Kaimu Mganga Halmashauri ya Mji Njombe Dkt. Allen Kitalu akifungua mafunzo kwa wahudumu wa afya juu ya ulishaji wa watoto wachanga na wadogo.Kulia kwake ni Afisa Lishe Mji Njombe Bi. Mwakalukila.
Afisa Mafunzo lishe kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe Doris Katana akiwasilisha mada ya ulishaji watoto wachanga na wadogo.
Majaribio kwa Vitendo. Afisa lishe Mkoa wa Njombe Bertha Nyigu akionyesha njia mbalimbali za kumpakata mtoto wakati wa unyonyeshaji.
Wahudumu wa afya walioshiriki mafunzo kutoka katika Zahanati 18 za Njombe Mji.
Hyasinta Kissima, Njombe.
Akieleza madhumuni ya mafunzo hayo Afisa Mafunzo ya Lishe kutoka Taasisi ya chakula na Lishe Doris Katana amesema kuwa lengo la kutoa mafunzo hayo ni kuinua kiwango cha uelewa kuhusu ulishaji watoto wadogo na wachanga.
“Kama tunavyojua ulishaji wa watoto wachanga na wadogo ni muhimu sana na unasaidia sana kupunguza vifo vya watoto na kupunguza uwezekano wa kupata magonjwa ya kuharisha na magonjwa mengine ambayo yanaondoa sana uhai wa watoto wetu hapa Tanzania. Kwa kupata hii elimu ya unasihi wa ulishaji watoto wachanga na wadogo tunategemea kiwango chao cha elimu kitakua na wataweza kutoa elimu ipasavyo kwa ufasaha zaidi kwa wamama ambao wana watoto kuanzia pale mama anapojifungua mpaka pale mtoto anapokua na umri chini ya miaka mitano.”Alisema Doris.
Aidha Doris amesema kuwa mafunzo hayo yamelenga vituo vya huduma ya afya kwani katika vituo hivyo ndio sehemu pekee ambapo mama anahudhuria kwanza akiwa mjamzito hivyo kwa kipindi mama anapokua mjamzito akiweza kupewa taarifa sahihi ya ulishaji mtoto wake tunategemea pale anapojifungua ataweza kumuhudumia mtoto kwa ufanisi zaidi, Na hata pale anapojifungua kuna vitu ambavyo mama anatakiwa asaidiwe na apewe taarifa sahihi zitakazomwezesha kunyonyesha mtoto wake chini ya miezi sita na hata pale baada ya miezi sita anapomwanzishia chakula cha nyongeza aweze kumwanzishia kwa usahihi zaidi na kuweza kuhakikisha mwanae anakua na afya njema.
Akitoa takwimu za viwango vyunyonyeshaji Kitaifa Afisa Mafunzo huyo amesema kuwa kadiri miezi ya mtoto inavyozidi kuongezeka ndivyo hivyo asilimia na kasi ya unyonyeshaji inazidi kupungua jambo ambalo linakosesha virutubishi muhimu kwa mtoto kwa kukosa kupata maziwa ya mama kwa wakati muafaka.
Takwimu za Kitaifa zinaonyesha kuwa watoto wanaopata maziwa ya mama pekee chini ya miezi miwili ni 70.0%, 42% ikiwa hupata maziwa ya mama pekee kwa muda wa miezi 2-3 na 13% ya watoto hupata maziwa ya mama pekee kwa muda wa miezi 4-5. Ameendelea kusema kuwa takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 33 ya watoto wenye umri chini ya miezi 6 huanzishiwa vyakula vya nyongeza hali inayopelekea tatizo la udumavu kwa watoto.
Awali, Akifungua mafunzo hayo Kaimu Mganga Mkuu Halmashauri ya Mji Njombe Dkt Allen Kitalu amesema kuwa Mafunzo hayo ni muhimu kwa watoa huduma wa Halmashauri ya Mji Njombe kwani licha ya kuwa Mkoa wa Njombe umebarikiwa kuwa na vyakula vya kutosha na uchumi mzuri lakini bado Mkoa huo unaongoza kwa tatizo la Utapiamlo.
Kwa wakati huo huo Dkt Kitalu amewataka washiriki wa mafunzo kuwa watulivu na wasikivu wakati wote wa mafunzo ili elimu watakayoipata ikatumike vizuri na kwa wakati sahihi ili kuhakikisha kuwa wanawasaidia wale wanaohitaji msaada walengwa wote wanafikiwa na mabadiliko yanakuwepo.
Mafunzo hayo yatakayofanyika kwa muda wa siku tano yanahusisha wahudumu wa afya 20 kutoka katika zahanati 18 zilizopo katika Halmashauri ya Mji Njombe.
Toa Maoni Yako:
0 comments: