Sehemu ya Chanzo cha maji cha Mto Mbukwa ambacho Kampuni ya TANWAT imepanda miti ndani ya mita sitini na kutishia uhai wa chanzo hicho. Kampuni hiyo imeamriwa kuondoa miti hiyo mara moja na kutakiwa kulipa faini ya Shilingi Milioni Hamsini.
Bustani darasa ya mbogamboga maarufu kwa jina la 'vinyungu' inayozingatia uhifadhi wa mazingira kwa kutolimwa pembezoni mwa chanzo cha maji.
Wakazi wa Kijiji cha Owadi Maheve ambao wanajishughulisha na kilimo cha mbogamboga kwa kufuata utaratibu wa kutolima kwenye vyanzo vya maji. Waziri Makamba amechangia mifuko hamsini ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa darasa litakalotumika kufundishia njia bora zaidi za kilimo.
Chanzo cha maji cha Mtitafu kilichopo Kata ya Igima, Halmashauri ya Wilaya ya Wanging'ombe kilichohifadhiwa vizuri na kuwa mfano mzuri wa kuigwa.
---
Na Lulu Mussa, Njombe.
Wadau wa Mazingira wametakiwa kufuata Sera, Kanuni na Tararibu katika kuendesha shughuli zao. Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. January Makamba ameyasema hayo leo Mkoani Njombe alipokuwa katika mwendelezo wa ziara ya kutembelea Mikoa mbalimbali hapa nchini kwa lengo la kujionea hali ya mazingira na kutoa maelekezo stahiki.
Waziri Makamba ametoza faini Kampuni ya TANMAT kwa kuikuka Sheria ya Mazingira inayokataza upandaji wa miti ndani mita sitini kutoka katika chanzo cha maji. "Kampuni hii imevunja sheria hivyo hamna budi kuchukuliwa hatua stahiki ili iwe mfano na kwa wengine" alisisitiza Waziri Makamba.
Kampuni hiyo imeagizwa kulipa faini hiyo ndani siku saba na endapo watakiuka hatua kali zaidi za kisheria zitachukuliwa dhidi yao. Waziri Makamba pia ameiagiza Kampuni hiyo kuondoa miti hiyo ambayo si rafiki kwa mazingira mapema iwezekanavyo na kuagiza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kuwapa 'Restoration Order" kurudisha mazingira katika hali yake ya kawaida.
Katika hatua nyingine, Meneja wa Kampuni hiyo inayojishughulisha na upandaji wa miti Bw. Joseph Shirima amekiri kupokea barua zizoelekeza kusitisha uharibifu huo wa Mazingira katika chanzo cha Mto Mbukwa ambacho kinasambaza maji kwa wakazi wengi wa Wilaya ya Wanging'ombe.
Aidha, Waziri Makamba ameupongeza Uongozi wa Mkoa wa Njombe kupitia Mkuu wa Mkoa huo Dkt. Rehema Nchimbi kwa kuwa mstari wa mbele kuhamasisha wanachi kuacha kulima bustani za mbogamboga pembezoni mwa mito.
Dkt. Nchimbi alimfahamisha kuwa kwa sasa kuna kikundi kijulikanacho kwa jina la "Jerusalemu" kinachotoa mafunzo kwa wananchi juu ya matumizi bora ya ardhi na kuhamasisha uhifadhi wa mazingira ambapo lengo ni kuanzisha vituo kama hivyo vya mafunzo kwa Halmashauri zote za Mkoa huo.
Waziri Makamba alitembelea na kuona "vinyungu" ambavyo awali vilikua vikilimwa kando ya mito na kwasasa vimehamishiwa majumbani, katika kuunga mkono jitihada hizo njema Waziri Makamba amechangia mifuko Hamsini ya Saruji kwa ajili ya ujenzi wa darasa litakalotumika kutoa mafunzo zaidi ya kilimo.
Waziri Makamba Waziri Makamba anaendelea na ziara yake ya kikazi ya kukagua hali ya mazingira nchini, hii leo amewasili katika Mkoa wa Mbeya.
Toa Maoni Yako:
0 comments: