Wajumbe wa Kamati ya Fedha Halmashauri ya Mji Njombe wakiwa wamesimama Nje ya jengo la zahanati ya Utalingolo iliyopo katika Kijiji cha Utalingolo ambayo ipo katika hatua za umaliziaji. Wa kwanza kulia ni Mwandisi wa Halmashauri Eng. Ibrahim Mkangalla.
Wajumbe wa Kamati ya Fedha Halmashauri ya Mji Njombe wakipata ufafanuzi juu ya ujenzi wa stand mpya ya Mabasi inayofadhiiliwa na Benki ya Dunia kupitia Mradi wa kukuza na kuendeleza Miji (ULGSP), mradi ambao unatekelezwa kwenye Halmashauri 18 Nchini.
Ujenzi wa Jengo la vyumba 04 vya madarasa unaoendelea katika Shule ya Sekondari Mgola.

Na Hyasinta Kissima - Njombe

Halmashauri ya Mji Njombe imetoa jumla ya shilingi milioni 128 kwa mwaka wa fedha 2015/2016 ili kukamilisha ujenzi wa zahanati na ununuzi wa vifaa vya zahanati kwenye jumla ya zahanati 12 zilizopo kwenye Halmashauri hiyo.

Akitoa ufafanuzi kwenye ziara ya ukaguzi wa miradi iliyofanywa na Kamati ya fedha ya Halmashauri, Mchumi wa Mji Njombe Ndugu Shigela Ganja amesema kuwa fedha hizo zilitolewa ziliambatana na maelezo ya kuhakikisha kuwa zinamalizia shughuli za ujenzi ili kuhakikisha kuwa zahanati hizo zinaanza kutoa huduma kwa wananchi haraka iwezekanavyo na kupunguza adha ya Wananchi hususani waliopo maeneo ya Vijijini ambapo huduma za afya zimekuwa ni za tabu.

Akifanya majumuisho ya ukaguzi wa miradi kwa upande wa Zahanati, Mwenyekiti wa Halmashauri Mheshimiwa Mwanzinga amesema kuwa miongoni mwa Zahanati ambazo Kamati yake imezikagua zinaridhisha ingawaje usimamizi wa karibu zaidi unahitajika ili kuhakikisha fedha ambazo halmashauri imezipeleka zinatumika kwa mujibu wa maelekezo na zinakamilika kwa wakati.

“Lengo la kuzisimamia Zahanati hizo ni kuhakikisha kuwa mpaka kufikia mwaka 2017 Majengo yote ya zahanati zilizokwisha patiwa fedha zinaanza kutoa huduma kwa Wananchi kama tulivyoahidi katika Kampeni za uchaguzi. Kuna Kata ambazo licha ya Zahanati zake kupatiwa fedha na

Halmashauri tangu mwezi Mei mpaka sasa, fedha hizo bado zipo kwenye Akaunti na Diwani wa kata husika yupo kimya. Zahanati hizo zinakuwa kero si kwa Kamati yangu bali hata kwa wale wananchi wa maeneo husika kwani zinakuwa za muda mrefu na bado ujenzi wake unakua hauna matumaini kwa Wananchi wa eneo husika.

Nawataka Waheshimiwa Madiwani washirikiane na Wataalamu katika usimamizi wa Zahanati hizo”

Aidha Mwanzinga ameitaka Halmashauri kuwaandikia madiwani wasiofahamu majukumu yao barua ya kuwakumbusha majukumu yao ya kazi kwani moja kati ya jukumu la diwani ni kufanya usimamizi wa miradi inayoendelea ndani ya Kata yake na kuitolea taarifa kwenye vikao mbalimbali vya Kisheria pale panapokuwa na changamoto inayokwamisha mradi husika kutokabidhiwa kwa Wananchi kwa wakati.

Nae mjumbe wa Kamati ya fedha wa Halmashauri Filoteus Mligo ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Lugenge amesema kuwa ni vyema Halmashauri itoe vipaumbele vya zabuni kwa wakandarasi ambao wanamaliza kazi zao kwa ubora na kwa wakati ili kuhakikisha kuwa miradi ya Halmashauri inakamilika kwa wakati.

Mheshimiwa Mligo ameongezea kuwa ni jukumu la Waheshimiwa Madiwani kuhakikisha wanawahamasisha wananchi wa Kata zao kuendelea kuchangia shughuli mbalimbali za maendeleo ili miradi hiyo iweze kukamilika kwa wakati badala ya kuitegemea serikali pekee.

Miradi mingine iliyotembelewa na Kamati hiyo ni pamoja na ujenzi wa madarasa, ujenzi wa stand mpya ya mabasi, ujenzi wa vyoo na ujenzi wa nyumba za kulala waalimu katika shule za sekondari.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: