Na Cathbert Kajuna - Kajunason/MMG.
Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), limesema hadi ifikapo 2020, linatarajia kuunganisha nyumba na viwanda 120,000 ili kupata gesi kupitia Mradi wa Kuunganisha gesi majumbani na viwandani.
Aidha, kwa kipindi hicho linalenga kukusanya mapato ya Sh trilioni moja ili kuchangia katika bajeti ya maendeleo ya taifa.
Akizungumza wakati wa kutembelea mradi huo katika kisima kilichopo Ubungo jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi wa TPDC, Kapuulya Musomba amesema mpaka sasa wateja wanaohitaji kuunganishiwa gesi wameongezeka kufikia 40 na kwamba mpaka mwaka ujao watakuwa wameunganisha wateja 1,000.
Alisema mtambo waliokuwa wanautegemea kuujenga ambao unatumika kuunganishwa na mtambo wa kupunguza mgandamizo wa gesi inayotoka bomba la Mtwara, umeshakamilika.
"Wateja wengine wameshaanza kutumia gesi na sasa tunampango kuunganisha Kiwanda cha CocaCola, maeneo ya Survey, Chuo Kikuu na Sinza kwa sababu tunaamini kupitia gesi itachangia uchumi wa viwanda," alisema Musomba.
Amefafanua kuwa mwishoni mwa Januari wateja wachache wataunganishwa na kuanza kutumia gesi hiyo ambapo wanatarajia kukusanya Sh bilioni 5,00 kwa kila mwaka.
Aidha, amesema wataunganisha kiwanda cha Dangote ili kiweze kupata gesi nyingi itakayotumika kuchomea udongo.
Musomba amesema pamoja na matarajio hayo makubwa, lakini wanakabiliana na changamoto ya ucheleweshaji wa utoaji wa mitambo bandarini ambayo husababisha kukwamisha mradi.
Amesema bado kunahitajika elimu ya kutosha kwa watu wanaopitiwa na mradi kwa sababu ni haki yao kupata huduma ya gesi lakini kutokana na miundombinu mibaya inasababisha watu wengine kupata huku wale waliotoa eneo wakacheleweshewa huduma hiyo.
"Asilimia 60 ya umeme unaotumika unatokana na gesi lakini changamoto iliyopo ni miundombinu ya jiji hili kwa sababu ya ujenzi holela hivyo tunashindwa kupeleka gesi kwa haraka na badala yake tunapeleka kwanza kwenye maeneo ambayo hayana changamoto kisha tutawapatia wengine gesi hii ni yetu sote," alisisitiza.
Mradi huo ambao umegharimu Sh bilioni nne utaanza kutumika kwenye Wilaya za Ilala, Kinondoni, Ubungo na Temeke kisha kwenda maeneo mengine.
Kwa upande wake, Meneja mradi huo, Silvanus Malimi amesema kuwa mtambo huo utapokea gesi kutoka Mtwara na kwamba bomba litaunganishwa na mtambo wa kupunguza mgandamizo wa gesi kutoka 60 hadi saba.
Amesema maeneo ya Ubungo Maziwa pia kuna mtambo wa kupunguza mgandamizo wa gesi ambayo inapelekwa moja kwa moja hadi maeneo ya Mikocheni na kuunganisha viwanda na wateja wa majumbani.
Amesema wateja waliopo sasa ambao wanasubiri kuunganishiwa gesi ni pamoja na Ubungo, Sinza, Mlalakuwa na Chuo Kikuu hivyo wanahakikisha wanakamilisha uunganishaji huo.
Toa Maoni Yako:
0 comments: