Wapagazi wa kampuni ya Easy Travel and Tours Ltd wanaobeba mizigo ya  watalii kwenye Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro (Kinapa) wakikusanya  mifuko na chupa za plastiki kwaajili ya kusafisha mazingira eneo la  Kwamrombo jijini Arusha.
Mkurugenzi wa Jiji la Arusha,Athumani Kihamia (kulia) akishiriki na wapagazi wa kampuni ya Easy Travel and Tours Ltd.
Wapagazi wa kampuni ya Easy Travel and Tours Ltd wakimwaga taka za mifuko na  chupa za plastiki baada ya kusafisha mazingira. Picha na  Filbert Rweyemamu. 

Na Filbert Rweyemamu, Arusha.

Wapagazi zaidi ya 100 wa kampuni ya utalii ya Easy Travel  & Tourism Ltd ya jijini hapa wamefanya usafi wa mazingira kwa  kukusanya mifuko na chupa za plastiki ikiwa ni sehemu za maadhimisho ya siku ya mazingira duniani yanayofanyika Juni 5 kila mwaka.

Mkurugenzi wa halmashauri ya Jiji la Arusha,Athumani Kihamia alisema eneo la  Kwamrombo Kata ya Muriet ambalo kampuni hiyo ilijitolea kufanya usafi  lina idadi kubwa ya watu na kuwa na mkusanyiko wa taka ngumu hasa mifuko na chupa za plastiki.

"Eneo hili lina idadi  kubwa ya watu na uzalishaji wa taka ni mkubwa ninaishukuru kampuni hii  kwa kushirikiana na halmashauri yetu kuona umuhimu wa kuweka mazingira yetu yakiwa safi,"alisema Kihamia

Mkurugenzi wa kampuni hiyo,Musaddiq Gullamhussein alisema tatizo la taka ngumu hasa   mifuko na chupa za plastiki limekua likiongezeka na wataalamu wa  mazingira wanadai ifikapo mwaka 2050 idadi ya chupa za plastiki baharini zitakua nyingi kuliko samaki.

Alisema  kuwashirikisha wafanyakazi wake ambao muda mwingi wanakua Mlima  Kilimanjaro kuwaongoza watalii ni sehemu ya kuwapa elimu ili wawe  mabalozi ya kutunza mazingira ya mlima huo ambao ni sehemu chanzo kikuu  cha mapato nchini.

Aliongeza kuwa baada ya kukusanya taka hizo watazipeleka kwenye moja ya viwanda kwaajili ya  kuzichakata na kupata bidhaa zitakazotumika kuvutia watalii kwenye  maeneo mbalimbali watakayotembelea.

Meneja  Msimamizi wa kampuni ya Easy Travel, James Makoye  alisema kuweka  mazingira safi ni njia ya sahihi ya kujiepusha na magonjwa  yanayoambukizwa na kulinda mazalia ya samaki kwaajili ya kupata lishe  bora na kuhakikisha usalama wa vizazi vijavyo.

Alisema wataendelea kukusanya chupa na mifuko ya plastiki ili kuwa na hatma  salama na kujenga mwamko wa jamii inayopenda kutunza mazingira  yanayowazunguka na vyanzo vya maji.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: