Duna Lawrence (78) ni raia wa Togo ambaye alijitosa kwenda nchini Ujerumani kutafuta maisha mwanzoni mwa miaka ya 80. Baada ya kufika huko, alipata kazi, akawa muaminifu kwa Bosi wake ili aweze kupata mafanikio.
Baada ya miaka mingi kupita, Duna alirudi nchini mwake kwa mara ya kwanza na akaoa, kisha kurejea tena Ujerumani. Bwana Duna aliendelea kufanya kazi kwa bidii huku mafanikio yake kimaisha yakizidi kushuka chini, akaomba kuongezewa mshahara ili kukidhi mahitaji yake, lakini hiyo haikumpa unafuu.
Jamaa huyu bado hakuona mafanikio yoyote, kazi zikaendelea kuwa nyingi, familia yake nayo ikawa kwenye wakati mgumu. Bwana Duna umri ulizidi kumtupa mkono, huku akijiona hana chochote cha kujivunia katika kazi anayofanya.
Duna akawa mzee, nguvu nazo zikamuisha, ufanisi kazini ukapungua na magonjwa ya kiutu uzima yakaanza kumwandama, akamweleza Bosi wake hali halisi ya kiafya, akaomba alipwe stahiki zake ili arudi nyumbani. Bosi wake alimwonea huruma Mzee Duna, ila hakuwa na namna nyingine ya kumsaidia zaidi ya kumpa stahiki zake zote. Mzee Duna alirejea nchini Togo.
Mzee Duna akiwa anapekua begi lake wakati wa usiku, alikutana na barua ikiwa na dola 2000 na kuandikwa maneno haya:
"... Duna umefanya kazi kwa muda mrefu lakini ulishindwa kuniuliza jinsi ya kuwa tajiri kama mimi, hilo hukuliona kuwa na maana kwako, ukang'ang'ania kuongezwa mshahara na kudai malimbikizo yako, halikuwa jambo baya, ni haki yako. Ulikuwa kama mfungwa kwangu kwa sababu ya kufanya kazi ukitegemea kupata pesa, uliitumikia pesa kwa muda mrefu na haikuweza kukuondolea umasikini. Ninachokushauri, licha ya umri kuwa mkubwa ila anza kujali mambo yako, Mind Your Own Business, Not Another One's. Tumia pesa niliyokupatia kujali mambo yako, umejali mambo yangu kwa muda mrefu sana, jifunze kujali shughuli zako... "
Mzee Duna alisikitika sana, akatoa machozi kwa uchungu, hakujali suala la umri kumtupa mkono, akajitosa kutafuta fursa mbalimbali ndani ya nchi yake akiwa na mtizamo tofauti kuhusu pesa. Mzee Duna alifungua mgahawa, akaajiri vijana kadhaa kwa ajili ya kumsaidia kuwahudumia wateja. Biashara ikawa nzuri, akazidi kutanua biashara yake, akaongeza eneo ili kuwahudumia wateja wengi zaidi. Mzee Duna alipata maeneo kadhaa, akafungua migahawa mikubwa na kuipa jina la "MIND YOUR OWN BUSINESS RESTAURANT".
Nini tunajifunza?
Ifikie wakati kila mtu aanze kujali mambo yake katika kuamua hatima ya maisha yake kiuchumi. Kuendelea kuomba nyongeza ya mshahara, malipo ya ziada, na malupulupu mbalimbali hayatakufanya ujitegemee kiuchumi, bali kuwa tegemezi. Una miaka zaidi ya kumi kazini lakini bado huna uchumi imara, jaribu kujiuliza unamtajirisha nani, nani ananufaika kupitia jasho lako. Lazima ukumbuke kuwa maisha yako yote hayataishia kwenye kazi tu, kuna kipindi hutaweza kufanya kazi kabisa. Je, utaishi kwa njia gani? Anza kufikiria kuhusu maisha yako, timiza ndoto yako na si ya mtu mwingine. Anza kutengeneza mazingira rafiki kwa ajili ya kujiajiri, usiache kazi kwa papara, tafadhali fuata hatua makini ili uanze kujali mambo yako.
Neno Ni Uhai.
Toa Maoni Yako:
0 comments: