Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akifuatilia mambo mbalimbali yaliyokuwa yakijadiliwa wakati wa ufunguzi wa mkutano wa 27 kwa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi wanachama wa Umoja wa Afrika AU ulioanza jana katika ukumbi wa KCC mjini Kigali Rwanda. Makamu wa Rais amemuwakilisha Rais John Magufuli kwenye mkutano huo. Picha na OMR.
KIGALI, RWANDA.
Tanzania imeuhakikishia Umoja wa Afrika (AU) kwamba itaendelea kufanya kazi kwa karibu na nchi wanachama wa AU katika kujadili changamoto za kiusalama zinazolikabili Bara la Afrika kwa njia ya mazungumzo na upatanishi kama inavyoelekeza Katiba ya umoja huo.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ametoa kauli hiyo wakati akichangia mada kuhusu Hali ya amani na usalama katika Bara la Afrika katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU) uliofanyika hapa Kigali, Rwanda.Mheshimiwa Samia alisema Tanzania inasikitishwa na inalaani vikali matukio ya uvunjifu wa amani yanayoendelea kujitokeza katika baadhi ya nchi za Kiafrika kiasi cha kutishia usalama wa raia.
Alielezea mauaji ya Hafsa Mossi, aliyekuwa Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki na waziri wa zamani wa Burundi na mapigano ya hivi karibuni Sudan ya Kusini ambapo mamia ya raia wasiokuwa na hatia waliuwawa na wengine maelfu wameachwa bila makazi kwamba ni muendelezo wa uvunjifu wa amani katika nchi hizo.
Aliwataka wadau husika katika nchi za Burundi na Sudan ya Kusini kushiriki kikamilifu katika mazungumzo yanayoendelea kwa kuwa hiyo ndiyo njia muafaka ya kuleta amani, usalama na utulivu wa kudumu katika nchi zao.Aidha, Makamu wa Rais ambaye alimwakilisha Rais John Magufuli katika mkutano huo aliiomba Jumuiya ya Kimataifa kuendelea kuisadia Sudan ya Kusini katika kutafuta ufumbuzi wa kudumu katika mgogoro ulioikumba nchi hiyo.
Akichangia kuhusu mageuzi ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Makamu wa Rais alisema Tanzania kwa ujumla inaunga mkono msimamo wa Afrika wa kuwa na viti viwili katika baraza hilo na kura ya turufu bila ya masharti yoyote.Wakati wa ufunguzi wa mkutano huo viongozi walisisitiza suala la kuimarisha umoja baina ya nchi wanachama na kusema hiyo ndiyo nguzo muhimu katika kukuza uchumi na ustawi wa wananchi wa Bara la Afrika.
Katika mkutano huo kulikuwa na uzinduzi wa pasi ya kusafiria ya Afrika ambayo ilitolewa kwa Mwenyekiti wa AU, Rais Idris Deby wa Chad na nchi mwenyeji wa mkutano, Rais Paul Kagame wa Rwanda.Mkutano huo ambao ulizungumzia pia gharama za kuendesha umoja huo na masuala ya haki za wanawake ulihudhuriwa na Wakuu wa Nchi zaidi ya 35, Marais wastaafu, wake wa Marais pamoja na viongozi wa serikali.
Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais.
Toa Maoni Yako:
0 comments: