Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Kigoma Bw. Daniel Machura akitoa hotuba ya kufunga mafunzo ya miradi ya maendeleo kwa ajili ya ufadhili wa washirika wa maendeleo kwa Mkoa wa kigoma. Kulia ni mmoja wa wakufunzi wa mafunzo hayo, Dkt. Wilhelm Ngasamiaku kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kushoto ni Mratibu wa mafunzo hayo Bw. Paul Sangawe kutoka Tume ya Mipango.
Mratibu wa Mafunzo Bw. Paul Sangawe akitoa muhtasari wa kile kilichojadiliwa katika mafunzo hayo yaliyodumu kwa muda wa siku tano. Katikati ni Katibu Tawala Msaidizi Mkoa wa Kigoma Bw. Daniel Machura na kulia ni mmoja wa wakufunzi wa mafunzo hayo, Dkt Wilhelm Ngasamiaku kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Mchumi kutoka Wizara ya Fedha na Mipango - Tume ya Mipango, Bw. Senya Tuni akionesha kitabu cha Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2016/17-2020/21) kwa washiriki (hawapo pichani) wakati akiwasilisha mada juu ya Mpango huo.
Baadhi ya washiriki wakifanya mazoezi ya kanuni zinazotumika kuchagua miradi sahihi kwa ajili ya kupata ufadhili kutoka kwa washirika wa maendeleo. Mazoezi hayo yalifanyika mapema kabla ya kuhitimishwa kwa mafunzo hayo.
Mmoja wa washiriki akichangia mada kabla ya kuhitimishwa kwa mafunzo hayo.
Mmoja wa washiriki akichangia mada kabla ya kuhitimishwa kwa mafunzo hayo.
---
Na Adili Mhina, Kigoma.

Serikali imewaonya watumishi wasio waaminifu katika kusimamia na kuratibu miradi inayotekelezwa kwa fedha za washirika wa maendeleo kuepukana na vitendo vya rushwa na ubadhirifu kwani Serikali ya Awamu ya Tano haina huruma wala msamaha kwa watu wa aina hiyo.

Onyo hilo limetolewa mwishoni mwa juma na Katibu Tawala Msaidizi Mkoa wa Kigoma Bw. Daniel Machura wakati akifunga mafunzo ya maandalizi ya miradi ya maendeleo kwa ajili ya ufadhili wa washirika wa maendeleo kwa mkoa wa Kigoma yaliyofanyika mjini hapa na kuendeshwa na Wizara ya Fedha na Mipango kupitia Tume ya Mipango kwa ufadhili wa Serikali ya Ubelgiji.

Mafunzo hayo yalishirikisha Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa, Makatibu tawala wa wilaya, Wakuu wa Idara za Mipango, Wachumi, Maafisa Mipango na Watakwimu ambao wana majukumu ya usimamizi na uratibu wa miradi katika sekretarieti ya Mkoa wa Kigoma na Halmashauri zake zote.

Machura alieleza kuwa Serikali ya sasa haina nafasi ya kuwalea watendaji ambao wanaweka maslahi yao mbele badala ya kuangalia wananchi katika kutekeleza miradi inayofadhiliwa na washirika wa maendeleo kitu kinachopelekea miradi mingi kutekelezwa chini ya kiwango bila kuzingatia thamani ya fedha.

Alieleza kuwa baadhi ya watumishi walifikia hatua ya kuandaa maandiko ya kuomba fedha za ufadhili wa miradi ya maendeleo ya wananchi lakini fedha hizo zikipatikana walikuwa wanagawana na kuzitumia katika shughuli zao binafsi badala ya kuzingatia malengo ya fedha hizo.

“Tulifika pabaya sana, watu walikuwa wanaandika proposal (andiko) kwa wafadhili ili wapate fedha za kutekeleza miradi ya wananchi lakini cha ajabu unakuta fedha zikipatikana wanagawana bila aibu kwa kuwa zimetoka nje, katika serikali ya sasa watu wa aina hiyo hawana nafasi kwenye utumishi wa umma,” alieleza Bw. Machura.

Alisisitiza kuwa viongozi wa mamlaka za serikali za mitaa hawana budi kuzingatia mafunzo waliyopata kwa ajili ya kuongeza ufanisi wa kusimamia miradi na kuleta maendeleo katika maeneo yao ya utawala ili wafadhili waendelee kuamini kuwa fedha zote wanazotoa zinatekeleza miradi iliyokusudiwa.

“Tukifanya hivyo Serikali ya Ubelgiji pamoja na wadau wengine wa maendeleo watakuwa tayari kuongeza michango yao katika kuusaidia mkoa wetu kujikomboa kutoka katika umaskini hususan kwa kuendelea kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo”, alisistiza.

Kwa upande wake mratibu wa mafunzo hayo ambaye pia ni Naibu Katibu Mtendaji anayesimamia Klasta ya Biashara za Kimataifa na Mahusiano ya Uchumi Tume ya Mipango, Bw. Paul Sangawe alibainisha kuwa kuna baadhi ya watendaji ambao hawatoi taarifa za matumizi ya fedha za miradi ya ufadhili kwa wakati, kitu ambacho kinarudisha nyuma jitihada za washirika wa maendeleo katika kufadhili miradi.

Kutokana na hali hiyo, Sangawe alishauri uongozi wa Ofisi ya Mkoa wa Kigoma kujiwekea utaratibu wa kukaa na halmashauri zake mara kwa mara ili kuangalia maendeleo ya miradi inayotekelezwa kwa fedha za washirika wa maendeleo na kuhakikisha utekelezaji wake unakwenda sambamba na malengo husika.

Aidha, Sangawe alisisitiza kuwa ni lazima mamlaka zinazohusika katika kufanya makubaliano ya mikataba na wafadhili kuwa makini na kuzingatia kuwa miradi inayotaka kufadhiliwa ni ile yenye tija kwa wananchi na ambayo inaharakisha kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya 2025 ya kuipeleka Tanzania katika uchumi wa kati.

“Tusisite kukataa miradi ambayo haina tija kwa wananchi wetu, hata kama fedha ni zao lakini lazima ufadhili wao uendane na vipaumbele tulivyojiwekea kama Taifa. Tusipo zingatia hilo tutajikuta tunatekeleza miradi isiyo na faida kwa wananchi na kupelekea Serikali kupata hasara,” alisisitiza Sangawe.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: