Katibu Mkuu Ban Ki Moon alipomkaribisha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dk. Augutine Mahiga ambaye anamwakilisha Rais John Pombe Magufuli katika Mkutano wa 71 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Na Mwandishi Maalum, New York.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, ameitaka Tanzania kuendelea na kazi nzuri ya usuluhishi wa migogoro katika baadhi ya nchi za Maziwa Makuu.Ban Ki Moon ametoa wito huo jana ( jumatano) wakati alipokutana Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dk. Augustine Mahiga, ambaye anamwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika mkutano wa 71 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa unaoendelea hapa Jijini New York, Marekani.Katika mazungumzo hayo Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesema, Tanzania ni kutovu cha Amani, usalama na demokrasia, na kutokana na sifa hizo Tanzania, inapashwa kuendelea na juhudi zake za kuzisaidia nchi zenye migogoro.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon na ujumbe wake akiwa katika Mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeongoza Ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa 71 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Akazitaja nchi hizo kuwa ni Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Burundi na Sudani ya Kusini ambayo ameitaja kuwa ipo katika kipindi kigumu sana.
“Ninawashukuru sana viongozi wa Serikali ya Tanzania kwa kazi nzuri ya utafutaji wa Amani katika nchi zenye matatizo, Sudani ya Kusini ni nchi ambayo inatupa mashaka makubwa. Rais asaidie katika kurejesha hali ya utulivu.Tanzania ni nchi kubwa kwa hiyo bado ninaendelea kuitumainia.” akasisitiza Ban Ki Moon.Vile vile Katibu Mkuu Ban Ki Moon ametoa pia shukrani wa ushiriki wa Tanzania katika operesheni za ulinzi wa Amani na kazi na weledi mkubwa unaoonyeshwa na wanajeshi wa Tanzania.
Akatumia fursa hii kuishukuru Tanzania na viongozi wake kwa mchango wao mkubwa uliofanikisha yeye kuchaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Na akatoa pole zake kwa serikali na kwa watanzania baada ya kupata taarifa kuhusu tetemeko la ardhi lililosababisha vifo na uharibifu wa mali.
“Naishukuru sana Tanzania, namshukuru Rais Mstaafu Jakaya Kiwete na wewe ( Waziri) na viongozi wengine, mlichangia sana kwangu mimi kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Ninawashukuru sana sana. ” .Katibu Mkuu Ban Ki Moon anamaliza kipindi chake cha uongozi cha miaka kumi mwishoni wa Mwaka huu.Na tayari mchakato wa upigaji kura wakumtafuta mrithi wake unaendelea katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.Kwa upande wake, akiwasilisha salamau za Rais John Pombe Magufuli, Waziri Mahiga amesema. “ Ninawasilisha salamu za Mhe. Rais, alipenda sana kuhudhuria mkutano huu wa 71 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, kwa bahati mbaya ilimbidi kuahirisha safari yake kutokana na tetemeko la ardhi lililotokea hivi karibu nchini kwetu ”.
Ban Ki Moon akimkabidhi kitabu Waziri Mahiga, kitambua ambacho Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa anasema kimeandika na kuelezea utekelezaji wa majukumu yake na kwamba ni kitabu kizuri kutumika kama hadidu ya rejea.
Aidha Waziri Mahinga ametumia pia fursa hiyo kumshukuru na kumpongeza Katibu Mkuu kwa utekelezaji wa kutukuka wa majukumu yake katika kipindi cha miaka kumi ya uongozi wake.
“Kwa niaba ya serikali ya Tanzania nikupongeza kwa utekeleaji wa majukumu yake. Ulionyesha ushirikiano wa karibu na Tanzania, ushirikiano uliokuwezesha kumteua Dkt. Asha-Rose Migiro kuwa Naibu Katibu Mkuu na msaidizi wako wa karibu. Lakini pia uliniteua mimi kuwa Mjumbe wako Maalum huko Somalia . Tanzania inashukuru kwa haya na mengine” akasema Mahiga.
Aidha amemwelezea Katibu Mkuu kama kiongozi ambaye aliifanya Afrika kuwa kipaumbele chake, lakini pia aliibeba sana ajenda ya wanawake jambo ambalo amesema limemjenga sifa kubwa.
Akizungumzia kuhusu Tanzania kuendelea na juhudi za usuluhishi wa migogoro. Waziri amemhakikisha Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwamba, Tanzania na viongozi wake wataendelea na kujukumu hilo.
“Ni kuhakikishie kwamba Serikali yangu itendelea na jukumu hili la usuluhisi. Na kwa upande wa Burundi Tanzania, inaushukuru Umoja wa Mataifa, kwa kutambua na kuamini kwamba Jumuiya ya Afrika Mashariki inaweza kuushughulikia mgogoro huu. Tanzania ambayo imekabidhiwa jukumu la uwezeshaji wa mazungumzo ya Amani inataka kufanya kazi kwa karibu na Umoja wa Mataifa hivyo misaada ya hali na mali kutoka Idara za Umoja wa Matifa ni jambo muhimu”.Amesisitiza Waziri Mahiga.
Toa Maoni Yako:
0 comments: