Na Mwandishi Wetu.
Mwanahabari mwandamizi, Mayage Mayage, (56), amefariki dunia jana (Jumatatu) baada ya kuugua kwa muda.
Mayage amekutwa na umauti katika Hospitali ya Misheni ya Mbweni, Dar es Salaam, alikokuwa amelazwa kwa muda wa wiki mbili.
Taarifa kutoka kwa mdogo wake Emmanuel Mayage, alisema kuwa madaktari waligundua kaka yake kuugua saratani na kifua kikuu (TB).
Emmanuel alisema kuwa Mayage atazikwa Alhamis Desemba 28, 2017 katika makaburi ya Mbweni, eneo linaloitwa Maputo.
Taratibu za mazishi zinaendelea nyumbani kwa marehemu Mbweni Kijijini, eneo la Maputo ambako ndugu na jamaa wanakutana.
“Mayage aligundulika kuwa na saratani mwaka mmoja uliopita na alianza matibabu katika hospitali mbalimbali nchini ikiwemo Ocean Road na Muhimbili.
Alisema hali yake iliimarika kwa muda, lakini ikabadilika wiki tatu zilizopita na kusababisha kulazwa katika hospitali ya Mbweni.
Emmanuel alisema kuwa akiwa hospitalini hapo, kaka yake aligundulika pia kuwa na maradhi ya kifua kikuu na alianzishiwa tiba.
Mayage alianza kazi za uandishi wa habari mwaka 1995, akifanya kazi katika kampuni ya magazeti ya Habari Corporation; inayochapisha magazeti ya Mtanzania, RAI, Dimba, The African na Bingwa.
Baadaye Mayage aliondoka katika magazeti hayo na kuanza kazi ya uandishi wa habari wa kujitegemea, yeye akijiita “mwandishi huru.”
Akiwa mwandishi huru, Mayage alikuwa akiandikia magazeti mbalimbali nchini, yakiwemo ya Raia Tanzania, MwanaHalisi na mpaka kufariki kwake alikuwa mwajiriwa wa gazeti la TAZAMA.
Salva Rweyemamu, aliyekuwa mhariri mtendaji wa magazeti ya Habari Corporation amemzungumzia Mayage na kueleza kuwa alikuwa mwandishi mzuri, mahiri, asiyeogopa na aliyefanya kazi yake kwa weledi, huku akiwa mchambuzi mzuri wa habari za siasa za nchi hii.
“Mayage hakushindwa kazi yoyote aliyotumwa, ukimwagiza lazima uwe na uhakika wa kuifanikisha, hakika tumepoteza mchapakazi,” alisema Salva kwa masikitiko.
Toa Maoni Yako:
0 comments: