Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu Mhe.Jenista Mhagama akipanda miwa ikiwa ni ishara ya uzinduzi wa shamba darasa kwa wakulima wa nje (Outgrowers) wa Wilaya ya Kilosa . Mpango huo unaratibiwa na kiwanda cha sukari cha Mkulazi kinachomilikiwa na PPF, NSSF pamoja na Jeshi la Magereza na unalenga kuwajengea uwezo wakulima ili kuzalisha miwa yenye ubora na kuiuza kiwandani hapo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu Jenista Mhagama akisisitiza jambo baada ya kukagua shamba la miwa la kiwanda cha sukari cha Mkulazi-Mbigiro mkoani Morogoro mwishoni mwa wiki. Wanaomsikiliza kutoka kulia ni Mkurugenzi wa NSSF Profesa Godius Kahyarara na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dk.Steven Kebwe.Kushoto ni Mkurugenzi wa PPF Bw.Wiliam Erio. Kiwanda hicho kinachomilikiwa na PPF, NSSF pamoja na Jeshi la Magereza kinatarajiwa kutoa ajira 100,000 na pia kitazalisha tani 250,000 za sukari kwa mwaka.
---
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu Mhe.Jenista Mhagama amewataka vijana kuchangamkia fursa zilizopo nchini na kuacha kulalamika kuhusu ukosefu wa ajira.
Akizungumza baada ya uzinduzi wa mradi wa shamba darasa kuwezesha wakulima wa nje (outgrowers) wa kiwanda cha Sukari cha Mkulazi mwishoni mwa wiki katika eneo la Dumila wilayani Kilosa mkoani Morogoro,Waziri Mhagama amesema kundi la vijana linapaswa kuzifuata fursa zilipo na sio kusubiri kuletewa.
Waziri Mhagama amesema serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Pombe Magufuli imejidhatiti kupunguza tatizo la ajira kwa kutekeleza miradi mikubwa ya kitaifa lakini vijana ambao ndio nguvu kazi ya taifa wanapoteza muda mwingi katika mitandao ya kijamii.
“Takwimu zilizopo kwamba 56% ndio nguvu ya vijana,pia 60.7% ya ajira nchini zinapatika kwenye fursa zinazotokana na kilimo lakini vijana hawa hawataki kabisa kusikia habari za kilimo,” amesema Waziri Mhagama.
Waziri Mhagama amebainisha kuwa serikali inaboresha mazingira ya kilimo kwa kutenga ardhi na mikopo kwa vijana lakini vijana bado wameonekana kutochangamkia fursa hiyo.
“Kujitokeza kwa vijana katika mradi huu ni wito kwa vijana wengine nchini kuelewa kuwa utajiri unapatikana shambani,njooni tutawapa mashamba mlime miwa na Mkulazi watawasaidia kufikia malengo yenu”, amesema waziri huyo huku akiwapongeza kikundi cha vijana wa KCL ambao walikutana katika mtandao wa ‘WhatsApp’ na kuamua kutafuta mashamba kwa ajili ya kilimo cha miwa.
Mpango huo unaoratibiwa na kiwanda cha sukari cha Mkulazi ambacho kinamilikiwa na Mifuko ya hifadhi ya Jamii ya PPF na NSSF pamoja na Jeshi la Magereza unalenga kuwajengea uwezo wakulima wanaokizunguka kiwanda hicho (Outgrowers) kuzalisha miwa yenye ubora kukidhi mahitaji ya uzalishaj kiwandani hapo.
Nae Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni hodhi ya Mkulazi inayomiliki kiwanda hicho ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya jamii wa Taifa (NSSF) Profesa Godius Kahyarara amesema mpango huo utawezesha wakulima hao kupata mazao bora ambayo watayauza kiwandani hapo na kujiongezea kipato.
“Mkulazi inafungua ajira kwa watu wa ‘level’ zote kwa vijiji na miji inayozunguka kiwanda,tutafungua mashamba darasa mengi zaidi ili kuhakikisha wananchi watakaojihusisha na kilimo cha miwa wazalishe kwa weledi zaidi”,amebainisha Prof. Kahyarara.
Kwa mujibu wa Makamu Mwenyekiti wa Bodi hiyo,ambaye pia ni Mkurugenzi wa Mfuko wa PPF Bw.Wiliam Erio uwepo wa kiwanda hicho ni mkombozi wa upungufu wa sukari ambao huwa unajitokeza nchini.
“Licha ya Kiwanda cha Mkulazi kutoa ajira zaidi ya 100,000 kwa wananchi,lakini kitazalisha tani za sukari 250,000 kwa mwaka hivyo tunaomba vijana waje kuchukua fursa za mashamba nasi tutawasiadia ili waweze kuzalisha malighafi kwa ajili ya kiwanda chetu”,amefafanua Bw.Erio.
Toa Maoni Yako:
0 comments: