Dar es Salaam, Ijumaa Aprili 21, 2017; Jumapili 23 April 2017 saa tano asubuhi, Macho na masikio ya watanzania yataelekezwa jijini London, kumshuhudia mwanariadha wetu pekee anayeshiriki mashindano ya London Marathon akifanya vitu vyake. Haya ni moja ya mashindano maarufu zaidi ya riadha ulimwenguni na yanashirikisha wanariadha wa viwango vya kimataifa kutoka nchi mbalimbali kikiwemo Kenya na Ethiopia ambazo zina sifa kubwa katika ulingo wa riadha.

Mashindano hayo yataonekana Mubashara kupitia king’amuzi cha DStv katika chaneli namba 209 ya SuperSport (SS9) kuanzia saa tano asubuhi kwa saa za Afrika Mashariki.

Mkurugenzi Mtendaji wa Multichoice Tanzania Maharage Chande amesema kuwa kupitia king’amuzi maarufu cha DStv kitaonyesha mashindano hayo mubashara hivyo watanzania wataweza kushuhudia wenyewe na wala siyo kwa kuhadithiwa.

“Wakati wote DStv imekuwa kinara katika kuwahakikishia watanzania wengi uhundo wa aina yake hususan katika ulingo wa michezo na burudani na kwa mara nyingine tena tunauwezesha umma wa watanzania kushuhudia tukio hili muhimu ambapo balozi wetu Alphonce Simbu anatuwakilisha katika mashindano makubwa ya riadha” akisema Maharage.

Alphonce, ambaye ni Balozi maalum wa DStv, ni Mtanzania wa kwanza kushinda medali ya dhahabu katika mashindano maarufu ya Standard Chartered Mumbai Marathon na anatarajiwa kuwapa wakati mgumu manguli wa riadha ulimwenguni wanaoshiriki mbio hizi za London.

Multichoice Tanzania inamdhamini Simbu kwa muda wa mwaka mzima kwa lengo la kufanikisha maandalizi yake ya kushiriki katika mashindano ya Dunia yatakyofanyika jijini London mwezi wa nane mwaka huu. Udhamini huu ulianza tangu mwaka 2016 ambapo Multichoice humpatia Alphonce posho ya kujikimu pamoja na kusaidia kambi yake ya mazoezi.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: