Nimesikia watu wengi wakijiuliza hili swali baada ya rais mstaafu kutumia maneno kama pumbavu na ujinga na wametoa mitazamo yao tofauti. Na mimi nimeona nichangie kidogo.
Neno linaleta maana kulingana na mahali na namna litakapotumika (context) na pia lengo au nia ya mtumiaji. Ninaweza nikasema "toka hapa" kwa wakati fulani na kwa upole bila kuwa tusi (kama utani) ila wakati mwingine likawa tusi (kukufukuza Kama mbwa kwa dharau) Kwa kutazama context hii BM alipokuwa akizungumza inajidhihirisha lengo lake ilikuwa kuwashusha hadhi/kuwadharau/kuwafanya wapinzani waonekane wasio na maana na wenye ufikiri mdogo aubufinyu wa mawazo . Kwa upande mmoja hii inaweza kuwa kama tusi. Lakini kwa upande mwingine tunaweza kusema ni kawaida ya siasa.
Nikiwa katika neutral ground ninachojiuliza ni kwamba kama ni siasa tu au kweli tusi inatuambia nini kuhusu sera na tactics za CCM katika uchaguzi huu? Kama chama ambacho ni kikongwe kinatakiwa kionyeshe uzoefu/ukomavu wake wa kisiasa na si kuwa frustrated na wapinzani. Inaonyesha wapizani wanacheza karata zao sawa na wanaanza kuichachafya CCM kana kwamba wanaacha kunadi misingi ya chama na kuanza kujiingiza kwenye malumbano na kutukanana.
Pia, nisingeshangaa sana kama hayo maneno yangetoka kwa vijana wadogo kwenye chama. Lakini kutoka kwa Mkapa, raisi msataafu ambaye tunamchukulia kama mzee wa taifa na mlezi wa chama tawala inashangaza. Inaonyesha kwamba ukuta wa CCM sasa umeanza kupata nyufa kuanzia kwenye msingi wake.
Wanatakiwa wajirudi na kulengesha nguvu zao katika kuwaonyesha Watanzania sera yao ina mipango gani ya kukibadilisha chama ili kiwe kinaenda na nyakati za sasa (remain relevant) ili kuleta maendeleo kwa kasi zaidi.
Watanzania wamechoka ufisadi uliokithiri ambao umelelewa na chama na wanataka mfumo mpya kwenye chama na serikali wenye uwezo wa kuleta mabadiliko ya haraka kwenye kukuza uchumi wa taifa na kuwapa wananchi huduma bora za kijamii, kuimarisha miundo mbinu na kuwapa nafasi sawa kila mmoja ili aweze kujiinua kiuchumi. Wananchi hawaamini kama mabadiliko hayo wanaweza kuyaona ndani ya CCM na ndiyo maana wanataka kuyatafuta nje ya CCM.
Hivyo CCM inatakiwa ilenge kwenye kuwaonyesha wananchi uwezo wakuleta hayo mabadiliko kwa kuanza kujikarabati na si kutupiana matusi na wapinzani. Wanatakiwa waonyeshe mabadiliko ndani ya chama ambayo yataleta mabadiliko kwenye taifa. Wakiweza hilo basi hawatahitaji hata kujibizana na wapinzani.
Ni mimi mwananchi wa Kawaida... Shabda Shalua - Mwanza.



Toa Maoni Yako:
0 comments: