Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama akijibu hoja za wabunge mbalimbali waliochangia wakati wa kujadili Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Ukimwi Bungeni Dodoma. 
---
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama amesema kuwa mapambano ya kukabiliana na tatizo la Dawa za Kulevya ni jukumu la kila mwananchi na wala sio suala la kuiachia Serikali peke yake.

Ameyasema hayo bungeni jana wakati akijibu hoja za wabunge waliochangia juu ya Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya UKIMWI na Dawa za Kulevya iliyoibua maswali kwa Serikali kuendelea kupambana na wanaoshiriki katika biashara haramu ya dawa za kulevya nchini.

Waziri Mhagama alieleza kuwa dhamira ya Serikali ni kuhakikisha jamii yote kwa ujumla inakuwa mstari wa mbele katika kutokomeza tatizo hili linalowaathiri vijana kwa kiasi kikubwa.

“Mapambano haya ni yetu sote, yasichague mtu na iwe agenda ya Kitaifa inayowahusu Watanzania wote na ikumbukwe kuwa tatizo la dawa za kulevya lina historia tangu mwaka 1990 na Serikali imekuwa ikipambana kwa jitihada nyingi hivyo niombe watanzania wote tuunge mkono vita hii ili kumaliza kabisa tatizo hili”. Alisema Waziri

Aliongezea kuwa, dhamira hii ya Serikali ilianza kuonekana tangu kuwepo kwa sheria namba 9 ya mwaka 1995 hadi ilipofanyiwa marekebisho mwaka 2014 na kubaini kuwa asilimia 56 ya nguvu kazi ya vijana ndiyo imeathiriwa na tatizo la dawa za kulevya.

Aidha pamoja na mapambano hayo, tayari sheria namba 5 ya mwaka 2015 na miundo ya mapambano inaelekeza namna ya kupambana na vita dhidi ya dawa za kulevya.

Kwa upande wake Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Harrison Mwakyembe alieleza Bunge kuwa ziwepo jitihada za makusudi za kuunga mkono mapambano haya yawe ya Watanzania wote kwa 
kutoa wito kwa jamii kutoa ushirikiano na kumpongeza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe.Paul Makonda kwa namna alivyojidhatiti kupambana na wote wanaoshiriki katika biashara hizi za dawa ya kulevya.

“Nieleza wazi kuwa jitihada za Serikali pekee hazitoshi ni lazima jamii iunge mkono kwa kuwafichua wanaojihusisha na mtandao huu wa Dawa za Kulevya na Mhe.Paul Makonda nampongeza kwa kuthubutu kuingia kikamilifu katika vita hii”.Alisema Mwakyembe

Alimalizia kwa kueleza kuwa, kinachohitajika ni dhamira ya dhati na si fedha, hivyo Serikali imedhamiria kukomesha kabisa tatizo hili nchini.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: