TAARIFA KWA UMMA KUTOKA KWA MSTAHIKI MEYA BONIFACE JACOB
Asalaam aleikum wananchi wa wilaya ya kinondoni na viunga vyake, niendelee kuwaombea ndugu zetu waislamu funga yao iwe na heri na baraka tele ikiwa leo ni chungu cha 19.
Leo tarehe 25 june 2016, nimepigiwa simu nyingi sana na kupokea taarifa kwa njia mbalimbali, nikiulizwa nilipo? kwanini sipo kwenye tukio la Biafra la uzinduzi wa shughuli ya jeshi la polisi? na wengine wakiniuliza neno baada ya kuuliziwa hadharani na mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania.
MHESHIMIWA RAIS John pombe Magufuli; Mstahiki meya manispaa ya Kinondoni leo siku ya jumamosi kijana wako na mtumishi wa wananchi wa manipsaa ya Kinondoni nilikuwa naunga mkono shughuli za usafi. Nimeshinda na wananchi wa ubungo kisiwani kutwa tukifukua mitaro ya maji machafu kuhakikisha usalama wa afya za Ubungo kisiwani zipo salama na zaidi kuweka miundo mbinu yetu sawa.
Nami nilitamani sana kukuona japo kwa karibu sana au kuongea na wewe mambo kadhaa kwa mustakabali wa kinondoni yetu na nchi yetu kwa ujumla, hasa hali ya kisiasa na kiuchumi ili kurahisisha upatikanaji wa Maendeleo.
Mheshimiwa Rais leo nadhani umejionea mahusiano yenye shaka na mabaya niliyokuwa nalalamikia siku zote kwa njia mbalimbali. Viongozi wa wilaya na mkoa hatuna tena ukaribu wakupashana wala kutaarifiana habari yoyote,
iwe nzuri au mbaya.
Mheshimiwa Rais, meza kuu ilipaswa kukwambia ama kukupa jibu kuwa sikuwa na mwaliko leo wa kuhudhuria shughuli hiyo hakuna kiongozi wa polisi yeyote, awe IGP, RPC, OCD wala OCS aliyenipigia simu au kunitumia ujumbe wa aina yeyote kuwa nikaribie tukio lako la leo. Hakuna mjumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa wala wilaya aliye nitumia ujumbe wa aina yeyote au kinipigia simu akinijulisha au kuniomba nikaribie kwenye tukio lako leo.
Mheshimiwa Rais; shughuli za ulinzi na usalama zina taratibu zake, na mimi mstahiki meya wa Kinondoni siyo mjumbe wa kamati ya ulinzi, kuanzia mtaa, kata, wilaya mpaka mkoa. Hivyo ni ngumu sana kujua shughuli hizo wala kuhusishwa kama haujapewa taarifa na wahusika walioandaa ujio wako na uzinduzi wa leo.
Mheshimiwa Rais, binafsi nilichukulia kwa uzito kuwa sihitajiki mahala hapo kwakuwa tukio lako la leo nilishatoa ushirikiano kabla ya kuona sina mualiko, kwakuwa greda la kusafisha na kuandaa eneo la tukio lako nili idhinisha mimi na kuhakikisha polisi wanapatiwa kutoka kwa wananchi wa kata ya Goba lilipo kuwepo likikwangua barabara.
Baada ya ombi lao la greda kufanikiwa kusafisha vizuri, Juzi siku ya alhamisi, karani wangu alipokea barua maalum yenye malekezo maalumu yakitaka madiwani watano waje kwemye shughuli hiyo. Barua hiyo maalumu yenye mihuri ya siri niliitekeleza kwa kuteua madiwani watano tena kutoka kwenye kamati ya fedha,nilijua ni taratibu tu za kiusalama, ambapo leo walihudhuria. Laiti barua hiyo ya polisi ingenitaja tu au kama ningetumiwa barua yangu binafsi basi ningehudhuria tukio hilo bila shaka.
Mheshiwa Rais, binafsi nimeshindwa kulielewa Jeshi la Polisi kama ulivyoshindwa kunielewa mimi, kwakuwa bado ninaamini kuwa pamoja na makandokando ya kisiasa yaliyopo walipaswa kunialika. Si mimi tu, bali pamoja na viongozi wengine wa upinzani kwakuwa zoezi hili lilikua ni lakitaifa.
Mheshimiwa Rais nimalize kwa kusema kuwa laiti ningepata mualiko ningefika kwa heshima yako kwakuwa naamini bado Kinondoni inahitaji mahusiano bora baina ya manispaa ya Kinondoni na serikali kuu. Jambo la leo lilitawaliwa na baadhi ya watendaji kusutwa na dhamira zao, kuona ningekaaje meza kuu mimi meya wa upinzani, ndiyo maana sikuwa meza kuu na kiti changu, wala rasimu ya ratiba hainitaji popote wala kunipa walau nafasi ya kusalimia, ukiondoa nia yako njema binafsi ya kunitambua, kwao waliona sistahili na hakuna haja hiyo ya kuapata wasaa au heshima wakati wamejipa kazi kuua demokrasia ambapo mimi ni tunda la siasa za vyama vingi.
Mheshimiwa Rais, binafsi nina historia ngumu sana ya kuonja machungu ya Jeshi la Polisi kama walivyo wapinzani wote. Ila kwenye maendeleo wakinihitaji wakati wowote, nitatoa ushirikiano wangu kwa nguvu na akili zote, ndiyo maana tumekuwa tukisisitiza *polisi wasitupige mabomu CHADEMA ni serikali ijayo*.
ASANTENI,
IMETOLEWA TAR 25/6/2016
NA MSTAHIKI MEYA WA MANISPAA YA KINONDONI: BONIFACE JACOB
Toa Maoni Yako:
0 comments: