Mwenyekiti wa UWT wilaya ya Mufindi, Marcelina Mkini akiweka shada la maua katika kaburi la aliyekuwa mwenyekiti mstaafu wa CCM mkoa wa Iringa marehemu Tasili Mgoda wakati wa mazishi yaliyofanyika juzi mjini Mafinga
Makamu wa mwenyekiti wa CCM Tanzania bara ,Philip Mangula akiweka shada la maua katika kaburi la aliyekuwa mwenyekiti mstaafu wa CCM mkoa wa Iringa marehemu Tasili Mgoda wakati wa mazishi yaliyofanyika juzi mjini Mafinga.
Waziri wa ardhi nyumba na maendeleo ya makazi, Wiliam Lukuvi ambae ni mbunge wa jimbo la Isimani mkoani Iringa akiweka shada la maua katika kaburi la aliyekuwa mwenyekiti mstaafu wa CCM mkoa wa Iringa marehemu Tasili Mgoda wakati wa mazishi yaliyofanyika juzi mjini Mafinga.
Mbunge wa jimbo la Mufindi Kaskazini, Mahamudu Mgimwa (kushoto) na mbunge wa Kilolo Venance Mwamoto wakiweka shada la maua katika kaburi la aliyekuwa mwenyekiti mstaafu wa CCM mkoa wa Iringa marehemu Tasili Mgoda wakati wa mazishi yaliyofanyika juzi mjini Mafinga.
Mwakilishi wa vyama vya upinzani kutoka chama cha Demokrasia na Maendeleo (chadema) wilaya ya Mufindi akiweka shada la maua katika kaburi la aliyekuwa mwenyekiti mstaafu wa CCM mkoa wa Iringa marehemu Tasili Mgoda wakati wa mazishi yaliyofanyika juzi mjini Mafinga (Picha zote na matukiodaimaBlog).
---
Na MatukiodaimaBlog

MAKAMU mwenyekiti wa chama cha mapinduzi (CCM) Tanzania Bara Philip Mangula ameongoza mamia ya wakazi wa mkoa wa Iringa na mikoa ya jirani katika mazishi ya aliyekuwa mwasisi wa TANU na mwenyekiti mstaafu wa CCM mkoa wa Iringa Tasili Mgoda aliyefariki Oktoba 14 wakati wa kumbukumbu ya miaka 17 ya kifo cha baba wa Taifa mwalimu Julius Nyerere na kuzikwa jana katika makaburi ya Mafinga wilaya ya Mufindi kudai kuwa ameondoka kwa kuacha upendo kwa Taifa.

Mangula katika salamu zake alisema kuwa siku mbili kabla ya kifo chake Mgoda alimpigia simu japo kwa bahati mbaya hakuweza kuwasiliana kutokana na kuwa katika mkutano na kuwa kati ya watu na viongozi ambao walikuwa na upendo kwa wengine marehemu Mgoda ni mmoja na hivyo kuwataka wanafamilia ,wananchi wa Mufindi na wana CCM kudumisha upendo na kuendelea kufanya kazi kwa uadilifu zaidi kama njia ya kumuenzi marehemu huyo Mgoda na baba wa Taifa ambao katika uongozi wao waliweza kuongoza kwa kuzingatia misingi ya uadilifu.

Alisema kuwa Mgoda kuna mambo mengi ambayo hayaelezeki aliyoacha kama kielelezo cha uzalendo wake ndani ya wilaya ya Mufindi ambako alianzisha shule za shirika la elimu Mufindi (MET) lakini katika Taifa ni moja kati ya watu waliofanya kazi kwa karibu na mwalimu Nyerere ila katika ukombozi wa Taifa la Namibia kwa kumhifadhi mpigania uhuru wa Namibia Rais wa Kwanza wa nchi hiyo Sam Nujoma akiwa anafukuzwa na serikali ya wakoloni nchini mwake.

Alisema kuwa marehemu Mgoda alikuwa ni mtu mwenye upendo kwa wote na hakupenda makuu katika utawala wake hivyo ni vizuri kuendelea kumuenzi kwa kutenda mema na kupendana zaidi .

Mwenyekiti wa UWT Mufindi Marcelina Mkini alisema kuwa wao kama wanawake wanatambua mchango mkubwa ambao Mgoda aliutoa kwao ikiwa ni pamoja na kujenga misingi bora ya uongozi ndani ya chama na jumuiya hiyo na kuwa katika wilaya ya Mufindi ni mengi ambayo ameyafanya na kubwa zaidi ni kupigania uanzishwaji wa mji mdogo wa Mafinga na barabara ya lami kutoka Mafinga kwenda Madibila wilaya ya Mbarali .

Alisema kuwa yote hayo ameyafanya wakati akiwa mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Mufindi na kubwa zaidi ni uongozi wake uliotukuka kwa kuongoza chama kama mwenyekiti kwa miaka zaidi ya 40 katika maeneo mbali mbali .

Marehemu akiwa mwenyekiti wa CCM mkoa wa Iringa aliweza kupigania ujenzi wa barabara ya Lami kutoka Iringa - Dodoma na baada ya kukamilika kwa ujenzi huo alifurahi zaidi na kuwa sasa yupo tayari kufa wakati wowote kwani furaha yake imetimia .

" Enzi ya uhai wake alitupa moyo sana wanawake wa wilaya ya Mufindi na kujikuta tunasonga mbele kwa upendo zaidi hivyo sisi kwa ajili ya kumuenzi tutaanzisha mradi wa wanawake ambao utapewa jina la Tasili Mgoda kama sehemu ya kumuenzi zaidi"

Mkini ambae ni mjumbe wa NEC Taifa alisema kuwa kutokana kifo chake kuwa ni histori kubwa ndani ya Taifa kwa mhasisi huyo wa TANU ambaye alifanya kazi na baba wa Taifa kifo chake kutokea siku ambayo ilikuwa ni kumbukumbu ya kifo cha mwalimu ni vema wana CCM kuendelea kuenzi uzalendo na kuwakumbuka waasisi hao kwa kuepuka chuki ndani ya chama na badala yake kudumisha umoja zaidi.

Alisema pamoja na kuondoka kwa baba wa Taifa hivi sasa watanzania wamepata tumaini jipya la uongozi unaofafana na ule wa mwalimu Nyerere kwa kuwa na Rais Dkt John Magufuli ambae misingi yake ni sawa kabisa na ya waasisi hao wa TANU hivyo ni vema kuzidi kumwombea na kuendelea kuwaenzi waasisi waliotangulia kwa kufanya kazi zaidi.

Hivyo alisema kutokana na Rais wa awamu ya tano Dkt Magufuli kuahidi kutoa kiasi cha Tsh milioni 50 kwa kila kijiji ana amini wao kama UWT wilaya ya Mufindi watakuwa ni mwanga wa kuhamasisha uanzishwaji wa vikundi vya kiuchumi ambavyo vitanufaika na fedha hizo ili kuwakumbuka waasisi hao na kutekeleza kauli mbiu ya hapa kazi Tu kwa kufanya kazi bila kuchoka.

Kwa upande wao wabunge walioshiriki katika mazishi hayo Mahamudu Mgimwa wa Mufindi Kaskazini , Cosato Chumi wa Mafinga , Deo Sanga kutoka mkoa wa Njombe Kaskazini na mbunge wa Kilolo Venance Mwamoto walisema kuwa kuendelea kumuenzi Mdoga ni kufanya kazi kwa umoja na kuepuka kutengana kwa misingi ya kisiasa ama dini.

Huku waziri wa ardhi nyumba na maendeleo ya makazi Wilima Lukuvi ambae ni mbunge wa jimbo la Ismani akisema kuwa misingi ya uongozi wake marehemu Mgoda ndio ambao leo wananchi wa mikoa ya kusini wanafurahia matunda yake ikiwemo lami ya Iringa - Dodoma na mengine mengi ambayo ameyafanya kazi nafasi yake kama mwenyekiti wa CCM mkoa wa Iringa.

Viongozi wengine walijumuika katika mazishi hayo ni pamoja na naibu katibu mkuu wa CCM Bara
Luhwavi , mkuu wa wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu na wengine pia Aliyekuwa mwenyeviti wa wenyeviti wa CCM, Pancras Ndejembi.

Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Iringa alisema kuwa wazee wetu hao ambao wametangulia mbele za haki uongozi wao hauonyeshi kama walikuwa wakifuata mikate katika serikali ya Tanzania wala ndani ya CCM hivyo kuwataka wana CCM kupunguza njaa katika kutumikia nafasi hizo na badala yake kuungana kuijenga nchi na Chama bila kutanguliza njaa mbele.

Akisoma wasifu wa marehemu Tasili Mgoda , Msambatavangu alisema kuwa Mgoda alizaliwa July 6 1931 katika kijiji cha Mdandu wilaya ya Njombe ambapo kwa sasa wilaya ya wanging'ombe kwa wakati huo kijiji cha Mdandu ndicho kilikuwa makao makuu ya serikali ya Kikoloni wilaya ya Njombe.

Elimu

Alipata elimu ya Msingi shule ya msingi Kidugala kwa muda wa miaka miwili kati ya mwaka 1942- 1943 baada ya hapo aliendelea na elimu ya msingi Ilembula ambapo alisoma hadi darasa la sita mwaka 1947 alipohamia sekondari ya Malangali iliyopo wilaya ya Mufindi mwaka 1952 alihitimu kidato cha nne pamoja na masomo ya ufundi.

Mwaka 1973 Mgoda alikwenda nchini Marekani kupata mafunzo ya kilimo na ufugaji ,aliwahi kupata mafunzo ya siasa na uongozi chuo cha Kivukoni Dar es Salaam kwa sasa kinajulikana kama chuo cha kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere.

Utumishi

Mwaka 1953 alianza kazi kama msimamizi wa kampuni ya Carpentry Furniture iliyokuwa jijini Dar es salaam na mwaka 1956 aliamua kuachana na kazi hiyo kwa kuwa alikuwa amejiunga na siasa akiwa ni mmoja wa vijana wachache wa TANU waliokuwa na jukumu la kuhamasisha wananchi kukiunga mkono chama cha TANu katika kutafuta UHuru wa Taifa letu ,mwaka 1957-1958 Mgoda alikuwa mjumbe wa Halmashauri kuu ya mkoa na wilaya lakini pia akiwa ni mjumbe wa kamati ya siasa ya wilaya na mkoa.

Katika uhai wake amepata kushika nafasi mbali mbali zikiwemo za ukuu wa wilaya katika wilaya mbali mbali nchini katibu wa chama ,Mwenyekiti wa chama mkoa wa Iringa na udiwani pia uenyekiti wa Halmashauri ya Mufindi nafasi ambayo alidumu nayo hadi alipostaafu siasa.

Alisema kuwa marehemu Mgoda kwa kipindi kirefu alikuwa akisumbuliwa na matatizo ya shinikizo la damu na hivyo akawa anapata matibabu yake Hospitali ya mji wa Mafinga Hospitali ya mkoa wa Iringa na Hospitali ya jeshi Lugalo Dar es Salaam na kuwa Oktoba 14 hali yake ilibadilika ghafla na kukimbizwa Hospitali ya mji wa Mafinga majira ya saa 8 mchana na uchunguzi wa madaktari ulibaini kuwa anasumbuliwa na kisukari na shinikizo la damu ndipo alipoanzishiwa matibabu na majira ya saa 3;45 usiku Oktoba 14 aliaga dunia ,Marehemu Mdoga ameacha watoto 14 wajukuu 20.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: