Picha ikionyesha Katibu wa TASWA mkoa wa Arusha Mussa Juma wa nne kutoka kulia akiwa pamaoja na wadhamini wa muda mrefu wa bonanza la wanahabari mkoani Arusha mara baada ya kumaliza mkutano na wanahabari ambapo wametangaza kuwa bonanza la mwaka huu litafanyika siku ya kumbukumbu ya kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius K. Nyerere.
Woinde Shizza, Arusha.
Wanahabari zaidi ya 400 wanatarajia kushiriki katika Tamasha la vyombo vya habari, Kanda ya kaskazini, litafanyika kuanzia Oktoba 14 siku ya kumbukumbu ya mwalimu Julius Nyerere hadi 15 mwaka huu.
Siku ya kumbukumbu ya mwalimu Nyerere kutakuwa na kongamano kujadili mchango wa hayati baba wa Taifa, katika masuala ya kiuchumi, kisiasa na michezo na baadaye Oktoba 15 kutakuwa na michezo katika uwanja wa General Tyre katika jiji la Arusha.
Tamasha hilo ambalo hufanyika kila mwaka linaandaliwa na Taasisi ya Arusha Media kwa kushirikiana na chama cha waandishi wa habari za michezo na burudani mkoa Arusha (TASWA).
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu wa TASWA mkoa Arusha, Mussa Juma, alisema tamasha hilo litashirikisha wanahabari 400 kutoka mikoa ya Arusha, Manyara, Kilimanjaro na Jijini Dar es Salam.
Juma alisema katika kongamano hilo mada mbali mbali zitatolewa na wabobezi katika masuala ya kiuchumi, kisiasa na michezo na wanahabari watapata fursa kutambua zaidi mchango wa hayati baba wa Taifa katika michezo.
"Mwaka huu, tumeamua kuanza na kongamano ili kukumbushana wanahabari masuala mbali mbali ambayo ni muhimu kwa mustakabali wa taifa letu" alisema.
Mratibu wa bonanza hilo Andrea Ngobole amesema katika tamasha hilo wanahabari na timu waalikwa watashiriki katika michezo ya soka, kuvuta kamba, mbio za magunia, riadha, kukimbiza kuku .
"Maandalizi yanakwenda vizuri lakini tunaomba wadhamini zaidi kujitokeza ili kufanikisha tamasha na Kongamano la wanahabari mwaka huu"alisema.
Alisema katika michezo timu ambazo tayari zimethibitisha kushiriki ni TASWA Dar es Salaam ambao ndio mabingwa watetezi, timu za Radio Sunrise, timu za vyuo vya Uandishi habari Arusha, Arusha one Radio, Triple A Radio, Radio 5, ORS Radio ya mkoa Manyara na TASWA Arusha.
"Tutangaza zawadi hivi karibuni na pia wageni waalikwa kama ambavyo hufanyika kila mwaka" alisema.
Toa Maoni Yako:
0 comments: