Mwanariadha pekee wa Tanzania anayeshiriki mashindano ya London Marathon yanayofanyika jijini London jumapili hii amewasili Uingereza tayari kwa mashindano hayo ambayo yanayotarajiwa kushirikisha wanariadha mashuhuri duniani.
Alphonce, ambaye ni Mtanzania wa kwanza kushinda medali ya dhahabu katika mashindano maarufu ya Standard Chartered Mumbai Marathon, anatarajiwa kuwapa wakati mgumu manguli wa riadha ulimwenguni wanaoshiriki mbio hizi za London akiwemo Muethiopia Kenenisa Bekela pamoja wa wengine kutoka Ethiopia na Kenya.
Akiongea muda mfupi kabla ya kupanda Ndege kuelekea Uingereza, Simbu alisema amejiandaa kupambana kufa na kupona kuhakikisha kuwa ananyakua medali kwenye mashindano hayo. “Nitapambana kwa nguvu zangu zote. Ninakwenda London nikijua wazi kuwa naiwakilisha nchi yangu kwenye mashindano haya makubwa. Nakwenda kupeperusha bendera ya Tanzania” alisema simbu na kuongeza kuwa “Nina imani nitashinda kwani nimefanya mazoezi ya kutosha na nina ari na moyo wa kushinda. Naomba sala za watanzania wote ili niweze kuleta medali nyumbani” Alisema Simbu.
Ameishukuru sana kampuni ya Multichoice Tanzania kupitia King’amuzi cha DStv kwa kumdhamini na kuhakikisha anakaa kambini kwa muda wote huo bila shida yoyote. “Nawashukuru sana DStv kwa udhamini wao mkubwa wa kambi yangu ya mazoezi pamoja na mahitaji yangu mengine kwa kipindi kirefu sasa. Kwa kweli wao ndiyo waliofanikisha maandalizi yangu” Simbu amewashukuru pia wadau wote wa riadha hususan Chama Cha Riadha Tanzania pamoja na wizara inayohusika na michezo kwa jitihada zao za kuahakikisha safari yake ya kwenda London inafanikiwa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Multichoice Tanzania Maharage Chande amesema kuwa wana imani kubwa sana na Simbu kutokana na mazoezi aliyofanya. “Tunafurahi sana kuwa baada ya kuweka nguvu kubwa sasa Simbu anakwenda kushiriki mashindano haya akiwa amejiandaa vizuri. Tunaamini atashinda, na pia huu ni mwanzo wa ndoto yetu kubwa, ya kusikia kwa mara ya kwanza wimbo wetu wa Taifa ukipigwa kwenye mashindano ya Olympic. Kwa mwenendo wake, tunaamin Simbu atatufikisha huko” alisema Maharage.
Multichoice Tanzania inamdhamini Simbu kwa muda wa mwaka mzima kwa lengo la kufanikisha maandalizi yake ya kushiriki katika mashindano ya Dunia yatakyofanyika jijini London mwezi wa nane mwaka huu. Udhamini huu ulianza tangu mwaka 2016 ambapo Multichoice humpatia Alphonce posho ya kujikimu pamoja na kusaidia kambi yake ya mazoezi.
Alphonce anatarajiwa kuswasili nchini siku ya jumatatu Aprili 24 saa mbili asubuhi katika uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro.
Toa Maoni Yako:
0 comments: