika ulifanya hivyo.

Ruge ni wewe ambaye ukiamua jambo liwe linakuwa. Kikubwa zaidi ambacho najifunza kutoka kwako ni uwezo wako mkubwa wa kuchuja kipi uzungumze sasa na kipi uzungumze baadaye.

Tanzania imesimama, inakusuburi uamke kitandani. Inakusubiri urudi. Rudi kaka Ruge, Rudi Bosi Ruge. Njoo tuungane kwenye harakati za maisha yetu ya kila siku.

Kukuzungumzia wewe unaweza kutumia siku, wiki, mwezi na hata mwaka bila kumaliza. Umefanya mengi na natamani kuona ukiendelea kufanya mengi zaidi. Moyo wangu unaumia, machozi yanatoka. Ugonjwa wako unatuliza wengi. Amka ndugu yetu, amka Mzee wa vipaji lukuki.

Nikiri nimefarijika kuona kuna kampeni maalumu ya kuchangisha fedha kwa ajili ya kusaidia matibabu yako. Tumeambiwa kwa siku gharama ni kati ya Sh5 mpaka 6 milioni kila siku.

Ni wakati wetu Watanzania kuungana kuchangia matibabu yako. Ni matumaini yangu Watanzania tutaendelea kukuombea na kukuchangia kadiri ya uwezo wetu. Familia kwa nafasi yake imeendelea kutimiza majukumu ya kuhakikisha mwanafamilia wao anapata matibabu.

Rais Dk. John Magufuli alikuwa wa kwanza kutoa fedha kwa ajili ya matibabu ya Ruge.

Kaka Ruge siku zote umekuwa mstari wa mbele kuchangia wengine, hivyo nasi tunayo nafasi ya kukuchangia. Nia yetu ni kuona afya yako inakuwa imara. Ulitumia nafasi yako kuwashika mkono Watanzania waliopoteza matumaini, ni wakati wetu nasi kukushika mkono.

Uliwapa faraja waliokosa faraja, ni wakati wetu kukupa faraja.Tanzania All Stars uliwatumia mara kwa mara pale ulipoona iko haja ya kusaidia jamii iliyo kwenye mataabiko. Ni matumaini yangu Tanzania All Stars nao watakushika mkono.

Kaka Ruge wewe ni bonge la binadamu. Mungu amekupa utu na ubinadamu. Vyote unavyo. Nitakuombea kwa Mungu akuponye maradhi yanayokusibu. Nitakuombea kila sekunde, kila dakika na kila saa.

Nihitimishe kaka Ruge pole kwa kuumwa. Watanzania tunakuombea. Ukiupata ujumbe huu naomba utambue bado tunakupenda na tuko pamoja nawe.

Hata hivyo nikiri tu naumia sana ninaposikia baadhi ya watu wakiwamo wasanii ambao umewajenga kupitia vyombo vyako vya habari, wakitoa lugha za kejeli, dharau na kiburi dhidi yako. Inaumiza sana. Nawasikiliza wee kisha nasema Mungu wahurumie. Bosi Ruge pole. Pole kaka.

Simu: 0713833822
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: