Mkuu wa Huduma za Fedha kwa njia ya simu wa Tigo Ruan Swanepoel (kushoto), akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam leo asubuhi kuhusu, Wateja Tigo Pesa kuvuna 6.04bn/- (dola 2,763,636) gawio la kumi la robo mwaka. Kulia ni Meneja Masoko na Usambazaji Huduma za Kifedha wa Tigo, Catherine Rutenge.
Meneja Masoko na Usambazaji Huduma za Kifedha wa Tigo, Catherine Rutenge (kulia), akizungumza katika mkutano huo.
Mkutano na wanahabari ukiendelea.

Na Dotto Mwaibale.

Kampuni inayoongoza kwa mtindo wa maisha ya kidijitali Tigo imetangaza gawio jingine la robo mwaka la shilingi bilioni 6.04 (sawa na dola za Marekani 2,763,636) kwa watumiaji wa Tigo Pesa ikiwa ni mara ya kumi katika mfululizo wa kampuni hiyo ya simu kugawa faida hiyo kwa watumiaji wake wa huduma ya fedha kwa njia ya simu.

Akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Mkuu wa Huduma za Fedha kwa njia ya simu wa Tigo Ruan Swanepoel alisema kwa ujumla kampuni hiyo imeshawalipa watumiaji wake wa huduma za fedha kwa njia ya simu jumla ya shilingi bilioni 52.28 (sawa na dola za Marekani 23,763,636) ikiwa ni malipo ya robo mwaka ya kumi tangu kuzinduliwa kwa huduma hiyo Julai 2014.

Hii ni mara ya tatu kwa mwaka huu kwa Tigo kulipa gawio kwa wateja wake.

Swanepoel alisema kuwa katika robo ya tatu ya mwaka huu kiwango cha faida kilipanda na kufikia asilimia 9 ikiwa kimepanda kwa asilimia 1 kutoka robo ya pili ambako kumechangiwa kwa kiwango kikubwa na kiwango kizuri cha riba katika mifuko ya dhamana ndani ya benki mbalimbali za biashara.

“Faida hii ya hisa inalipwa kwa wateja binafsi, mawakala wa reja reja na washirika wengine wa kibiashara wa Tigo ambao kila mmoja anapokea malipo yake kulingana na thamani ya fedha zilizowekwa kielektroniki ndani ya pochi zao za Tigo Pesa,” alifafanua Swanepoel.

Swanepoel aliongeza, “Tunayofuraha kubwa kutangaza ongezeko hili la faida katika gawio la mara ya kumi mfululizo. Hii inaonesha jinsi tulivyojikita katika kuwawezesha wateja wetu kufikia huduma za kifedha pamoja na nchi zima kwa ujumla kupitia huduma za Tigo Pesa.”

Aidha alidokeza kuwa ongezeko kubwa katika kiwango cha gawio kumechangiwa na kuongezeka kwa faida, kuboreshwa kwa mazingira ya soko na kukua kuliko imara kwa idadi ya watumiaji wa Tigo Pesa kama nyenzo kuu katika ongezeko kubwa la kiwango cha faida hususani katika kundi la wafanya biashara. Tigo Pesa hivi sasa ina mtandao mkubwa wa wafanya biashara zaidi ya 50,000.

Swanepoel alisema kuwa kama ilivyokuwa hapo awali gawio kwa wateja linakokotolewa kwa kuangalia wastani wa salio la kila siku la wateja la Tigo Pesa katika pochi zao za simu na kuongeza kuwa mpango huu wa kugawa faida umeainishwa katika kanuni za Benki Kuu iliyotolewa Februari 2014.

Mwaka 2014 Tigo Tanzania ilikuwa kampuni ya kwanza ya simu duniani kugawa faida iliyozalishwa na fedha za simu zilizopo katika Akaunti ya Udhamini kwa kipindi cha robo mwaka kwa wateja wake.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: