Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Richard Kayombo, akiwasilisha mada kuhusu Umuhimu wa Kodi kwenye Kikao Kazi cha Maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano Serikalini kinachoendelea jijini Arusha. Kikao hicho kinatarajia kumalizika tarehe 16 Machi, mwaka huu. (Picha na Benedict Liwenga).
Na Veronica Kazimoto, Arusha.
Maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano Serikalini wameombwa kuwa mabalozi wazuri katika sehemu zao za kazi na katika jamii wanayoishi kwa kuwaelimisha wananchi masuala mbalimbali yanayohusu kodi.
Akizungumza wakati akiwasilisha mada kuhusu Umuhimu wa Kodi kwenye Kikao Kazi cha Maafisa hao kinachoendelea jijini Arusha , Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Richard Kayombo, alisema elimu ya kodi itawafikia watu wengi zaidi kwa kuwa maafisa hao wana ushirikiano mkubwa katika kutoa habari sahihi kwa umma.
"Kila mmoja wetu anachokifanya ni sauti kwa mwenzake mahali alipo, ndio maana hata katika mitandao mbalimbali tumekuwa tukisaidiana kwa kuwa, ukiona jambo baya linasemwa juu ya taasisi ya mwenzako au Serikali unamsaidia kutoa ufafanuzi, hivyo, mkielewa mada yangu hapa, najua mtanisaidia kuelimisha masuala ya kodi katika sehemu zenu za kazi na maeneo mengine", alisema Kayombo.
Kayombo alisema kuwa, maafisa hao wana nafasi kubwa katika kuelimisha jamii na kusahihisha baadhi ya wananchi ambao wanakuwa na elimu isiyo sahihi kuhusu masuala yanayohusu kodi na ukusanyaji wa mapato kwa ujumla.
Aidha, pamoja na mambo mengine, Richard Kayombo aliwakumbusha Maafisa hao suala zima la kudai risiti kila wakati wanaponunua bidhaa ili kuchangia maendeleo ya nchi.
"Ni vizuri tu mkafahamu kuwa, tunasimamia kodi mbalimbali ikiwa ni pamoja na Kodi ya Mapato na Kodi ya Ongezeko la Thamani au kwa jina lingine Kodi ya Mlaji, ndio maana tunasisitiza kudai risiti kila mnapofanya manunuzi kwasababu usipopewa risiti na mfanyabiashara aliyesajiliwa kwa VAT na hata ambaye hajasajiliwa kwa VAT maana yake unakuwa umemnufaisha mfanyabiashara huyo na familia yake", alisisitiza Kayombo.
Bwana Kayombo aliwaambia Maafisa hao kuwa, wananchi wakidai risiti kila wanaponunua bidhaa mbalimbali, wanaepusha udanganyifu unaofanywa na wafanyabiashara wa kuficha mauzo halisi ambayo yanatumiwa na TRA kama sehemu mojawapo ya kuwakadiria kodi wafanyabiashara hao.
Kikao kazi cha Maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano Serikalini kinatarajia kumalizika tarehe 16 Machi, mwaka huu kikiwa na lengo la kuwajengea uwezo wa namna ya kutangaza shughuli za Serikali na kuhakikisha Idara na Vitengo vya Mawasiliano na Uhusiano Serikalini vinaimarishwa ili kuendana na kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano katika kuwahudumia wananchi.
Toa Maoni Yako:
0 comments: