Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
KUNDI la ngoma za asili lenye kupendwa na wengi jijini Dar es Salaam linalojulikana kama Naukala Ndima, limejipigia debe likisema lina hamu kubwa ya kufanya kazi ya maana katika tamasha la Handeni Kwetu, litakalofanyika Desemba 13, mwaka huu wilayani Handeni, mkoani Tanga.
Pichani ni Mkurugenzi wa kundi hilo, Fadhili Lugendo maarufu kama Koka Star anayecheza tumbo wazi akiwajibika.
Tamasha hilo linalosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa matukio makubwa ya sanaa na burudani linafanyika kwa msimu wa pili, baada ya kuzinduliwa rasmi mwaka jana Desemba 14 na kuhudhuriwa na wengi.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa kundi hilo, ambaye ni miongoni mwa wasanii wa ngoma za asili, Fadhili Lugendo, maarufu kama ‘Koka Star’, alisema kuwa wamelipania tamasha hilo kwasababu wanafahamu linavyopendwa na wengi mkoani Tanga na Tanzania kwa ujumla kutokana na kuandaliwa vizuri.
Alisema kuwa tamasha la mwaka jana lilikuwa zuri na kuwapatia mafanikio makubwa kutokana na mikataba mingi waliyoipata, ukiwapo ule unaohusisha wao na televisheni ya CTN iliyowapa haki ya kurusha vipindi vya utamaduni wa Tanzania.
“Baada ya kusikia waandaaji wa tamasha hilo wamejipanga tena kufanya tukio hilo mwezi Desemba mwaka huu, tunapata shauku ya kuomba na sisi tuwe miongoni mwa makundi kutoka nje ya mkoa wa Tanga tutakaoshiriki.
“Nikiwa kama msanii wa ngoma za asili natambua matamasha makubwa kama haya ndio yanayoweza kutangaza sanaa yetu pamoja na kukuza utamaduni wa Mtanzania, hivyo endapo tutapewa mwaliko wa kuelekea Handeni, hakika tutafanya kazi ambayo haitasahaulika,” alisema.
Naukalanda Ndima ni miongoni mwa makundi kutoka nje ya Handeni, mkoani Tanga yaliyopata fursa ya kuonyesha sanaa yao mwaka jana kwenye tamasha hilo linaloandaliwa chini ya Mratibu wake Mkuu Kambi Mbwana.
Toa Maoni Yako:
0 comments: