*Wizara yake yaanza kumchunguza aliyesambaza nyaraka na matamko mitandaoni

Na Said Mwishehe, Globu ya jamii.

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi Dkt. Mwigulu Nchemba ametangaza kumsimamisha kazi Msajili wa Taasisi za kidini Maryline Komba, huku akiwaomba viongozi wa dini kuendelea na shughuli zao za kutoa huduma za kiroho.

Pia amesema kwa sasa wizara yake inaendelea kuchunguza aliyeandika na kusambaza nyaraka katika mitandao ya kijamii ambayo imeibua sintofahamu kwa viongozi wa dini mbalimbali na Watanzania kwa ujumla ili sheria ichukue mkondo wake.

Ameongeza kuwa viongozi wa dini na watanzania kwa ujumla wafahamu kuwa nyaraka na matamko ambayo yamesambazwa kwenye mitandao ya kijamii hazina baraka za Wizara husika wala Serikali na hivyo ni vema zikapuuzwa tu.

"Tuwaombe viongozi wa dini kupuuza nyaraka ambazo zinasambazwa kwenye mitandao ya kijamii. Endeleeni na shughuli zenu kama kawaida kwani nchi hii inaendeshwa kwa mujibu wa Katiba na hivyo msiwe na hofu.

"Serikali na viongozi wa dini wamekuwa na ushirikiano mkubwa na hakuna mahali ambapo wanaonekana kutoaminiana. Hivyo aliyesambaza nyaraka hizo tunachunguza na kisha tutachukua hatua zinazostahili,"amesema Dk. Mwigulu.

Akizungumza leo wizarani hapo Dk. Mwigulu amesema msajili huyo amesimamishwa kupisha uchungu wa kina na iwapo atabainika kutohusika na matamko hayo au nyaraka ambazo zinasambaa mtandaoni basi atarudi kwenye majukumu yake.

Amesisitiza kuwa Serikali inaheshimu viongozi wa dini zote huku akionya wanaotaka kutumia dini kama kigezo cha kufanya siasa au kuigawa nchini.

"Wale ambao wanataka kutugawa kwa misingi ya kidini ni vema wakaacha kwani haitakuwa na tija kwao wala kwa Taifa letu. Hivyo tusiwe sehemu ya kushabikia mambo yanayohusu dini,"amesema.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: