NAIBU WAZIRI – ELIMU OFISI YA WAZIRI MKUU - TAMISEMI, Mhe. Kassim Majaliwa akiongea na waandishi wa habari kuhusu taarifa za wanafunzi waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza kwa mwaka 2015. Mkutano huo umefanyika leo Disemba, 2014 jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu wa TAMISEMI, Zuberi Samataba na Mkurugenzi wa Elimu (Uratibu), Bernard Makali.
---
OFISI YA WAZIRI MKUU TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA
TAARIFA YA SERIKALI KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU WANAFUNZI WALIOCHAGULIWA KUJIUNGA KIDATO CHA KWANZA MWAKA 2015

1.0      Utangulizi

Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi ulifanyika kuanzia tarehe 10 hadi 11 Septemba, 2014. Kwa mara ya tatu watahiniwa walifanya mtihani huo kwa kutumia Teknolojia mpya ya  “Optical Mark Reader-(OMR)” ambapo mitihani inasahihishwa kwa kutumia Kompyuta.

2.0      Usajili wa watahiniwa
Jumla ya wanafunzi 808,085 wa shule za msingi walisajiliwa kufanya mtihani huo wakiwemo wasichana 429,624 sawa na asilimia 53.16 na wavulana 378,461 sawa na asilimia 46.83. Watahiniwa 792,122 sawa na asilimia 98.02 ya waliosajiliwa walifanya mtihani. Kati yao wasichana walikuwa 422,625 sawa na asilimia 98.37 na wavulana walikuwa 369,497, sawa na asilimia 97.63. Watahiniwa 15,963 sawa na asilimia 1.98 hawakufanya mtihani kutokana na sababu mbalimbali, zikiwemo utoro, vifo na ugonjwa. Kati yao  wasichana ni 6,999, sawa na asilimia 1.63 na wavulana  ni 8,964 sawa na asilimia 2.37

3.0 Matokeo ya Mtihani
Matokeo ya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi yanaonesha kuwa alama ya juu kabisa kwa wavulana ilikuwa 243 na kwa wasichana ni 240 kati ya alama 250. Mwaka 2013 alama ya juu ilikuwa 244. Upande wa ufaulu matokeo ya mtihani yanaonesha kuwa jumla ya wanafunzi 451,392 (wavulana 224,909 na wasichana 226,483) walifaulu kwa kupata alama A – C kati ya wanafunzi 792,122 waliofanya mtihani huo; hii ni sawa na asilimia 56.98. Hili ni ongezeko la asilimia 6.37 la ufaulu ikilinganishwa na ufaulu wa asilimia 50.61 katika mwaka 2013.  Aidha, jumla ya wanafunzi 10,331 walipata alama za daraja la A, wakati wanafunzi 98,789 walipata daraja la B. Jumla ya wanafunzi  342,272 walipata alama za daraja la C; wanafunzi 321,939 walipata alama za daraja la D na watahiniwa waliobaki 18,787 walipata alama E.  Alama kikomo kwa ajili ya kuchagua wanafunzi watakaojiunga na Kidato cha Kwanza kwa mwaka huu imeishia daraja la C.
4.0 Uchaguzi wa Wanafunzi wa Kuingia Kidato cha Kwanza 2014
Kufuatia ongezeko la fursa za utoaji wa Elimu ya Sekondari nchini, wanafunzi 438,960 kati ya 451,392 waliofaulu mtihani wamechaguliwa kujiunga Kidato cha Kwanza katika shule za sekondari za Serikali katika awamu ya kwanza. Idadi hiyo ni sawa na asilimia 97.23 ya wanafunzi waliofaulu mtihani. Aidha, kati ya wanafunzi hao waliochaguliwa, wasichana ni 219,996 sawa na asilimia 97.1 na wavulana  ni 218,964 sawa na asilimila 97.28. Takwimu hizi zinaonesha pia kwamba idadi ya wanafunzi walichaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza imeongezeka kwa asilimia 1.08 ikilinganishwa na asilimia 96.3 ya wanafunzi waliochaguliwa awamu ya kwanza mwaka 2014.

5.0      Udanganyifu katika mtihani
Takwimu zinaonesha kuwa idadi ya watahiniwa waliofutiwa matokeo kutokana na kujihusisha na vitendo vya udanganyifu katika Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi, 2014 imepungua. Kwani waliofutiwa matokeo mwaka 2014 ni watahiniwa 4 ikilinganishwa na wanafunzi 13 waliofutiwa matokeo yao kwa udanganyifu mwaka 2013 .

Kufuatia  udanganyifu huo, Serikali itawabaini wale wote waliohusika katika udanganyifu huo na kuwachukulia hatua stahiki ,nia ni kukomesha kabisa udanganyifu.
6.0 Hitimisho
Napenda kuchukua nafasi hii kuwapongeza wanafunzi waliochaguliwa kujiunga Kidato cha Kwanza katika shule za Sekondari. Pia nawashukuru Walimu, Walimu Wakuu, Kamati za Shule, Waratibu Elimu Kata, Viongozi wa Halmashauri na Wadau wa Elimu nchini kwa kutoa ushirikiano katika kusimamia uendeshaji na utoaji wa Elimu bora Nchini. Napenda kuwaasa wanafunzi wote waliochaguliwa kutumia fursa hii vizuri katika kujifunza. Aidha, ninawaagiza walimu na watendaji wa elimu katika ngazi zote kuongeza bidii katika usimamiaji na ufuatiliaji wa utoaji wa elimu ili kuboresha elimu nchini.
Natoa wito kwa Halmashauri wakishirikiana na wadau wote wa elimu kukamilisha majengo na kuandaa mazingira ya kuwapokea wanafunzi wote waliochaguliwa kuanza Kidato cha Kwanza mwaka 2015. Ninawahimiza, wazazi, walezi na jamii kushirikiana na uongozi wa wilaya, Halmashauri na shule, kuhakikisha kwamba wanafunzi wote waliochaguliwa wanaandikishwa, wanahudhuria na kubakia shuleni hadi watakapohitimu elimu ya Sekondari.
Aidha, ninaziagiza Halmashauri zilizobakiza wanafunzi 12,432 katika awamu ya kwanza ya uchaguzi katika mikoa ya Dodoma (9824), Dar es Salaam (1414), Morogoro(752), Mtwara ( 281) na Katavi ( 161) kukamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa  ili kuwawezesha wanafunzi hao kujiunga na Kidato cha Kwanza ifikapo mwezi Machi, 2015. 

Asanteni kwa kunisikiliza.

Mhe. Kassim Majaliwa (Mb)
 NAIBU WAZIRI – ELIMU
OFISI YA WAZIRI MKUU - TAMISEMI
Disemba, 2014
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: