Na Mohammed Hammie
"Hujambo msikilizaji wa Pangani Fm na karibu katika kipindi cha Sauti Ya Mwanamke, kipindi hiki ni mahsusi kwa ajili ya kujadili changamoto mbali mbali anazokabiliana nazo mwanamke...." Ni sauti yake Maajabu Ally Madiwa anapokuwa redioni akitangaza kipindi.
Sauti yake iliyojaa bashasha ya kumfanya kila msikilazaji wa redio Pangani Fm iliyopo wilayani Pangani mkoani tanga atake kuisikia awapo redioni ndiyo iliyomfanya mpaka sasa awe miongoni mwa waandishi wa habari wadogo Tanzania wenye vipaji vya hali ya juu.
Uwezo wake wake kutangaza na kutambua aina gani ya habari inapaswa kutolewa kwa jamii anayoifanyia kazi uligunduliwa na shirika la Uzikwasa lenye kufanya
shughuli zake wilayani Pangani, ambalo linaelimisha jamii kwa kutimia sanaa.
Shirika hili limekuwa msaada mkubwa katika kuelimisha jamii ya Pangani kuachana na tabia hatarishi, kupinga ukatili dhidi ya watoto, wasichana na wanawake, na kuhakikisha viongozi
wanatekeleza majukumu yao kwa mguso.
Huko ndipo ambapo Maajabu Ally Madiwa aliponogesha uwezo wake mpaka kuwa miongoni mwa wateule 66 wa Tuzo za Umahiri wa Uandishi wa Habari Tanzania (EJAT) kwa mwaka 2016 kati ya washindani 810.
Maajabu Ally anakuwa mwandishi wa habari pekee kwa tuzo za Ejat za mwaka 2016 kutokea mkoani Tanga, kati ya waandishi 31 kutokea mkuo huo ambao waliwasilisha kazi zao kupitia tuzo hizo zenye heshima ya hali ya juu kwa sasa nchini Tanzania.
Endapo mwandishi huyu chipukizi kutokea mkoani Tanga atafanikiwa kutunukiwa tuzo na zawadi kwenye sherehe za kilele mnamno April 29 2017 basi atakuwa anachukua tuzo yake ya pili na itakuwa faraja si tu kwa Pangani Fm na Uzikwasa pekee bali kwa waandishi wa Tanga nzima.
Ikumbukwe mnamo mwaka 2015 Pangani Fm ilifanikiwa kutoa waandishi wawili kwenye tuzo za Ejat, Pili Mlindwa ambaye kwa sasa yupo Azam Media pamoja na Maajabu Ally Madiwa ambaye bado mpaka sasa anafanya kazi na Uzikwasa/Pangani Fm.
Maajabu Ally kuwa miongoni mwa wateule wa Tuzo za Umahiri wa Uandishi wa Habari Tanzania (EJAT) kwa mkoa wa Tanga wote, ni kielelezo cha ubora wa kazi nzuri na usimamizi uliotukuka kupitia shirika la Uzikwasa/Pangani Fm.
Kila la kheri Maajabu Ally Madiwa, nyota ya uwandishi wa habari inayong'aa kwa kasi nchini Tanzania kwa sasa, Pangani inakutegema, Tanga inakutegemea, leta tuzo nyumbani.
Toa Maoni Yako:
0 comments: