KUELEKEA mkutano mkuu wa Yanga Juni 10 mwaka huu, uongozi umeweka wazi ajenda kuu zitakazojadiliwa huku ajenda ya uchaguzi ikiwa imewekwa kando kwanza.
Maandalizi ya Mkutano huo kwa wanachama wa klabu ya Yanga yameshika kasi sasa zikiwa zimesalia siku nne kuelekea Mkutano huo muhimu utakaotoa dira kwa klabu hiyo.
Akielezea masuala mbalimbali kuhusu maandalizi Katibu Mkuu wa Yanga Charles Mkwasa amesema wako katika hatua za mwisho kukamilisha maandalizi ya Mkutano huo utakaofanyika kwenye ukumbi wa Maafisa wa Polisi Oysterbay, jijini Dar es salaam.
Mkwasa amesema wanakusudia kuwaalika watu mbalimbali akiwemo aliyekuwa Mwenyekiti na mfadhili wa klabu hiyo, Yusuph Manji.
"Tunatarajia kuwaalika watu mbalimbali akiwemo Yusuph Manji ambayr alikua mwenyekiti na mfadhili wa klabu hii, Baraza la Michezo,TFF pamoja na wizara husika,"amesema Mkwasa.
Mwaliko utapelekwa pia kwa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Moja ya ajenda katika Mkutano huo maalumu kwa wanachama ni kujadili masuala mbalimbali ya klabu hiyo, ikiwa pamoja na suala zima la mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji.
Katika ajenda zingine zinazotarajiwa kuwasilishwa kwenye mkutano huo ni pamoja na kujadili ushiriki wa Yanga katika michuano ya kimataifa ikiwemo hatua waliyofika kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho, Mapato na Matumizi, bila ya kusahau Mabadiliko kuhusu mfumo wa uendeshaji.
Katika suala la uchaguzi wa kujaza nafasi zilizo wazi huenda litawasilishwa kupitia mengineyo ingawa kuna uwezekano mkubwa kwa ajenda hiyo kuondolewa ili kuwapa nafasi Wanachama kujadili masuala muhimu.
Kwa upande wa Kaimu Mwenyekiti wa Yanga Clement Sanga alisema mkutano huo utakuwa na lengo la kuwaeleza wanachama matatizo yanayoikabili timu yao, kuhusu uchaguzi wa kuziba nafasi zililizo wazi utatangazwa baadaye.
Toa Maoni Yako:
0 comments: