Mkuu wa wilaya ya Hanang, Sara Msafiri akifafanua jambo
Na Woinde Shizza, Arusha
MKUU wa Wilaya ya Hanang, Sara Msafiri, ameutaka uongozi wa Kijiji cha Gidika kilichopo Kata ya Getanus, kuitisha mkutano mkuu utakaowapa wanakijiji fursa kutoa maoni juu ya viongozi wanaodaiwa kusababisha mgogoro wa ardhi.
Aidha alitaka aliyekuwa mwenyekiti wa kijiji hicho, Deo Luizer na viongoz wenzake, kufikishwa katika vyombo vya sheria kwa kukiuka maamuzi ya ugawaji wa ardhi.
Mgogoro huo umedumu kwa miaka mitano sasa.
Alitoa agizo hilo wakati akizungumza na wananchi wa kijiji hicho mwishoni mwa wiki.
Alisema viongozi hao waliendesha zoezi la ugawaji wa shamba la ekari 3365 ambalo serikali kuu ilirudisha kwa wananchi kutoka sehemu ya shamba lililokuwa chini ya Nafco.
Aliwataka viongozi hao kumpa mrejesho juu ya maamuzi ya mkutano ambao ameagiza uitishwe.
“Hatuwezi kuendelea na viongozi ambao wanashindwa kuwajibika, halafu wanakiuka maamuzi ya wananchi, hawa tunawaita wezi hawawezi kwenda na kasi ya mabadiliko ya serikali hii ya awamu ya tano lazima wafikishwe katika vyombo vya sheri.
“Shamba hili lilirudishwa kwenu na serikali kuu ili nyie wananchi muweze kunufaika nalo lakini hati bado ipo serikali kuu kwa hiyo mkiendelea kuleta vurugu juu ya shamba hilo serikali ina uwezo wa kuzuia hati yake,” alisema.
Alisema kama wanakijiji waliamua kuweka shamba hilo katika mipango ya matumizi bora ya ardhi lakini viongozi wao walishindwa.
“Viongozi hao ndiyo waliotufikisha huku leo. Nafahamu mlipopewa shamba hili mliweka matumizi bora ya ardhi mlitenga eneo la mifugo, mlitenga eneo la kilimo na mkatenga Land bank,” alisema.
Alisema kiini cha mgogoro huo wa ardhi kinatokana na viongozi wa serikali ya kijiji akiwemo Afisa Mtendaji wa Kata ya Getanusi, kukiuka makubaliano ya mkutano mkuu wa kijiji ambao uliridhia shamba hilo lenye hekari 3,366 kugawiwa kwa wananchi wa kijiji hicho cha Gidika.
Alisema mkutano huo uliridhia kila kaya ipewe hekari tatu jambo ambalo halikufanyika badala yake baadhi ya kaya zilipewa chini ya hekari hizo na kaya nyingine kukosa kabisa.
Pia alisema viongozi hao walikiuika makubaliano ya kutenga eneo la malisho la hekari 612, baada ya kujigawia jumla ya hekari 48 na kuuza jumla ya hekari 186 ikiwa ni sehemu ya eneo la malisho ambalo kijiji kiliazimia litengwe ikiwa ni mpango wa matumizi bora ya ardhi.
Alifafanua kuwa licha ya viongozi hao kujigawia na kuuza maeneo hayo kwa manufaa binafsi viongozi pia walishindwa kubainisha na kuwagawa jumla ya hekari 469.
Alisema hekari hizo kwa mujibu wa uchunguzi na upimaji uliofanyika katika eneo hilo badod wananchi hawajagawiwa wala kuwekwa katika mpango wowote wa matumizi bora ya ardhi ya kijiji.
Hata hivyo, Sara alisema kuna baadhi ya watu wanalima hekari hizo 469 lakini hawajachukuliwa hatua kutokana na kukingiwa kifua na baadhi ya viongozi.
Alitoa agizo la kuchukuliwa hatua viongozi hao ambao wamejunufaisha na ardhi ya kijiji kwa kujichukulia hekari 703 kati ya 3,366 hivyo kupelekea mgogoro uliodumu kwa miaka miatano sasa ndani ya kijiji.
Kwa upande wake kaimu afisa kilimo wa wilaya hiyo, Daniel Lyimo, akibainisha namna matumizi ya eneo hilo yanavyopaswa akisema serikali ilitoa sehemu ya shamba hilo kwa ajili ya wananchi wa Gidika.
Alisema kwa mujibu wa mihutasari ambayo wamepewa na kijiji hicho inaonyesha mkutano mkuu wa kijiji uliazimia itengwe eneo la malisho la ekari 612, na kila kaya katika kijiji wagawiwe kwa kupewa ekari tatu tatu.
Toa Maoni Yako:
0 comments: